Kadiri jibu la Iran kwa kitendo cha kigaidi cha utawala wa Kizayuni wa Israel linavyozidi kuchukua muda mrefu, ndivyo taathira za kimaada, kiroho na kisaikolojia zinavyozidi kuongezeka na kuwaumiza Wazayuni.
Kuhusu wakati wa jibu la Tehran kwa utawala wa Israel baada ya kuuawa shahidi Ismail Haniyeh, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Hamas, mwakilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa ametangaza kwamba: Jibu la Iran pengine litakuwa katika wakati, mazingira na kwa namna isiyotarajiwa na utawala huu.
Wasiwasi na mkanganyiko wa kinafsi wa Wazayuni unazidi kuongezeka siku baada ya siku kutokana na jibu la uhakika la Iran kwa mauaji ya hivi karibuni ya Shahidi Ismail Haniyeh akiwa mgeni mjini Tehran, na pia majibu ya harakati ya Muqawama kwa mauaji ya Shahidi Fuad Shukr, aliyekuwa mmoja wa makamanda wa harakati Hizbullah ya Lebanon.
Baada ya mauaji ya kigaidi ya Ismail Haniyeh na Fuad Shukr, maafisa wakuu wa mhimili wa mapambano walitangaza kwamba watalipiza kisasi cha damu za mashahidi hao kutoka kwa utawala wa Kizayuni wa Israel.
Redio ya utawala wa Kizayuni wa Israel imekiri kuwa baada ya kuuawa shahidi Haniyeh, Wazayuni wanasubiri majibu ya operesheni hiyo ya mauaji kwa wasiwasi mkubwa. Ikiashiria barabarani zisizo na watu na wasiwasi unaotawala nyuso za Wazayuni, redio hiyo imefananisha hali hiyo na ile ya kipindi cha mambukizi ya Corona.
Vyombo vya habari vya Kizayuni pia vinazungumzia kuvurugika shughuli za vivuko na viwanja vya ndege, kusitishwa safari nyingi za ndege na mkanganyiko wa abiria huko Israel. Idara za ujasusi za utawala huo pia zinajaribu kupata habari za aina, shabaha na wakati wa shambulio la kulipiza kisasi la Iran na kambi ya Muqawama kwa msaada wa washirika wake.
Udhaifu wa kiuchumi, kijeshi, kiusalama, mitandao na wa kijasusi wa utawala wa Kizayuni katika kivuli cha jibu la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Hizbullah na Mhimili wa Muqawama unazidisha wahka na wasiwasi wa Wazayuni. Mbali na changamoto za kijeshi, kiusalama, kiintelijensia na kadhalika, utawala wa Kizayuni wa Israel unakabiliwa na matatizo ya kiuchumi kutokana na vita, hasa oparesheni za jeshi la Yemen katika Bahari Nyekundu, Bahari ya Hindi na Bahari ya Arabia. Uchumi uliokumbwa na mgogoro wa Israel umeingia katika kipindi kipya cha shaghalabaghala na mchafukoge kutokana na vita vya Gaza.
Leo hii, kwa kutilia maanani vita vya Gaza na mlingano mpya wa baharini uliowekwa na Yemen dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel, hakuna meli yoyote inayoruhusiwa kuingia na kutoka kwenye maeneo ya utawala huo kupitia njia ya Bab al-Mandab, hadi mzingiro wa Gaza utakapoondolewa, na chakula, dawa na mahitaji mengine ya kimsingi yakaruhusiwa kuingia eneo hilo.