Marekani ingali inaendelea kuingilia masuala ya ndani ya Iraq kwa namna hasi, kwa kuzingatia nyenzo za mashinikizo ilizonazo mikononi mwake.
Tangu mwaka 2003 hadi leo, Marekani imejaribu kutumia visingizio mbalimbali kuendeleza ushawishi na uwepo wake nchini Iraq. Ushawishi huo, ambao umebadilika na kuwa uingiliaji, haujailetea Iraq amani na usalama, kwa sababu kundi la kigaidi la DAESH (ISIS) liliishambulia kijeshi Iraq na kushikilia theluthi moja ya ardhi ya nchi hiyo wakati wanajeshi wa Marekani wakiwa nchini humo. Hata hivyo, uingiliaji huo umekuwa na changamoto kubwa kwa Iraq, mfano mpya ukiwa ni wa kushuka thamani ya sarafu ya dinari ya nchi hiyo dhidi ya ile ya Marekani ya dola. Katika siku za hivi karibuni, gazeti la al-Madaa la Iraq, likinukuu vyanzo vya habari vya nchi hiyo liliandika, “wizara ya fedha ya Marekani imeripoti kwa kunukuu nyaraka za Benki Kuu ya Iraq, kwamba benki na taasisi za fedha zaidi ya 60 za nchi hiyo zinafanya kazi nje ya viwango halisi vya mfumo wa kibenki; na kwa kweli kwa kughushi nyaraka za kibiashara na hasa bidhaa zinazoagizwa kutoka nje, zinawasaidia wafanya magendo ya sarafu ya dola kuhamisha fedha hizo kwa kutumia kichaka cha uingizaji bidhaa.”
Safwan Qausi, mwanauchumi wa Iraq anaitakidi kuwa, kupanda kwa bei ya dola ya Marekani katika soko la Iraq kunatokana na vizuizi vipya ambavyo wizara ya fedha ya Marekani imeviweka kuhusiana na kinachoitwa “mabadilishano ya kifedha na baadhi ya nchi”. Bila kutaja moja kwa moja nchi hizo, Qausi anaeleza kwamba, baadhi ya nchi hizo ni “washirika wa kibiashara wa Iraq”. Kwa mujibu wa mwanauchumi huyo, baadhi ya wafanyabiashara wameanza kuingiza bidhaa kutoka nje ya nchi bila kuzingatia vizuizi hivyo, na kutokana na matatizo yanayojitokeza katika uhamishaji fedha kupitia njia rasmi, wanalazimika kutafuta fedha wanazohitaji kupitia njia zisizo rasmi; hatua ambayo imesababisha kupanda kwa bei ya dola katika soko lisilo rasmi.