Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kipaumbele katika sera za kigeni za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hivi sasa ni kuimarisha uhusiano na mataifa jirani.
Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema hayo leo katika mazungumzo yake na Rais Serdar Berdimuhamedow wa Turkmenistan na kuongeza kuwa: Kuimarisha uhusiano wa pande mbili na pande kadhaa na majirani ni kipaumbele cha sera za kigeni za Iran, na sera hii ni mzuri na sahihi mno.
Ayatullah Ali Khamenei amesema kupanuliwa uhusiano wa pande mbili wa Iran na Turkmenistan ni kwa maslahi ya mataifa haya mawili jirani.
Amesema irada thabiti inahitajika kwa ajili ya kuboresha uhusiano wa nchi mbili hizi, ili kuweza kuondoa vizingiti katika njia ya kuimarisha zaidi uhusiano huo.
Kiongozi Muadhamu ameeleza bayana kuwa: Bila shaka, uhusiano wa kirafiki kati ya Iran na Turkmenistan una maadui wa kieneo na kimataifa, hata hivyo visiki vilivyoko vinapaswa kuondolewa.
Amesema Kamisheni ya Pamoja ya Ushirikiano ya nchi mbili hizi inapaswa kuamilishwa, ili kukamilisha mchakato wa kufunga mikataba wa pande mbili kupitia ufuatiliaji wa kina.
Kwa upande wake, Rais Serdar Berdimuhamedow wa Turkmenistan amesema serikali yake ina azma ya kuboresha uhusiano na mataifa jirani, na inafanya kila liwezekanalo kuimarisha uhusiano na Jamhuri ya Kiislamu katika nyuga mbalimbali kama gesi, umeme, uchukuzi, sanjari na kukamilisha miradi mikubwa, kwa misingi ya makubaliano yaliyosainiwa mapema leo.
Ameashiria miaka 30 ya uhusiano wa kidiplomasia baina ya nchi yake na Iran, na kumshukuru Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa kuunga mkono kupanuliwa uhusiano wa Tehran na Ashgabat.