Gazeti la The Guardian limechapisha nyaraka mpya za jinai za utawala haramu wa Israel dhidi ya Wapalestina, jinai ambazo zimefanyika kwa himaya na uungaji mkono wa Marekani.
Ripoti ya gazeti la The Guardian imeashiria baadhi ya jinai za utawala ghasibu wa Israel dhidi ya Wapalestina ambazo zinajumuisha kuamiliana vibaya na watoto, kuwatesa mateka, kubomoa nyumba za Wapalestina na kuziwekea mbinyo familia za Kipalestina katika vituo vya upekuzi. Ripoti hii ina nukta mbili muhimu.
Nukta ya kwanza ni kuwa, ripoti hii ina mashiko na ni ya kuaminika hasa kwa kutilia maanani kwamba, imetegemea simulizi na ushahidi wa maafisa wa zamani wa jeshi la Israel.
Ama nukta ya pili ni kuwa, katika ripoti hiyo ya The Guardian imesisitizwa kwamba, Marekani nayo ni mshirika wa jinai hizo za Israel hasa kutokana na hatua yake ya kuunga mkono vitendo vya kinyama na utumiaji mabavu vinavyofanywa na jeshi vamizi la Israel huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu sambamba na kuusaidia kifedha utawala huo katili.
Pamoja na hayo, katika ripoti hiyo hakujaashiriwa kabisa himaya na uungaji mkono wa kisiasa wa Marekani kwa Israel hususan katika kukiuka maazimio ya Umoja wa Mataifa hususan azimio nambari 2334 la Baraza la Usalama na vilevile hatua ya Washington ya kupiga kura ya hapana katika asasi zote na kuukingia kifua utawala huo mbele ya kuchukuliwa hatua dhidi yake.
Hapana shaka kuwa, lau kama si himaya na uungaji mkono wa pande zote wa Marekani na madola ya Ulaya kwa utawala vamizi wa Israel unaofanya mauaji kila uchao huko Palestina, basi utawala huo usingeweza kutenda jinai hizi kwa kiwango hiki tena bila wasiwasi wowote.
Licha ya kuwa hatua ya gazeti la The Guardian ya kuvunja kimya mbele ya jinai za utawala haramu wa Israel inapaswa kupongezwa, lakini mambo yaliyoashiriwa na jarida hili kama ni jinai za Israel dhidi dhidi ya Wapalestina ni madogo mno ikilinganishwa na kiwango cha jinai ambazo zinazotekelezwa na utawala huo bandia.
Kabla ya hapo asasi kadhaa za haki za binadamu zisizo za kiserikali zilitoa takwimu katika ripoti zao mbalimbali kuhusiana na baadhi ya jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel huko Palestina. Shirika la Msamaha Duniani la Amnesty International Februari mwaka huu lilitoa ripoti inayoeleza vitendo visivyo vya kibinadamu vinavyofanywa na Israel kama kamatakamata ya kiholela na iliyo kinyume cha sheria, kupora ardhi na majengo ya Wapalestina, mauaji haramu, kuwahamisha kwa lazima Wapalestina, sheria kali za kwenda na kurudi na kuzuia Wapalestina kusoma ni mifano ya wazi ya ukiukajai wa dhahir shahir wa haki za binadamu.
Kutolewa ripoti hiyo kunabainisha tofauti iliyopo ya utendaji baina ya vyombo vya habari na asasi za kimataifa zisizo za kiserikali na zile ambazo ni za serikali. Vyombo vya habari na asasi ambazo zina uhuru wa namna fulani vinakiri kuhusiana na jinai za utawala haramu wa Israel dhidi ya Wapalestina na hata zimekuwa zikitoa miito ya kufuatiliwa kisheria jinai hizo za Tel Aviv. Amnesty International imekuwa ikisisitizia udharura wa kufuatiliwa kisheria jinai za utawala haramu wa Israel na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC), asasi za kieneo, kimataifa na kuhukumiwa.
Licha ya kuweko miito na matakwa hayo, lakini himaya na uungaji mkono wa madola ya Magharibi hususan Marekani kwa Israel na kuweko lobi zenye nguvu za Kiyahudi katika mfumo wa dunia na ndani ya madola ya Magharibi na kadhalika kutokuwa na uhuru wa kuchukua maamuzi asasi za kimataifa ni miongoni mwa sababu ambazo zinaupa kiburi utawala huo haramu wa kuendeleza jinai zake na wakati huo huo, kusalimika na suala la kufuatiliwa kisheria.
Jinai hizo dhidi ya Wapalestina zinatekelezwa katika hali ambayo, eneo la Ukanda wa Gaza tangu mwaka 2006 limekuwa chini ya mzingiro wa kila upande wa utawala vamizi wa Quds. Mashaka, tabu na masaibu ambayo wananchi wa Gaza wamekumbana nayo katika kipindi cha miaka 16 iliyopita ni makubwa zaidi ya jinai ambazo zimeashiria na gazeti la The Guardian katika ripoti yake na zile zilizobainishwa na Shirika la Msamaha Duniani la Amnesty International.
Jumuiya na asasi za kisheria hadi sasa hazijachukua hatua yoyote ya maana ya kukabiliana na jinai za utawala ghasibu wa Israel katika Ukanda wa Gaza. Hii ni katika hali ambayo, Umoja wa Mataifa umetangaza mara chungu nzima kwamba, Gaza imegeuka na kuwa gereza kubwa zaidi la wazi ulimwenguni.