Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Hossein Amir-Abdollahian amesema katika mazungumzo ya simu aliyofanya na mwenzake wa Uswisi Tobias Billström kwamba, nchi za Ulaya zina deni la malipo ya shukrani kwa juhudi kubwa za Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu katika kupambana na ugaidi na akabainisha kwamba: Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) liliiokoa miji mikuu ya Ulaya na mashambulizi ya DAESH (ISIS).
Katika muendelezo wa hatua zake za karibuni dhidi ya Iran na misimamo yake ya kuingilia masuala ya ndani ya Iran, Bunge la Ulaya, siku ya Alkhamisi ya tarehe 19 Januari lilipitisha mpango dhidi ya Iran na kutaka jina la Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran (IRGC), ambalo ni maarufu hapa nchini kama Sepah, lijumuishwe kwenye kile kinachotajwa kama orodha ya “kigaidi” ya Umoja wa Ulaya. Pamoja na hayo, maamuzi yanayopitishwa na Bunge la Ulaya hayana ulazima wa kutekelezwa, bali yana sura ya kimapendekezo tu kwa Baraza la Ulaya.
Wakati huo huo, ikumbukwe pia kwamba, katika miezi ya hivi karibuni nchi za Ulaya na Umoja wa Ulaya, -ikiwa ni katika mwendelezo wa kuchochea zaidi fujo na machafuko nchini Iran na kudhoofisha nguvu na uwezo wa vikosi vya kijeshi na usalama vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kuimarisha usalama- zimechukua hatua mara kadhaa za kuwawekea vikwazo makamanda wa kijeshi wa Iran; lakini licha ya hatua na njama zote hizo, kwa ung’amuzi na kuwa macho wananchi na kwa juhudi za vikosi vya ulinzi likiwemo Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu, amani na usalama vimerejea katika miji mbalimbali ya Iran.