Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amelitaja tukio la kimiujiza la maandamano na matembezi ya Arubaini ya Imam Hussein (as) kuwa ni ishara ya irada ya Mwenyezi Mungu ya kunyanyua juu bendera ya Uislamu ya Ahlul Bayt.
Ayatullah Ali Khamenei amesema leo Jumamosi katika shughuli ya maombolezo ya wanafunzi wa vyuo vikuu kwa mnasaba wa Arubaini ya Imam Hussein kwamba: “Tukio la kimuujiza la matembezi ya Arubaini haliwezi kutekelezwa kwa sera na tadibiri yoyote ya kibinadamu; na kwa tukio hili, mkono wa Mwenyezi Mungu unaotoa ishara njema kwamba njia iliyo mbele yetu iko wazi na inaweza kupitika.”
Ayatullah Khamenei amesema, nyoyo safi na zenye imani za vijana ndio sababu ya kuongeza ubora wa dua na mawaidha na kuongezeka hidaya ya Mwenyezi Mungu na akasema: Shuguli ya Arubaini ya Imam Hussein (as) ambayo ni bendera ya juu ya Bwana wa Mashahidi, mwaka huu imefanyika kwa ufanisi zaidi na imekuwa kubwa zaidi kuliko kipindi kingine chochote katika historia.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amewausia vijana kuthamini ujana wao na kuvipa kipaumbele maalumu vikao na makundi yanayojihusisha na shughuli ya kukumbuka ya mauaji ya Imam Hussein (as) na akasema: Makundi hayo pia yanapaswa kubakisha hai kumbukumbu ya Ahlul-Bayt na kuwa kitovu na msingi wa kueleza haki na kweli.
Ayatullah Khamenei ameashiria njama zinazoendelea kufanywa na watu wenye nia mbaya na maharamia wanaopindisha haki na kweli kuhusu matukio muhimu kama vile maandamano yenye hamasa kubwa ya Arubaini ya Imam Hussein, na amewakumbusha watu wote kutekeleza wajibu wao katika uwanja huo. Amesema: Sentensi mbili muhimu na za milele za Qur’ani, yaani, himizo la kuusiana haki na lile linalohimiza kuwa na subira daima hasa katika kipindi cha sasa, ni mwongozo wa msingi.
Wakati huo huo Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameitaja Arubaini ya Imam Hussein (as) kuwa ni muujiza wa Mwenyezi Mungu na moja ya madhihirisho na vielelezo vya umoja wa Waislamu na akasisitiza kuwa: Ashura ingali hai na itaendelea kuwa hai.
Sayyid Ebrahim Raisi ameongeza kuwa: “Arubaini ya Imam Hussein inaonyesha umoja na mshikamano wa Waislamu” na kuongeza kuwa: Arubaini pia ni dhihirisho la muqawama na mapambano ya Kiislamu na inaonyesha kwamba Ashuraa bado iko hai na itabakia hai.
Leo Jumamosi, tarehe 20 Safar 1444 Hijria (17 Septemba 2022), ni siku ya arubaini tangu baada ya kuuawa shahidi Imam Hussein (AS), mjukuu wa Mtume Muhammad (saw) na masahaba zake waaminifu katika jangwa la Karbala tarehe 10 Muharram mwaka 61.
Katika siku hii ya leo mamilioni ya Waislamu kutoka pande zote za dunia, ikiwemo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, wako katika mji mtakatifu wa Karbala ulioko kusini mwa Iraq kuhudhuria shughuli hiyo ya Arubaini ya Imam Hussein (as).