Kiongozi wa upinzani nchini Tanzania Tundu Lissu kurejea kutoka uhamishoni

Kiongozi wa upinzani nchini Tanzania Tundu Lissu amesema kwamba atarejea nyumbani hivi karibuni kutoka uhamishoni baada ya rais kuondoa marufuku ya mikutano ya kisiasa.

Lissu, ambaye alipigwa risasi 16 katika jaribio la kutaka kumuua mwaka 2017 na amekuwa akiishi uhamishano nchini Ubelgiji, alihutubu kwa njia ya intaneti Ijumaa na kutangaza kuwa atarejea Tanzania Januari 25.

Hatua ya Lissu inafuatia tangazo la Rais Samia Suluhu Hassan mwezi huu kwamba marufuku ya mikutano ya kisiasa iliyowekwa na mtangulizi wake itaondolewa .

Akizungumza moja kwa moja kwenye YouTub siku ya Ijumaa, Lissu amesema, “Hatuwezi kuendelea kuishi uhamishoni bila kikomo.”

Aidha ameutaja mwaka wa 2023 kuwa mwaka muhimu katika historia ya Tanzania. Chama cha upinzani cha Chadema cha Lissu kimetangaza kuanza mikutano ya hadhara Januari 21.

Mara ya mwisho alikuwa Tanzania mwishoni mwa 2020 aliposhiriki katika uchaguzi dhidi ya Rais John Magufuli aliyekuwa akiwania muhula wa pili na ambaye alifariki miezi mitano tu baada ya kushinda katika uchaguzi huo.

Ushindi wa Magufuli ulipingwa na upinzani ulioitisha maandamano. Lissu alikimbilia katika ubalozi wa kigeni baada ya vitisho kwa maisha yake, kabla ya kutoroka nchini.

Lissu, mkosoaji mkubwa wa Magufuli na chama tawala CCM, alipigwa risasi akiwa ameketi kwenye gari lake mwaka 2017 na baada ya kupokea matibabu ya awali nchini Kenya alielekea uhamishoni nchini Ubelgiji.

Akizungumza Ijumaa, Lissu amesema, “Rais Samia Suluhu Hassan kupitia serikali yake na chama chake wameonyesha wako tayari kwa safari mpya, tunatakiwa kudhihirisha kuwa tuko tayari kwa hilo.” “Amesema anarejea Tanzania kwa ajili ya mwanzo mpya.

Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania Jumanne, Januari 3, 2023 alikutana na viongozi wa vyama 19 venye usajili kamili wa siasa nchini humo Ikulu jijini Dar es Salaam na kusisitiza kuwa, ni haki kwa vyama vya siasa kuendesha mikutano yao ya hadhara nchini humo lakini kuna wajibu wa kila mmoja na upande wa serikali kuhakikisha mikutano hiyo inafanyika salama.

Akihutubia mjumuiko huo, Rais Samia alisema, wajibu wa vyama vya siasa ni kufuata kanuni na sheria zinavyosema huku akivitaka vyama hivyo kuendesha siasa za kiustaarabu, kiungwana na bila ya matusi. Amesema ndani ya Chama chake Tawala cha CCM wanaamini katika kukosolewa na kujikosoa, kama ambavyo anaamini pia kwamba akikosolewa na kufanyia kazi changamoto ataendelea kuwa Rais. Aidha, amesema yeye haviiti vyama tofauti na CCM kama ‘Vyama vya Upinzani’ bali anaviita ‘Vyama vya Kumuonesha Changamoto’ kwani haaminini kama Watanzania wanapingana.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *