Wizi na usafirishaji kimagendo mafuta ya Syria ungali unaendelea kufanywa na wanajeshi wa Marekani na wanamgambo wenye mfungamano nao katika ardhi ya nchi hiyo.
Tangu mwaka 2011, wakati Syria ilipolazimishwa kuingia kwenye vita vya kupambana na magaidi, mbali na Marekani kuyaunga mkono baadhi ya makundi ya magaidi hao imekuwa ikilipa kipaumbele pia suala la uporaji wa maliasili za nishati za nchi hiyo; na katika miaka ya karibuni imepora na kuhamisha kimagendo sehemu kuu ya akiba ya mafuta ya Syria. Kwa msaada wa wanamgambo wa Vikosi vya Kidemokrasia vya Wakuridi wa Syria SDF jeshi la Marekani linalishikilia eneo kuu la visima vya mafuta na gesi vya Al Hasakah na Deir ez-Zur ndani ya ardhi ya Syria.
Katika kutekeleza mkakati wake huo wa kiharamia, jeshi la Marekani limeanzisha kwa msaada wa wanamgambo hao wa Kikurdi wa kundi la SDF barabara maalumu zisizo rasmi kwa ajili ya kusafirishia kimagendo mafuta ya Syria. Wiki iliyopita, Marekani ilisafirisha kimagendo kupeleka nchini Iraq malori 300 ya mafuta kupitia kivuko cha al Mahmudiyah.
Mnamo tarehe 8 Agosti, wizara ya mafuta ya Syria ilieleza katika taarifa kwamba, kwa wastani, Marekani na vibaraka wake wanapora kila siku mapipa 66,000 ya mafuta, ambayo ni sawa na asilimia 80 ya mafuta ya nchi hiyo yanayozalishwa kwa siku. Wizi wa mafuta ya Syria hadi sasa umeisababishia sekta ya mafuat ya nchi hiyo hasara za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja za dola bilioni 105.
Askari wa jeshi la Marekani wanaendeleza wizi na usafirishaji kimagendo wa mafuta ya Syria katika hali ambayo serikali ya Damascus imeshatangaza mara kadhaa kuwa Washington inapora maliasili na rasilimali hizo zikiwemo za mafuta na gesi pamoja na ngano na kutaka wanajeshi hao wavamizi waondoke katika ardhi ya nchi hiyo. Mbali na hayo, wananchi wa Syria hadi sasa wameshaandamana mara kadhaa na kupaza sauti zao kutaka askari wa Marekani waondoke nchini humo na wizi wa maliasili za nchi hiyo ukomeshwe.
Sambamba na hayo, kwa nyakati tofauti, serikali ya Syria imeliandikia barua Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kulalamikia wizi wa mafuta unaofanywa na Marekani. Lakini licha ya malalamiko na mashtaka hayo yaliyowasilishwa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Syria kwa Baraza la Usalama, si Marekani iliyositisha uporaji wa mafuta ya nchi hiyo, wala si Baraza la Usalama lililochukua hatua yoyote ya kuilazimisha Washington ikomeshe uharamia wake wa kuiba maliasili ya mafuta ya Syria.
Japokuwa Marekani imedai mara kadhaa kwamba imejiingiza kijeshi katika ardhi ya Syria kwa lengo la kupambana na magaidi, lakini aliyekuwa rais wa nchi hiyo Donadld Trump alishawahi kutamka kinagaubaga kuwa, wanajeshi wa Marekani wamepiga kambi huko Syria kwa sababu ya visima vya mafuta vya nchi hiyo. Ukweli ni kuwa, ugaidi umefanywa kisingizio tu kwa ajili ya kupora maliasilii ya mafuta na rasilimali za chakula za Syria. Kwa sababu mbali na mafuta, kila wiki wanajeshi wa Marekani wanavusha kimagendo kiwango kikubwa cha ngano na nafaka zingine za Syria na kuzipeleka Iraq kwa ajili ya askari wenzao walioko nchini humo. Na hii ni katika hali ambayo idadi kubwa ya raia wa Syria ambao wametaabika na kuteseka mno katika miaka ya karibuni kutokana na ukatili wa magenge ya kigaidi, wanahitajia sana misaada ya kibinadamu ikiwemo ya chakula.
Gazeti la Kichina la China Daily liliandika hivi karibuni kuwa, Marekani imezidi kuwa na jeuri ya kuendeleza jinai za wizi na uporaji katika nchi nyingi duniani na kwamba wizi wa mafuta ya Syria ni doa jeusi na la kuaibisha kwa nchi hiyo. Gazeti hilo limeashiria wizi wa mafuta ya Syria unaoendelea kufanywa na wanajeshi wa Marekani na kuhamishiwa kimagendo nchini Iraq na kuandika: “ni rahisi kufahamu ukweli huu, kwa sababu uporaji na kukataa haki za wengine ni utaalamu wa Marekani wa muda mrefu sana”