Mwanajeshi mmoja Mzayuni aliyejipenyeza nchini Qatar kwa sura bandia ya msanii wa vichekesho, amekimbia haraka nchini humo baada ya Mpalestina mmoja kumgundua na kufichua uhakika wake kupitia mtandao wa kijamii wa Twitter.
Tovuti ya habari ya al Khalij al Jadid imeripoti habari hiyo leo Jumapili na kuongeza kuwa, Samar Dahmash Jarrah, mwandishi Mpalestina raia wa Marekani amesambaza picha ya mwanajeshi huyo wa utawala wa Kizayuni katika ukurasa wake wa Twitter na kufichua kwamba, Guy Hochman si msanii bali ni mwanajeshi wa Israel aliyejipenyeza nchini Qatar.
Mwandishi huyo Mpalestina ambaye ana wafuasi laki moja na 71,000 katika ukurasa wake wa Twitter, pia ameandika: Hochman alikuwa kamanda wa kikosi cha 932 cha brigedi za Nahal ambacho kiliua maelfu ya Wapalestina katika Intifadha ya Kwanza na ya PIli ya Palestina.
Ujumbe huo wa Twitter wa Samar Dahmash Jarrah umepokewa kwa shauku kubwa na watu wengi.
Vyombo vya habari vya Kizayuni vilikuwa vimetangaza kuwa, Hochman amepanga kubakia Qatar hadi mwishoni mwa mashindano ya Kombe la Dunia, lakini amekimbia haraka mara baada ya kusambazwa ujumbe huo wa Twitter uliofichua uhakika wake.
Mwishoni mwa mwezi uliopita wa Novemba pia, gazeti la Kizayuni la Yedioth Ahronoth liliashiria matatizo makubwa yanayowakumba waandishi wa habari wa utawala wa Kizayuni katika mashindano ya Kombe la Dunia 2022 yanayoendelea hivi sasa nchini Qatar na kuandika, katika mashindano haya tumeelewa ni kiasi gani hatupendwi na tunachukiza vibaya katika ulimwengu wa Kiarabu.
Kwa mujibu wa shirika la habari la FARS, gazeti hilo la Kizayuni limeandika katika ripoti yake kuwa, waandishi wa habari wa utawala wa Kizayuni wa Israel waliotumwa Qatar kuakisi mashindano ya Kombe la Dunia ya Kandanda 2022 wanakabiliwa na wakati mgumu.
Waaandishi wa utawala wa Kizayuni wamesusiwa kikamilifu na wanashindwa kufanya mahojiano na watu, kwani kila wanapojitambulisha kuwa ni kutoka Israel, Waarabu wanawakwepa kama ukoma huku wengine wakisema waziwazi kuwa katika dunia hakuna kitu kinachoitwa Israel.
Tovuti ya televisheni ya Al Mayadeen nayo imelinukuuu gazeti la hilo la Kizayuni la Yedioth Ahronoth likisema: “Tumeelewa vizuri ni kiasi gani Israel haipendwi katika ulimwengu wa Kiarabu.”