Timu ya taifa ya soka ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iimeichapa Wales mabao 2 kwa 0 katika fainali za mashindano ya soka ya Kombe la Dunia yanayoendelea nchini Qatar.
Vijana wa Kocha Mreno Carlos Queiroz leo waliingia uwanjani katika mechi ya kundi B wakiwa na jeraha kubwa la kutandikwa na Uingereza mabao 6 kwa mawili katika mechi yao ya awali. Waswahili wanasema nyota njema huonekana asubuhi kwani timu ya soka ya Iran al-maaruf “Team Melli” ilionekana kuwa na usonga wa kupata ushindi na ilianza kusakata kandanda safi tangu dakika ya mwanzo baada ya kipyenga cha kuanza mechi kupulizwa.
Iran ambayo katika mechi ya awali licha ya kupoteza mchezo huo ilimpoteza pia kipa wake mahiri nambari moja Alireza Beiranvand ambaye aliumia vibaya, lango lake leo lilindwa vyema na golikipa wake nambari mbili Sayyid Hussein Hussein.
Kipindi cha kwanza kilimalizika huku Iran ikitawala mchezo lakini ikishindwa kutikisa nyavu za Wales. Washambuliaji mahiri wa Iran kama Sardar Azmon anayesakata soka la kulipwa katika ligi ya Bundesliga ya Ujerumani na Ali Gholizadeh anayesakata kambumbu la kimataifa huko nchini Ubegiji walikosa nafasi kadhaa za kufunga baada ya mashuti yao kugonga mwamba.
Mambo yalianza kuindea vizuri zaidi Iran baada ya mlinda mlango wa Wales kutolewa nje kwa kadi nyekundu katika dakika ya 86 baada ya kumchezea rafu nyota hatari wa Iran Mehdi Taremi mchezaji mahiri wa Porto ya Ureno.
Magoli ya Iran katika mechi ya leo yaliyohuisha matumaini ya Iran kusonga mbele katika kundi lake kama itashinda katika mechi iliyobakia na Marekani yalipachikwa wavuni la kiungo Ruzbeh Cheshmi na beki wa kulia Ramin Rezaeian. Mabao yote ya Iran yalifungwa katika dakika za nyongeza za mchezo huku mabeki wa Iran wakifanikiwa kuwatia mfukoni nyota wa timu ya soka ya Wales akiwemo nahodha na mchezaji wao mahiri Gareth Bale. Miji mbalimbali ya Iran leo imeshuhudia furaha, nderemo na vifijo vya kushangilia ushindi wa timu ya soka ya Iran katika mashindano ya Kombe la Dunia 2022 nchini Qatar.