Kiswahili Sasa Kutumiwa Na AU katika Uendeshaji wa Vikao Vyao

UMOJA wa Afrika (AU) sasa utaanza kutumia Kiswahili kama moja ya lugha kuu kuendeshea kazi zake, kufuatia hoja iliyopitishwa kwenye kongamano kuu la shirika hilo Jumapili jijini Addis Ababa, Ethiopia.

Ombi hilo liliwasilishwa na Makamu wa Rais wa Tanzania, Philip Mpango (pichani), akishikilia kuwa Kiswahili kinapaswa kukwezwa hadhi na kuanza kutumika kutekelezea shughuli za kikazi za muungano huo, kwani ni miongoni mwa lugha asili zenye wazungumzaji wengi barani humo.

Kiswahili kinakadiriwa kuwa na zaidi ya wazungumzaji milioni 100 katika nchi kama Kenya, Tanzania, Uganda, DR Congo, Msumbiji, Malawi, Angola, visiwa vya Comoros (Ngazija) kati ya nchi nyingine.

Kwenye ombi lake kwa AU, Mpango alisema umefika waka – ti wa Kiswahili kukumbatiwa vilivyo na umoja huo, kwani tayari kinatumika na mashirika mengine ya kikanda kama vile Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Kiuchumi ya Mataifa ya Kusini mwa Afrika (SADC).

Vilevile, alisema kuwa mbali na matumizi yake kwa mazungumzo ya kawaida, lugha hiyo inafundishwa katika nchi nyingi barani humo na hata ughaibuni.

“Kuna haja kwa AU kuanza kukitumia Kiswahili kuendeshea majukumu yake ya kikazi. Kinyume na lugha zinazotumika, Kiswahili ni sehemu ya tamaduni za Mwafrika. Ni lugha inayotupa utambulisho kama Waafrika,” akasema.

Mwezi uliopita, Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Utamaduni, Sayansi na Elimu (UNESCO) lilitangaza mnamo Julai 7 kila mwaka kama Siku ya Kitaifa ya Kiswahili Duniani.

Ili kufanikisha juhudi hizo, Tanzania iliahidi kutoa msaada wa kifedha kusaidia utekelezaji wa mpango huo.

Wakati huo huo, Uganda na Tanzania zi – mechaguliwa kuwa wanachama wa Baraza la Umoja wa Afrika kuhusu Amani na Usalama (AUPSC).

Baraza hilo linajumuisha nchi 15 kutoka maeneo matano makuu ya muungano huo. Lengo lake kuu huwa ni kuzuia, kudhibiti na kutatua mizozo inayotokea barani.

Wanachama hao wanachaguliwa na Baraza Kuu la AU na baadaye kuungwa mkono na Kongamano Kuu la umoja huo.

Baraza hilo lilipiga kura Alhamisi iliyopita. “Uganda ilipata kura 34 kwenye raundi ya tatu ya upigaji kura. Ni shughuli iliyozivutia nchi za Tanzania na Ethiopia.

Uganda ilifanikiwa kuchaguliwa kuhudumu kwenye baraza hilo kwa miaka miwili (2022 hadi 2024) pamoja na Tanzania na Djibouti. Nchi hizo tatu ndizo zitakazowakilisha eneo la Afrika Mashariki,” ikasema Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Uganda kwenye taarifa.

Nchi nyingine zilizochaguliwa kuhudumu kwenye baraza hilo ni Tunisia (Kaskazini mwa Afrika); Cameroon, Burundi na Congo (Afrika ya Kati); Nigeria, Ghana, Gambia na Senegal (Afrika Magharibi); na Namibia, Afrika Kusini na Zimbabwe (Kusini mwa Afrika).

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *