Baada ya miaka 15, sasa ndege za utawala haramu wa Israel zinaweza kufanya safari nchini Uturuki.
Yair Lapid, Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Israel ametangaza habari ya kupasishwa hati ya makubaliano ya mahusiano ya safari za ndege baina ya Uturuki na utawala huo. Amesema hayo katika kikao cha hivi karibuni cha Baraza la Mawaziri la utawala vamizi wa Israel. Kwa mujibu wa makubaliano hayo, kuanzia sasa na kuendelea, ndege za mashirika ya ndege ya utawala ghasibu wa Israel unaoikali kwa mabavu Beitul-Muqaddas, zitaweza kufanya safari nchini Uturuki na kutua katika Uwanja wa Ndege wa Istanbul pamoja na miji mingine ya nchi hiyo. Sambamba na kuondolewa vikwazo vilivyokuweko kwa ndege za Israel kuelekea Uturuki, vyombo vya habari vya Kiebrania katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni maghasibu, vimeripoti habari ya kutia nanga manowari ya Uturuki katika pwani ya utawala huo kwenye maji ya Mediterania.
Magazeti ya utawala ghasibu wa Israel yameripoti habari hiyo kwa kuandika: Manowari ya Uturuki pamoja na meli ya kivita ya kombora ya Marekani zimetia nanga katika bandari ya Haifa kaskazini-magharibi mwa ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu.
Uturuki na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel hivi karibuni zilitangaza kuwa, zimerejesha tena kikamilifu na katika hali ya kawaida uhusiano wao wa kidiplomasia. Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni Yair Lapid na Waziri wa Masahuri ya Kigeni wa Uturuki Mevlut Cavusoglu walitangaza rasmi mwishoni mwa mwezi uliopita wa Agosti kwamba uhusiano kati ya pande hizo mbili umerejea katika hali ya kawaida na kwamba hivi karibuni Tel Aviv na Ankara zitateua mabalozi wao.
Uhusiano wa Uturuki na utawala wa Kizayuni wa Israel ulikuwa umedorora na kutawaliwa na mivutano kwa muda wa miaka 12 kufuatia tukio la meli ya Uturuki ya “Mavi Marmara”. Mwaka 2010, jeshi la utawala haramu wa Israel lilishambulia meli hiyo ya Msafara wa Uhuru” iliyokuwa imebeba shehena za misaada ya kibinadamu kwa ajili ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza. Raia 10 wa Uturuki miongoni mwa wanaharakati waliokuwemo ndani yake waliuawa katika hujuma hiyo ya jeshi la Kizayuni.
Harakati za hivi karibuni za Uturuki za kufufua uihusiano wake na utawala ghasibu wa Israel zinafanyika katika hali ambayo, kabla ya hapo maafisa wa utawala wa Tel Aviv waliitaka serikali ya Recep Tayyip Erdogan ifunge ofisi ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS katika mji wa Ankara.
Irit Lilian mwanadiplomasia wa Israel alisema katika mkutano wake na waandishi wa habari mjini Istanbul kwamba: Israel inaona kuwa, kuendelea kuweko harakati za ofisi ya HAMAS mjini Istanbul ni changamoto muhimu inaoukabili uhusiano wa pande mbili yaani Tel Aviv na Ankara.
Mwanadiplomasia huyu amesema bayana kwamba:
Hapana shaka kuwa, Israel inataraji kuiona Uturuki mbali na kufunga ofisi ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS mjini Istanbul, inawatimua pia nchini humo viongozi wa kundi hilo.
Harakati mpya za serikali ya Uturuki zina maana ya kusalimu amri serikali ya Rais Erdogan mbele ya matakwa ya utawala haramu wa Israel. Inapasa kusema kuhusiana na harakati za hivi karibuni za serikali ya Ankara kwamba: Kivitendo Rais wa Uturuki ametoa pigo kubwa kwa malengo matukufu ya wananchi madhulumu wa Palestina. Hii ni katika hali ambayo, Erdogan katika kipindi cha miaka yote ya huko nyuma akitumia nara ya kuwaunga mkono wananchi wa Palestina alifanya juhudi za kujipatia uungaji mkono wa wananchi wa Uturuki na mataifa ya eneo kwa ajili ya maslahi yake binafsi na ya chama chake.
Kwa kuzingatia mgogoro wa kiuchumi na matatizo ya kimaisha yanayoongezeka ya wananchi wa Uturuki inapasa kusema kuwa: Viongozi wa serikali ya Uturuki hawajaweza kuchukua hatua za maana za kuyapatia ufumbuzi matatizo ya kiuchumi ya wananchi pamoja na matatizo ya kifedha yanayoikabili serikali. Hatua ya Uturuki ya kurejesha uhusiano wa kawaida na baadhi ya mataifa ya eneo ukiwemo utawala ghasibu wa Israel ni juhudi ambazo kupitia njia hiyo zinalenga kupunguza matatizo ya kiuchumi ya wananchi wa nchi hiyo.
Kwa zaidi ya mmoja mmoja sasa ambapo kumeshuhudiwa ndoto za serikali ya Rais Erdogan za kuanzisha tena uhusiano na baadhi ya mataifa ya eneo ambapo hadi sasa hilo halijawa na taathira yoyote chanya kwa uchumi wa nchi hiyo.
Kiujumla tunapasa kusema kuwa, kufufuliwa uhusiano baina ya Uturuki na utawala haramu wa Israel siyo tu kwamba, hatua hiyo haiwezi kupunguza matatizo ya kiuchumi ya Uturuki, bali harakati hizi zitakiongezea matatizo maradufu chama tawala na Erdogan mwenyewe na kuwafanya wapoteze nafasi yao baina ya wananchi wa nchi hiyo.