MASHEHA wa Mkoa wa Mjini Magharibi, wameelezwa kuwa na wajibu wa kuwasimamia wamiliki wa majengo katika shehia zao kuhakikisha wanalipa kodi hiyo ili serikali iweze kupata fedha kwa ajili ya shughuli za kimaendeleo.
Mkuu wa wilaya ya Magharibi ‘B’ Hamida Mussa Khamis alieleza hayo wakati akifungua kikao kazi kwa masheha kwa wilaya tatu za Mkoa wa Mjini Magharibi katika ukumbi wa ZSSF Kariakoo.
Alisema masheha ni viongozi na wasimamizi wa serikali kwenye mamlaka za tawala za mikoa hivyo wana wajibu mkubwa wa kuendelea kuelimisha jamii juu ya umuhimu wa ukusanyaji wa mapato na wajibu wa kuendelea kuhakikisha kila kodi ambayo serikali imeianzisha basi inalipwa kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa.
Aidha alisema hakuna mtu asiefahamu umuhimu wa kodi hivyo masheha wana wajibu huo kuona kila anaestahili kulipa kodi hiyo kwa nafasi yake basi anawajibika kufanya hivyo.
Alibainisha kwamba masheha makatibu tawala ndio nyenzo muhimu ya kuhakikisha mapato yanapatikana na sio kwa utashi bali sheria kwa mujibu wa sheria ilivyoelekeza.
“Tuendelee kutimiza wajibu wetu kuwepo kwetu hapa ni wajibu wetu wa kukumbushwa kulisimamia jambo hilo na hili linatokana na ZRA kuona sisi wakuu wa wilaya, makatibu tawala na masheha ndio nyenzo muhimu ya kuwasaidia kutekeleza wajibu wao wa msingi kuhakikisha mapato haya yanakusanywa,” alisisitiza.
Mbali na hayo, aliwasisitiza kuwa mstari wa mbele kuhakikisha majengo hayo yote yaliyobainishwa katika sheria yanayotakiwa kulipa kodi hiyo ya majengo basi wanayataja na yanawajibika katika sheria.
Mkuu Hamida alipongeza ZRA kwa uamuzi wa kufanya Mafunzo hayo ambayo yatasaidia kwa pamoja kutekeleza jambo hilo kwa ufanisi mkubwa na kuahidi kusimamia wajibu huo ili kuhakikisha wananchi wanashiriki kikamilifu katika kulipa kodi hiyo.
Naye Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA), Yussuph Juma Mwenda, aliwaomba masheha hao kuhakikisha elimu waliyopatiwa wanaifikisha kwa wananchi na kuona wanashirikiana katika kusajili majengo yote na wale walioanishwa katika sheria ya majengo basi wanawajibika.
Alisema hatua hiyo itasaidia kufanya zoezi hilo kwa ufanisi na kuona kodi hiyo inakusanywa na kurudi moja kwa moja kwa wananchi katika kuboresha miundombinu mbalimbali ikiwemo barabara.
Shaaban Yahya Ramadhan ni Mkuu wa Kitengo cha Habari, Uhusiano na Huduma kwa Walipakodi alitoa elimu kwa masheha hap alisema kodi ya majengo sio kodi mpya kwani sheria yake ilipitishwa tokea mwaka 2008, lakini haikufanyiwa kazi lakini mwaka 2023 ndio inataka kuanza kufanyiwa kazi ya kukusanya kodi ya majengo.
Alisema Baraza la Wawakilishi mwaka Jana lilipitisha viwango maalum vya kutoza kodi hiyo ya majengo ili kuona sheria hiyo inatekelezwa kwa vitendo.
Akiyataja majengo hayo yaliyoidhinishwa kulipa kodi ya majengo alisema ni majengo ya mahoteli ambapo hoteli ya nyota tano 500,000, hoteli ya nyota nne 400,000 hoteli ya nyota tatu 300,000 hoteli ya nyota mbili 100,000 na hoteli nyenginezo 50,000.
Alisema majengo ya biashara ni shilingi 50,000, majengo ya ya biashara yenye ghorofa 50,000 kwa ghorofa na majengo ya ghorofa ya makaazi ni shilingi 10,000 ambapo viwango hivyo vitatozwa kwa mwaka mzima.
Alisisitiza kwamba sheria inasisitiza kwamba kodi hiyo ya majengo inatakiwa kulipwa na mmiliki mwenyewe na sio alimpangisha.
Alisema nyumba ya makaazi ya chini haizimo katika sheria hiyo hivyo aliwaomba masheha kushirikiana na mamlaka hiyo kuona sheria hiyo inatekelezwa vyema.
Mapema Kamishna wa Mapato ambayo sio ya Kodi Said Ali Mohammed, aliahidi kwamba watahakikisha wanatoa elimu kwa wananchi wote wa Zanzibar ili waweze kufahamu jambo hilo na kuona wanatekeza agizo lililowekwa katika sheria.
Hiyo, aliwaomba kushirikiana ili kuona zoezi hilo linafanikiwa katika Shehia zote 388 za Unguja na Pemba.