Kimya cha kufikirisha cha Waziri Mkuu wa India mbele ya mauaji ya Wahindu dhidi ya Waislamu

Zaidi ya Waislamu 3000 wamekimbia makazi yao katika mji wa Gurugram katika jimbo la Haryana, wakihofia kushambuliwa na Wahindu wenye misimamo ya kufurutu ada. Maduka ya Waislamu katika mji huu pia yamefungwa.

Kukimbia nyumba na makazi yao Waislamu kumetokea baada ya watu saba kuuawa katika mapigano katika mji wa Gurugram, na Waislamu hao wameamua kuondoka katika mji huo na kufunga milango ya nyumba na maduka yao ili kuokoa roho na maisha yao.

Kwa kuzingatia historia ya kutisha ya mashambulizi ya Wahindu wenye itikadi kali dhidi ya Waislamu katika maeneo tofauti ya India, yakiwemo majimbo ya Gujarat na Uttar Pradesh na hata katika mji mkuu  New Delhi, hofu ya Waislamu wa Gurugram ya kutekelezwa mara hii hujuma za umwagaji damu  za Wahindu hao  katika jimbo la Haryana siyo ya bure. Kim Singh Yadav mtaalamu wa masuala ya kisiasa anasema:

Swali la kimsingi ambalo linaulizwa katika jamii yenye  kaumu na dini mbalimbali nchini India ni je, watu wa nchi hii wanapaswa kutangatanga katika nchi yao hadi lini? Sio Waislamu pekee, bali pia watu wengine walio wachache hawako salama kutokana na mashambulizi ya watu wenye itikadi kali na daima wananyanyaswa.

“Hasa katika majimbo ambayo chama tawala chenye mielekeo ya Kihindu cha BJP kina nguvu ambapo watu wenye msimamo mkali wanatumia  hiyo kama fursa ya kuwanyanyasa na kuwashambulia Waislamu.”

Ghasia na vitendo vya utumiaji mabavu vilizuka katika mji wenye Waislamu wengi wa Gurugram katika jimbo la Haryana mnamo Julai 31 baada ya mapigano kati ya Waislamu Wahindu na wenye misimamo ya kufurutu ada.

Licha ya juhudi za jeshi la polisi la India kudhibiti machafuko hayo; lakini mashambulizi machache ambayo kimsingi yanawalenga Waislamu yangali yanaendelea.

Lakini kile kinachoonekana kuwatia wasiwasi zaidi Waislamu wa India hususan Waislamu wa Gurugram ni kushindwa kwa wapinzani wa Waziri Mkuu wa India Narendra Modi kupiga kura ya kutokuwa na imani naye. Kimya cha “Modi” dhidi ya jinai za Wahindu wenye itikadi kali katika jimbo la kaskazini mashariki la Manipur kimesababisha dhana miongoni mwa watu wa India, hususan Waislamu, kwamba makundi yenye itikadi kali ya RSS na Shiv Sena yanawashambulia Waislamu kwa nguvu na yakiwa yanajiamini zaidi kwani hakuna baya linalowapata kwa hujuma na vitendo vyao hivyo.

Hii ni katika hali ambayo, mzozo wa kikaumu ungali unaendelea huko Manipur, na Wahindu wenye misimamo mikali hawana wasiwasi kuhusu kuzidisha vita vya kidini huko Gurugram, na kwa hakika hilo ndilo lililowafanya Waislamu kuondoka katika mji huo na kuacha nyumba na maisha yao.

Ali Alai, mweledi na mchambuzi wa masuala ya India anasema kuhusiana na hilo kwamba:

Nguvu ya makundi vya Wahindu wenye misimamo mikali nchini India inafuata nguvu ya chama tawala cha Bharatiya Janata chenye muelekeo wa Kihindu. Mintarafu hiyo, kutoweza mrengo wa upinzani katika Bunge la India kupitisha kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu Narendra Modi kwa sababu ya kimya chake dhidi ya uhalifu unaoendelea katika jimbo la Manipur, bila shaka hilo litawafanya Wahindu wenye itikadi kali kuwa na ujasiri zaidi katika kuendeleza jinai zao katika maeneo mbalimbali ya India. Hapana shaka kuwa, hali hiyo itafanya jamii ya India iendelee kuwa na wasiwasi kuhusu kuibuka unyanyasaji wa kikaumu na kidini unaofanywa na Wahindu wenye msimamo mkali.

Vyovyote iwavyo, kurusha mawe, kuchoma moto maduka na kubmoa makaburi ya Waislamu katika vitongoji duni na vya masikini huko Gurugram katika jimbo la Haryana na kuwalazimisha mamia ya Waislamu kuacha nyumba na maduka yao, kwa hakika si ujumbe mzuri hata kidogo kwa jamii ya watu wengi wa kaumu na dini mbalimbali nchini India.

Hata hivyo kinachoibua wasiwasi zaidi katika nchi hiyo ni ukimya wa Waziri Mkuu Narendra Modi na viongozi wengine wa BJP dhidi ya jinai  za Wahindu wenye misimamo mikali, kwa sababu yeye na viongozi wengine wa chama cha Bharatiya Janata wana wanahofia kupoteza himaya na uungaji mkono wa Wahindu wenye misimamo mikali hususan makundi ya RSS na Shiv Sena katika uga wa kisiasa wa India, ambapo katika maeneo ya mbali na vijiji na miji midogo chama hicho kimeendelea kuungwa mkono kutokana na ushajiishaji wa Wahindu hao wenye chuki na Uislamu.

Kwa msingi huo, wananchi wa India wanataraji kuona kunakuweko na uingiliaji madhubuti wa Waziri Mkuu na serikali kuu ya India katika matukio ya hujuma na vitendo vya utumiaji mabavu dhidi ya Waislamu vinavyofanywa na Wahindu wenye misimamo ya kufurutu ada katika katika maeneo mbalimbali likiwemo jimbo la Haryana, na hivyo kurejesha amani na usalama katika nchi. Hii ni kwa sababu kuendelea kwa migogoro ya kikaumu kunaweza kuwa na matokeo mabaya na haribifu kwa usalama wa taifa wa India.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *