Kuendelea kukandamizwa wanawake nchini Saudi Arabia

Wanaharakati 35 wa kike wa Saudi Arabia wamehukumiwa kifungo cha miaka 11 jela ikiwa ni muendelezo wa ukandamizaji unaofanywa na ukoo wa Aal Saud dhidi ya wanawake.

Saudi Arabia ni miongoni mwa nchi zenye historia mbaya sana ya uvunjaji wa haki za wanawake duniani. Takwimu zinaonesha kuwa, utulivu na usalama kwa wanawake wa Saudia ulikuwa wa chini sana mwaka 2019. Licha ya kuongezeka idadi ya wanawake waliosoma na pamoja na kushirikishwa hivi sasa katika masuala ya afya, lakini wanawake wa Saudi Arabia hawapewi uhuru wa kutosha wa kufanya kazi.

Mohammad bin Salman, mrithi wa ufalme wa Saudia ambaye kimsingi ndiye anayeongoza nchi hiyo hivi sasa, amechukua baadhi ya hatua kwa manufaa ya wanawake katika miaka ya hivi karibuni, lakini sehemu kubwa ya hatua hizo zinaonekana ni za kumfanya mwanamke kutumiwa vibaya na wanaume. Hadi hivi karibuni, mwanamke wa Saudi Arabia alikuwa amenyimwa hata haki ya kuendesha gari. Mabadiliko mapya ya Bin Salman ni ya kumruhusu mwanamke wa Saudia kushiriki katika kumbi za starehe za miziki ya mchanganyiko wa wanaume na wanawake wasio maharimu, na kumruhusu mwanamke kutembea bila ya kuwa na mtu wa familia yake, mambo ambayo kwa miaka mingi lilikuwa ni jambo la kawaida kabisa kwa nchi nyinginezo.

Mohammad bin Salman alijigamba na kupiga makelele mengi kwa kufanya marekebisho hayo. Lakini ukweli ni kwamba hayo yalikuwa ni marekebisho ya kijuujuu tu. Marekebisho hayo si lolote si chochote kwani ukandamizaji na udhalilishaji wa wanawake umekita mizizi huko Saudi Arabia. Katika miaka ya hivi karibuni, utawala wa kiimla wa Saudia hata umeweka sheria kali zaidi za kuwakandamiza wanaharakati wa kike huku hatua ya karibuni kabisa ikiwa ni kuwafunga jela wanaharakati 35 wa kike kwa kutangaza mitazamo yao ambayo haikuwafurahisha wakuu wa ukoo wa Aal Saud.

Lina al Hathloul, mkuu wa kitengo cha mahusiano ya umma na usimamizi cha shirika la haki za binadamu la ALQST lenye makao makuu yake mjini London Uingereza amesisitiza kuwa, ukandamizaji wa wanawake bado ni mkubwa nchini Saudi Arabia. Ameandika: Ustawi wa wanawake katika miaka ya hivi karibuni hata haujakabiria kiwango wanachotaka wanawake wa Saudia. Tunataka tuishi nchini Saudi Arabia bila ya woga wowote na tuweze kupigania haki zetu kwa uhuru na kuzipata. Matamshi hayo yanaonesha ni kiasi gani wanawake nchini Saudi Arabia wanaendelea kuishi katika mazingira ya woga na wasiwasi huku muundo wenyewe wa Saudia ukiendelea kuwa kandamizi kwa wanawake.

Ijapokuwa Mohammad bin Salman anadai kufanya marekebisho kwa manufaa ya wanawake wa Saudi Arabia, lakini ukandamizaji wake wa kisiasa unazidi kufichua uongo na hila za mrithi huyo wa ufalme wa Saudia. Kwa hakika ukandamizaji huo unazidi kuonesha kwamba, lengo la Bin Salman ni kujikurubisha zaidi tu kwa jamii za Magharibi. Kukandamizwa wanaharakati wakubwa wa haki za wanawake huko Saudi Arabia kuliongezeka mwaka 2018. Hii inaonesha kuwa, hata kama kuna baadhi ya marekebisho yamefanyika, lakini watetezi wa haki za wanawake wanaendelea kukandamizwa vibaya. Takwimu kamili za wanawake waliotiwa mbaroni nchini Saudi Arabia kwa kuelezea hisia zao hazijulikana lakini baadhi ya duru zinasema kuwa, wanawake hao hawapungui 100.

Licha ya majigambo mengi ya Bin Salman, lakini wanawake wa Saudi Arabia hadi hivi sasa hawapewi haki zao za kisiasa. Shirika jingine moja la haki za binadamu la Saudia lenye makao yake barani Ulaya limesema kuwa, madai kuwa hali ya haki za wanawake nchini Saudi Arabia imekuwa nzuri ni uongo. Limesisitiza kuwa, madai hayo yanakinzana kikamilifu na uhalisia wa mambo.

Amma jambo la kulitilia maanani zaidi hapa ni kwamba, licha ya kuwa Saudi Arabia ina historia mbaya ya uvunjaji wa haki za binadamu hasa za wanawake, lakini inajipa uthubutu wa kuzungumzia haki za wanawake katika nchi nyingine huru kama Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Tena hii ni katika hali ambayo haki za wanawake ndani ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni za kiwango cha juu mno katika nyuga zote za kijamii, kisheria, kiuchumi, kisiasa n.k, na Saudia haiwezi hata kukaribia haki za wanawake ndani ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *