Kuendelea chokochoko za Marekani katika Rasi ya Korea

Harakati za kijeshi za Marekani na Korea Kusini katika Rasi ya Korea zingali zinaendelea, ambapo katika mazoezi ya pamoja ya kijeshi ya karibuni zaidi kufanywa na Marekani na Korea Kusini kwenye rasi hiyo, ndege za kivita kadhaa za Marekani zikiwemo za mashambulio ya kimkakati za B-52 na za kushambulia kwa kujificha za F-22 zilipaa katika anga ya eneo hilo.

Ndege za kivita za F-35A na F-15K nazo pia zilishiriki katika manuva hayo. Hii inamaanisha kwamba, Marekani imetumia nguvu na uwezo wake wote wa kijeshi kutoa vitisho kwa Korea Kaskazini na kwa China pia. Wakati hivi karibuni serikali ya Korea Kaskazini iliionya na kuitahadharisha Korea Kusini juu ya matokeo mabaya ya kuchochea mgogoro na kufanya chokochoko za kijeshi katika Rasi ya Korea, Marekani imeamua kufanya mazoezi ya pamoja ya kijeshi ya majini na angani na washirika wake wawili katika eneo hilo, yaani Japan na Korea Kusini, ili kuendeleza sera ya mashinikizo ya juu zaidi dhidi ya Korea Kaskazini na kuipandisha hasira nchi hiyo.

Kuhusiana na suala hilo, Li Kaisheng, mtaalamu wa masuala ya kisiasa nchini China, anasema:

“Marekani inajaribu kuupima ustahamilivu wa kimkakati wa China na Korea Kaskazini, wakati lengo lake kuu ni kuchochea mashindano ya silaha katika eneo hilo na kuuza zana za kijeshi. Marekani inaelewa fika kwamba si Korea Kaskazini wala China iliyo tishio kwa majirani zake, lakini inachochea hisia za hofu kuhusiana na Korea Kaskazini, ili kujaribu kuhalalisha uwepo wake wa kijeshi huko Korea Kusini na Japan”.
Ingawa Korea Kaskazini imeonyesha kivitendo kwamba haiathiriwi na rabsha na makeke ya Marekani na washirika wake katika eneo hilo, hata hivyo, ili kuimarisha nguvu za kuzuia hujuma, Kim Yo Jong, dada wa kiongozi wa Korea Kaskazini, alisisitiza katika hotuba, alipozungumzia uendelezwaji wa mipango ya makombora ya Pyongyang licha ya vikwazo vya kimataifa ilivyowekewa, ya kwamba, majaribio ya makombora ya Korea Kaskazini yana uhusiano wa moja kwa moja na usalama wa nchi hiyo. Kuhusiana na hilo, tangu mwanzoni mwa mwaka huu hadi sasa, Korea Kaskazini imesharusha makumi ya makombora. Wakati huo huo, Wakorea Kusini daima wamekuwa wakipinga sera za serikali yao za kuchochea mvutano katika uhusiano wa nchi hiyo na Korea Kaskazini, na wanataka nchi yao ifuate sera huru, na si kuwa na utegemezi kwa Marekani; sera ambayo inazingatia maslahi ya kitaifa ya Korea Kusini tu.

Abolfazl Zahravand, mtaalamu wa masuala ya kimataifa, analizungumzia hilo kwa kusema:

“Wakorea Kusini wanajua wazi kwamba ikiwa utatokea mgogoro wowote kwenye Rasi ya Korea, ni watu wa eneo hilo ndio watakaodhurika zaidi, si Marekani iliyoko umbali wa maelfu ya kilomita kutoka eneo hilo; na ndio maana wanapinga vikali sera za serikali yao za kushupalia harakati za kijeshi kwa ushirikiano na Marekani.”
Alaa kulli hal, Marekani inaendesha kampeni ya uenezaji hofu kuhusiana na Korea Kaskazini, ili kufanikisha sera yake ya kuizingira China na kuzusha mgogoro katika eneo la Rasi ya Korea. Na hii ni katika hali ambayo, kwa kufuata sera ya ustahamilivu wa kimkakati, China na Korea Kaskazini zimeonyesha kivitendo kuwa, haziathiriwi na sera za uchochezi za Marekani. Lakini pamoja na hayo, siasa za kushupalia na kuwasha moto wa vita za Washington zitaifanya Korea Kaskazini izidi kuchukua hatua za kuimarisha zaidi nguvu na uwezo wake wa kuzuia hujuma za kijeshi.
Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *