Kwa mujibu wa ripoti zilizochapishwa, Taliban imeondoa likizo au siku ya maombolezo ya Ashura katika kalenda rasmi ya Afghanistan na badala yake kuweka mahala pake matukio kadhaa yanayohusiana nayo.
Hii ni katika hali ambayo kabla ya hapo siku hii ya Ashura ilikuwa imesajiliwa katika kalenda rasmi ya Afghanistan kama siku ya mapumziko ya umma kwa ajili ya kusisitiza umuhimu wa tukio hilo la kidini ambalo linaheshimiwa na kuenziwa na watu wengi wa nchi hiyo.
Kitendo hicho cha kuchukiza cha kundi la Taliban tena ambacho kimefanyika katika mwezi mtukufu wa Muharram, wakati ambao watu wa Afghanistan wameanza maombolezo ya kukumbuka kuuawa shahidi mjukuu wa Mtume Mtukufu (saw), Bwana wa Mashahidi Imam Hussein (as), kimeshtua na kuwashangaza wengi katika jamii ya Afghanistan. Hii ni kwa sababu yapata mwaka mmoja uliopita, Taliban walipotwaa tena madaraka ya Afghanistan, daima walikuwa wakisisitiza kuzingatiwa nara na shaari za kidini nchini humo.
Seyyed Hossein Hosseini, mtaalamu wa masuala ya Afghanistan anasema kuhusiana na kadhi hiyo kwamba:
“Kwa kufutilia mbali siku ya maombolezo ya Ashura kwenye kalenda rasmi ya Afghanistan, Taliban imeanika wazi utambulisho na asili yake ya kweli kuhusu shaari na nembo rasmi za kidini katika nchi hiyo, jambo ambalo zaidi ya kitu kingine chochote, linathibitisha mienendo na nia ya kundi hilo ya kuhodhi kila kitu na kufanya ubaguzi wa kikabila na kimadhehebu dhidi ya makundi mengine ya nchi hiyo.”
Ukweli ni kwamba kwa kufuta mapumziko ya Ashura kutoka kwenye kalenda rasmi ya Afghanistan, kundi la Taliban limeamua kukabiliana na kudhihirisha wazi uadui wake dhidi ya watu wa nchi hiyo. Wengi wanaamini kuwa uamuzi huo unatokana na fikra za kuibua mifarakano na migawanyiko za Taliban zilizoagizwa kutoka nje, fikra ambazo zimelinyima kundi hilo fursa ya kufanya uamuzi wa busara na wakati huo huo kupiga kumbo na kuwatenga wanachama wake wakuu. Fikra hizo potovu sio tu zimelenga shaari na marasimu ya kidini ya watu wa Afghanistan, bali pia zimelenga mila za kitaifa za raia hao kwa kufuta likizo yao ya Nowruz.
Amin Farjad, mtaalamu wa masuala ya Afghanistan anasema:
“Kufutwa likizo ya siku ya mambolezo ya Ashura katika kalenda rasmi ya Afghanistan kumeathiriwa na mawazo ya makundi ya kigaidi na migawanyiko nchini Pakistani, ambayo katika miaka ya hivi karibuni yameshindwa kuitumbukiza Afghanistan katika vita vya kimadhehebu na migawanyiko ya ndani. Hivi sasa makundi hayo yanajaribu kuisukuma Afghanistan katika migogoro na unafiki wa kimadhehebu kupitia tabia, utendaji na fikra hizo potovu.
Kwa vyo vyote vile, kusambazwa ripoti zinazohusiana na kufutwa na Taliban mapumziko na siku ya maombolezo ya Ashura katika kalenda rasmi ya Afghanistan tena katika mwezi mtukufu wa Muharram na katika kukaribia siku za huzuni kubwa katika ulimwengu wa Kiislamu za Tasua na Ashura, ambazo ni siku za kukumbuka kuuawa kinyama mjukuu mpendwa na mtukufu wa Mtume Muhammad (saw) al-Imam Hussein (as), sio tu hakuna maslahi yoyote kwa kundi hilo bali ni hatua inayolitenganisha na watu wa Afghanistan.
Hii ni katika hali ambayo watu wa Afghanistan wanatarajia kwamba Taliban, itatimiza ahadi zake za kuheshimu na kulinda tamaduni za kimadhehebu za watu wa nchi hiyo na kuwaruhusu wafanye na kushiriki vilivyo katika maombolezo makubwa ya Ashura ambayo kama tulivyotangulia kusema huandaliwa kwa ajili ya kukumbuka mauaji ya kikatili yaliyofanywa na maadui wa Uislamu dhidi ya Imam Hussein (as) na wafuasi wake wachache waamini katika jangwa la Karbala nchini Iraq ya leo. Mtukufu huyo alikuwa mjukuu mpendwa wa Mtume Mtukufu wa Uislamu Muhammad al-Mustafa (saw).
Viongozi wa Taliban wanashauriwa kuzingatia maslahi makuu ya Afghanistan na kutoruhusu baadhi ya watu walio na nia mbaya kuibua mifarakano ya kutaka kuigawanya Afghanistan katika misingi ya kimadhehebu, ambayo bila shaka matokeo yake yatakuwa ni kudhoofisha zaidi nafasi ya Taliban katika jamii ya kidini ya Afghanistan.