Kuanza kazi baraza la mawaziri la sita la Netanyahu katika mazingira ya mivutano katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu

Benjamini Netanyahu amepata kura ya kuwa na imani naye kwenye Knesset, bunge la utawala haramu wa Israel, na hivyo kupata fursa nyingine ya kuongoza baraza la mawaziri la utawala huo.

Netanyahu ameweza kupata kura chanya 63 kati ya wabunge 120 wa Knesset ambapo yeye na washirika wake waliweza kushinda viti 64 katika uchaguzi wa Knesset uliofanyika mnamo Novemba 1. Hili ni baraza la mawaziri la sita la Netanyahu tangu 2009.

Baraza hilo limeanza kufanya kazi huku likiwa ni baraza lenye mawaziri walio na mitazamo kinzani na tofauti kabisa katika historia ya utawala huo unaokalia kwa mabavu aradhi za Wapalestina. Huko nyuma Netanyahu amewahi kuhudumu katika nafasi ya waziri mkuu wa Israel kwa miaka 15, lakini hili linachukuliwa kuwa baraza lake la mawaziri lenye misimamo mikali zaidi katika historia yote ya utawala wa Kizayuni. Kwa msingi huo, kikao cha Knesset kilichoandaliwa kwa ajili ya kupigia kura ya imani baraza lake la mawaziri kilishuhudia ghasia na malalamiko ya Wazayuni na wakati huo huo hotuba ya Netanyahu katika bunge hilo ilikatizwa mara kwa mara na makelele na malamiko ya mamia ya wapinzani wake waliokuwa ndani na nje ya bunge hilo.

Ni wazi kuwa katika duru hii ya uwaziri mkuu, Netanyahu atakabiliwa na hali ngumu zaidi kuliko ile aliyoishuhudia katika vipindi vilivyopita vya utawala wake. Kwa upande mmoja, anakabiliwa na kesi za ufisadi, ambayo ni moja ya sababu za maandamano dhidi yake na kwa upande wa pili ameunda muungano katika baraza jipya la mawaziri na watu ambao wana rekodi chafu za uhalifu ikiwa ni pamoja na wizi, ufisadi, ubaguzi wa rangi na vitendo vya kigaidi, jambo ambalo limeamsha hasira za wapinzani ndani na nje ya ardhi zinazokaliwa kwa mabavu.

Huku baadhi ya wachambuzi wa mambo wakiamini kwamba washirika wa Netanyahu ndio sababu ya mivutano katika baraza lake jipya la mawaziri, wengine wanamchukulia yeye mwenyewe kuwa sababu kuu ya mivutano hiyo kwa sababu ameunda muungano na watu wenye itikadi kali ili kutwaa mamlaka ya utawala ghasibu wa Israel. Katika uwanja huo, Yossi Warter, mchambuzi wa masuala ya vyama katika gazeti la Kiebrania la Haaretz, amaandika: “Baraza hili jipya la mawaziri ni la watu wenye misimamo mikali, wenye mawazo ya giza na hatari, na ili kuthibitisha jambo hili, tunaweza kutazama matokeo yaliyoletwa na wanachama wenye misimamo mikali kwenye baraza hili la mawaziri, na ambao wana nguvu nyingi, na pia walowezi ambao wameazimia kuchochea matatizo, tofauti na ubaguzi wa rangi, lakini hilo sio tatizo kuu, bali ni tatizo la pili. Hatari kubwa zaidi inatoka kwa Waziri Mkuu mwenyewe ambaye amevuka mipaka yote inayowezekana na kukiuka maadili na sheria zote.”

Aidha Netanyahu ameunda baraza lake la 6 la mawaziri katika hali ambayo utawala wa Kizayuni umeshuhudia misukosuko na migogoro mingi ya kisiasa katika kipindi cha miaka minne iliyopita, kadiri kwamba uhai wa bunge katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu haukufikisha hata mwaka mmoja, na katika kipindi cha chini ya miaka minne, chaguzi tano za bunge zimefanyika. Ingawa baraza la mawaziri la Netanyahu mara hii limeundwa kwa urahisi zaidi kuliko vipindi vya nyuma, lakini muungano wake na watu wenye itikadi kali umewafanya wapinzani wake kuwa na matumaini ya kuvunjika mapema zaidi kwa baraza hilo la mawaziri. Kwa hiyo, ni wazi kuwa baraza imara la mawaziri na lenye nguvu halitapatikana karibuni katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu na Wazayuni.

Pamoja na hali hiyo, Netanyahu kwa mara nyingine ameibua madai ya kukaririwa na yaliyo dhidi ya Iran katika kikao cha Knesset. Katika hotuba yake kwenye Knesset, Netanyahu amedai kuwa Iran inataka kutengeneza bomu la nyuklia na kwamba kipaumbele cha baraza lake la mawaziri kitakuwa kushughulikia suala hilo. Inaonekana kwamba madai hayo ya Netanyahu yanahusiana moja kwa moja na udhaifu wa baraza lake jipya la mawaziri, na kwa kuibua suala la Iran, anajaribu kupotosha fikra za waliowengi pamoja na wapinzani wake katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na kuzielekeza kwenye masuala mengine yasiyohusiana na machafuko ya kisiasa na udhaifu wa baraza lake jipya la mawaziri.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *