Kufichuliwa jinai za Uingereza nchini Afghanistan

Mwanamfalme Harry wa ukoo wa kisultani na kifalme wa Uingereza amekiri kuua watu 25 nchini Afghanistan wakati wa vita vya miaka mingi vya nchi hiyo.

Harry ambaye ni maarufu kwa jina la Duke of Sussex, ni mtoto mdogo wa Charles III, mfalme wa hivi sasa wa Uingereza. Hivi karibuni Harry alitanga kujitoa kwenye ukoo wa kifalme wa Uingereza. Gazeti la Telegraph la nchi hiyoi limetangaza kuwa, “Harry” mwenye umri wa miaka 38 ameandika katika kitabu chake cha Spare ambacho kinatarajiwa kusambazwa wiki ijayo kwamba, alishiriki katika vita vya kivamizi huko Afghanistan kwenye miaka ya 2007 hadi 2008. Alishiriki vita hivyo akiwa kwenye jeshi la nchi kavu la Uingereza. Baada ya hapo na katika miaka ya 2012 na 2013 alishiriki tena katika vita vya Afghanistan akiwa rubani wa helikopta za kijeshi za Apache.

Ijapokuwa habari za jinai za wanajeshi wa Marekani na Uingereza huko Afghanistan zinachujwa mno, na madola ya kibeberu hayaruhusu hata kidogo kuvuja habari za jinai hizo, lakini baadhi ya wakati hufichuliwa habari za kutisha za jinai hizo. Ripoti za duru huru zinaonesha kuwa, wanajeshi wa Uingereza walikuwa wanashindana katika kuua wananchi wa Afghanistan na kuhesabu miili isiyo na roho ya Waafghani hao. Walijifakharisha kwa kuua idadi kubwa zaidi ya wananchi wa Afghanistan.

Hosseini Mazari, mtaalamu wa masuala ya kisiasa wa Afghanistan anasema: Roho za wananchi wa Afghanistan hazina thamani yoyote kwa Marekani na Uingereza kiasi kwamba katika kipindi cha miaka 20 ya uvamizi wa kijeshi nchini Afghanistan, wanajeshi wa Marekani na Uingereza walifanya ni burdani kwao kuua raia wa Afghanistan. Ukweli ni kuwa wananchi wa Afghanistan walifanywa ni shabaha za kufanyia mazoezi wanajeshi wa Uingereza na hadi hivi sasa jinai kubwa waliyofanya wavamizi hao dhidi ya wananchi wa Afghanistan haijaweza kufichuliwa kikamilifu.

Kukiri mwanamfalme wa Uingereza, “Harry” kuwa aliua watu 25 huko Afghanistan tena wakati huu ambapo wananchi wa nchi hiyo wanaendelea kuteseka kwa matatizo makubwa ya kimaisha waliyosababishiwa na madola vamizi ya Magharibi hasa Marekani na Uingereza, ni sehemu ndogo tu ya jinai za Uingereza katika maeneo yote inayoyavamia duniani na kupeleka wanajeshi wake huko. Jinai za kutisha zilizofanywa na wakoloni wa Uingereza nchini India ni kubwa sana na ni mara chache zimeshuhudiwa katika kurasa za historia. Mwanafamle wa Uingereza, “Harry” ambaye alishiriki mara mbili katika vita vya Afghanistan, kwa hakika ni mtu wa ngazi za juu zaidi wa Uingereza kushiriki kwenye jinai za kutisha huko Afghanistan. Kama yeye amekiri kushiriki kwenye jinai hizo, itakuwaje wa wanajeshi wa daraja za chini wa Uingereza? Bila ya shaka jinai zao ni kubwa zaidi. Lakini jinai hizo zimelalamikiwa kwa njia tofauti ndani na nje ya Afghanistan. Miongoni mwa malalamiko hayo ni yale yaliyoandikwa na raia wa Afghanistan kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter. Mmoja wao ameandika: Ukweli ni kuwa wananchi wetu wasio na hatia walikuwa ni sawa na kete za mchezo wa chesi, lakini ni nyinyi madola vamizi ndio mliofeli na kushindwa kwenye mchezo huo. Mwengine ameandika: Jinai hizo haziishii kufanywa tu na mwanamfalme wa Uingereza “Harry” bali wavamizi wote wamefanya jinai kubwa katika kipindi chote cha historia na Waafghani hawawezi kamwe kusahau jinai hizo.

Naye Suroush Amiri, mtaalamu mwingine wa masuala ya kisiasa anasema: Tunaposoma historia ya nchi ambazo zimevamiwa na kukaliwa kwa mabavu na Uingereza  tunaona kuna jinai nyingi sana zimefanywa na wanajeshi wa mkoloni huyo kizee wa Ulaya. Tofauti pekee iliyopo ni kwamba hadi hivi sasa hakuna taasisi yoyote ya kimataifa iliyofuatilia jinai hizo kisheria, na wanajeshi wa Uingereza wanaendelea kufanya jinai kwa jeuri kubwa katika kona mbalimbali duniani ikiwemo Afghanistan.

Alaakullihaal, kwa mtazamo wa duru za kijeshi na kifalme za Uingereza, kuua watu na kufanya jinai ni jambo rahisi na jepesi sana kwao kiasi kwamba hivi sasa hata mtu wa ukoo wa usultani wa Uingereza pia amejitokeza hadharani na kujifakhari kufanya mauaji huko Afghanistan na bila ya shaka hakuna hatua yoyote ya kisheria itakayochukuliwa dhidi yake.

 

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *