Kiongozi wa mapinduzi Niger: Tuko tayari kwa mazungumzo, na vita ikilazimu

Kiongozi wa mapinduzi yaliyomuondoa madarakani Rais Mohammed Bazoum wa Niger amesema yupo tayari kufanya mazungumzo ili kuepusha mgogoro na mapigano baina ya nchi hiyo na Jumuiya Kiuchumi ya Magharibi mwa Afrika (ECOWAS) lakini anasisitiza kuwa, taifa hilo limejiandaa kujihami.

Jenerali Abdourahamane Tchiani alisema hayo usiku wa kuamkia leo katika hotuba yake kwa taifa kupitia runinga na kubainisha kuwa, wananchi wa Niger hawataki vita, na mlango wao wa mazungumzo upo wazi.

Hata hivyo ametoa onyo kali kwa kusema, “ECOWAS inajiandaa kuishambulia Niger kwa kuunda jeshi vamizi kwa ushirikiano na vikosi ajinabi. Endapo uvamizi wowote utafanyika dhidi yetu, hayatakuwa matembezi katika bustani (lele mama) kama baadhi wanavyodhani.”

Aidha Jenerali Tchiani bila kutoa maelezo ya kina, amependekeza kipindi cha mpito wa miaka mitatu kabla ya kurejeshwa utawala wa kiraia nchini humo.

Alisema hayo baada ya kufanya mkutano wake wa kwanza na ujumbe wa ECOWAS katika mji mkuu wa nchi hiyo, Niamey. Kadhalika ujumbe huo wa ECOWAS umeruhusiwa kuonana na rais Bazoum aliyepinduliwa Julai 26.

Mapema jana, wakuu wa majeshi ya Mali, Burkina Faso na Niger walikutana kujadili mkakati wa pamoja wa ulinzi, kujibu tamko la Jumuiya Kiuchumi ya Magharibi mwa Afrika la kuwa tayari kuingilia kijeshi nchini Niger.

Taharuki imetanda nchini Niger baada ya wakuu wa majeshi ya jumuiya ya ECOWAS kutangaza kuwa wameafikiana juu ya tarehe ya kuishambulia kijeshi Niger ili eti kurejesha uawala wa kikatiba.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *