Kuendelea mwenendo wa kufutwa kazi wafanyakazi huko Marekani; Amazon kupunguza wafanyakazi elfu 18

Mkurugenzi Mtendaji wa Amazon amesema kuwa kampuni hiyo itawafuta kazi wafanyakazi zaidi ya 18,000.

Baadhi ya waajiri wakubwa wa Marekani, ikiwa ni pamoja na Walmart, Facebook na Pepsi, hivi karibuni wamepunguza maelfu ya nafasi za kazi nchini humo.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, Andy Jaycee amesema leo Alhamisi kwamba idara muhimu zitakazopunguziwa wafanyakazi ni za nguvu-kazi na mauzo ya mtandaoni za shirika hilo, na kwamba mchakato wa kuwafuta kazi wafanyakazi hao utaanza kutekelezwa wiki mbili zijazo.

Katika dokezo kuhusu kufutwa kazi wafanyikazi 18,000 wa Amazon, mkurugenzi mtendaji huyo amesema: “Tumekuwa tukiwaajiri watu kwa kasi kubwa katika miaka ya hivi karibuni. Pamoja na hayo kutokana na hali mbaya ya kiuchumi, imekuwa vigumu sana kuchukua uamuzi wa kuwafuta kazi.”

Amazon ina takriban wafanyakazi rasmi 300,000, na kufutwa kazi watu 18,000 kutamaanisha kufutwa kazi asilimia 6 ya wafanyakazi hao.

Shirika hilo lina jumla ya wafanyakazi zaidi ya milioni 1.5, ikiwa ni pamoja na wale wanaofanya kazi katika maghala, shirika ambalo ni la pili kwa ukubwa katika sekta kibinafsi nchini Amerika baada ya shirika la Walmart.

Kupungua ukuaji wa uchumi na kuongezeka mfumuko wa bei huko Marekani pamoja na kushuka kwa thamani ya hisa za kampuni hiyo ni miongoni mwa mambo ambayo yameilazimisha kuamua kuachisha kazi idadi kubwa ya wafanyakazi wake.

Awali Amazon ilikuwa imepanga kuwaachisha kazi wafanyakazi 10,000 pekee mwezi Novemba, lakini sasa idadi hiyo imepanda na kufikia 18,000.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *