Kiongozi Muadhamu asisitizia udharura wa kuondolewa udhaifu wa kiutamaduni

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, Baraza Kuu la Mapinduzi ya Kiutamaduni la Iran lina wajibu wa kutambua kwa kina udhaifu na mapendekezo ghalati ya kiutamaduni katika nyuga tofauti na kuzipatia ufumbuzi wa kiutaalamu kwa ajili ya kueneza utamaduni wa kuwa na mapendekezo sahihi na ubunifu unaofaa.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei alisema hayo jana wakati alipoonana na wajumbe wa Baraza Kuu la Mapinduzi ya Kiutamaduni la Iran na kusisitiza kuwa, kuongoza vizuri masuala ya kiutamaduni humu nchini  ndiyo hadhi na kazi kuu ya baraza hilo. Aidha amehimiza kujengwa upya na kwa sura ya kimapinduzi; muundo wa kiutamaduni humu nchini.

Amegusia utamaduni ghalati wa “Hatuwezi” uliokuwa umetawala katika jamii ya Iran kabla ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na kusema, Mapinduzi ya Kiislamu yameweza kuvunja pole pole utamaduni huo ghalati katika akili za watu kwa kupitia ujenzi wa nchi na harakati ya kiubunifu na matokeo yake ni kwamba, taifa la Iran limeweza kufanya kazi kubwa katika ujenzi wa mabwawa, vinu mbalimbali, mabarabara makubwa, vifaa vya viwandani na kazi nyingine kubwa na muhimu za kuimarisha miundombinu kwa kutumia vijana wake wenye utaalamu wa fani mbalimbali.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiisalmu amezungumzia utamaduni mwingine ghalati wa kupenda Umagharibi na hata kutumia misamiati ya lugha za kigeni kama lugha ya Kifaransa kwa mfano kuwa ni mbinu nyingine mbaya iliyokuwa imetawala katika jamii ya Iran lakini Mapinduzi ya Kiislamu yameweza kubadilisha utamaduni huo na kuufanya kuwa ni wa kupinga Umagharibi.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei vile vile amesema, Mapinduzi ya Kiislamu yameweza kubadilisha utamaduni ghalati wa kujiona na kupenda umaarufu na kuufanya kuwa utamaduni wa kujitolea kwa ajili ya wengine akisisitiza kuwa, huo ni mfano mwingine wa taathira sahihi za utamaduni wa Mapinduzi ya Kiislamu katika maisha binafsi ya watu wa Iran.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *