WAKENYA wameungana na ulimwengu kuadhimisha Sikukuu ya Krisimasi mnamo Desemba 25, 2023, huku maelfu wakiwa kwenye kambi kutokana na athari za mvua ya El-Nino.
Wakazi katika kaunti za Tana River, Meru, Taita Taveta, Kwale, Lamu, Isiolo kati ya maeneo mengine, wanateseka kwenye baridi, kung’atwa na mbu na kukosa maji safi na chakula.
Isipokuwa tu kaunti ya Lamu, ambako kambi zilizotengenezwa ni za watu waliotoroka makwao kutokana na mashambulio ya kigaidi, kambi zilizo katika kaunti nyingine nchini ni za watu ambao makazi yao yaliharibiwa na mafuriko.
Kwa wengi wao, hii itakuwa ni mara ya kwanza kusherehekea sikukuu hiyo bila kuwepo kwenye makazi yao rasmi.
Bi Dorothy Halubva, ambaye ni mama wa watoto wanne, kwa sasa anaishi kwenye chumba cha muda katika kijiji cha Gumba, Kaunti ya Tana River.
Kwa mara ya kwanza katika maisha yake, amejua uchungu ambao mtu asiye na makazi huwa anapitia.
Pia, amekaa kwa siku kadhaa bila chakula. Awali hajawahi kukosa chochote maishani mwake.
Hata hivyo, hali ni tofauti mara hii kwani atasherehekea Sikukuu ya Krisimasi kwa namna tofauti kabisa.
“Kufikia sasa, ningekuwa nishaweka taa maalum za kurembesha kuta za nyumba yangu. Hata hivyo, mara hii nitawasha tu mshumaa. Ninatarajia kuimba nyimbo za kusherehekea sikukuu hii usiku,” akasema.
Bi Mary Hiribae pia hana furaha kuihusu siku hii, ikiwa hatukatokea mtu yeyote wa kumsaidia kutoka kambini.
“Sina hema. Ninahangaika sana kupata chakula na makazi. Siwezi kumpa shinikizo yoyote mume wangu kwani hii ndiyo hali inayotukabili sote,” akasema.
Mama huyo mwenye watoto wawili, hataimba nyimbo za kuisherehekea sikukuu kwani haoni lolote la kufurahia.
“Watoto wangu wanaonekana wenye furaha wakicheza na wenzao lakini Krismasi hii itakuwa tofauti sana kwao,” akasema.
Mashambulio
Katika Kaunti ya Lamu, hatima ya zaidi ya familia 200 haijulikani, baada ya kuachwa bila makao kutokana na mashambulio ya kigaidi.
Kwa miezi saba iliyopita, familia hizo zimekuwa zikikaa katika kambi iliyo katika shule ya msingi ya Juhudi.
Mwenyekiti wao, Bw Joseph Ngige, asema zawadi yao kubwa itakuwa kusherehekea Sikukuu ya Mwaka Mpya kwenye makazi yao.
“Hali ni mbaya hapa. Hivyo, tunaiomba serikali iharakishe utengenezaji wa kambi za polisi na jeshi katika vijiji vyetu,” akasema Bw Ngige.
Kwa Bi Beatrice Kilinguli, anayetoka katika eneo la Ukunda, Kaunti ya Kwale, maana ya Sikukuu ya Krismasi ni kujumuika pamoja na familia yake.
Mama huyo wa watoto wawili anasema kuwa huwa anawategemea wahisani kwa mahitaji yake ya kimsingi. Anasema anatarajia kuwa kuna mtu atakayejitokeza ili kumsaidia.
“Tungependa usaidizi zaidi kutoka kwa serikali, hasa wanawake ambao hawana waume na wanahangaika kuzilisha familia zao. Sh2,000 ambazo huwa tunapata kila mwezi kutoka kwa serikali huwa hazitoshi,” akasema Bi Kilinguli.
Ijapokuwa yeye ni Mwislamu, Bw Rashid Chano kutoka Kwale ni mwingi wa matumaini kuhusu msimu huu wa Krismasi.
Kwake, hali ilivyo siku hii ni ishara kwamba mwaka huu umekuwa mgumu, ijapokuwa unakaribia kufikia mwisho.
Katika Kaunti ya Mombasa, kauli ya Bw Darrel Midega, ambaye ni mwanafunzi wa chuo kikuu, inafanana na zile za Bi Keziah Katile na Bw Maxwell Kiche.
“Zawadi ambayo serikali inaweza kutupa msimu huu wa Krismasi ni kupunguza gharama ya maisha. Kama mwanafunzi aliye katika chuo kikuu, gharama kubwa ya maisha imetuathiri sana,” akasema.
Wakenya wengi walio katika kambi hizo wanasema kuwa misaada ambayo serikali imekuwa ikitangaza kutoa ili kuwasaidia bado haijawafikia.