‘Kufanyika kikao cha Kizayuni Azerbaijan ni utangulizi wa mapatano baina ya Baku na Tel Aviv’

Makundi ya Muqawama ya Palestina yametangaza kuwa, kufanyika mkutano wa Wazayuni nchini Azerbaijan ni utangulizi wa kufikiwa mapatano baina ya Baku na Tel Aviv.

Ubalozi wa Israel mjini Baku ulitangaza Jumatatu kuwa, kikao rasmi cha mabalozi wa utawala wa Kizayuni katika nchi za eneo la Eurasia kitafanyika mjini Baku mnamo siku chache zijazo kwa kuhudhuriwa na maafisa wa ngazi za juu.
Kwa mujibu wa kanali ya Telegram ya Al-I’lamul-Muqawim, makundi ya mapambano ya Palestina yametangaza katika taarifa yao iliyotolewa usiku wa kuamkia leo kwamba, makundi ya muqawama na taasisi zote za kitaifa za Palestina zinaeleza kuchukizwa kwao, zinalaani na kukasirishwa na hatua ya serikali ya Azerbaijan kuuruhusu utawala wa Kizayuni kuitisha mkutano wa aina hiyo, kwa sababu utawala huo dhalimu ungali unaendelea kufanya jinai dhidi ya taifa la Palestina na umma wa Kiislamu.

Imeelezwa katika taarifa hiyo kwamba, hatua hiyo ni utangulizi wa kuanzishwa uhusiano wa kawaida kati ya Baku na Tel Aviv, na inashangaza kwamba Azerbaijan, ikiwa nchi ya Kiislamu, imechukua hatua hiyo hatari na ya kuzusha mvutano; kwa sababu hatua hiyo ina madhara mengi kwa watu wa Azerbaijan.

Makundi ya muqawama ya Palestina yameeleza kuwa wananchi wa Azerbaijan wanapinga kuanzishwa uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni na yakabainisha kwamba, kinachofanywa na utawala huo haramu katika eneo sio tu uchokozi, uvamizi na hujuma za waziwazi dhidi ya taifa la Palestina, bali pia hujuma na uvamizi dhidi ya nchi hizo na wananchi wa mataifa ya eneo. Kwa hiyo, Wazayuni watasababisha matatizo kwa serikali ya Azerbaijan.
Muqawama wa Palestina umetoa mwito kwa wananchi wa Azerbaijan kukabiliana na hatua hizo zinazochukuliwa na serikali ya nchi hiyo za kufanya mapatano na utawala haramu wa Israel kwa sababu Marekani na utawala huo wa Kizayuni zinajaribu kutumia ardhi ya Azerbaijan kupanga njama na kufanya uchokozi na ujasusi dhidi ya nchi jirani jambo ambalo lina madhara kwa wananchi wa Azerbaijan.
Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *