Baraza la mawaziri la Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Israel Benjamiin Netanyahu halijafikisha hata muda wa mwezi mmoja ambapo tayari linakabiliwa na hatari ya kusambaratika.
Serikali ya Netanyahu inakabiliwa na matatizo mawili makuu na ya kimsingi ambayo yameifanya ikabiliwe na hatari ya kusambaratika. Tatizo la kwanza ni maandamano makubwa na ya mapema ya wananchi dhidi ya serikali hiyo. Katika siku za hivi karibuni kumeshuhudiwa maandamano makubwa yanayolalamikia sera za serikali yenye misimamo ya kufurutu ada ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu.
Makumi ya maelfu ya wakazi wa ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina zilizopachikwa jina bandia la Israel wameandamana kulalamikia sera za Netanyahu na serikali yake. Maandamano hayo yamekuwa makubwa zaidi katika mji wa Quds unaokaliwa kwa mabavu, Haifa na Tel Aviv. Waandamanaji hao wanakosoa vikali maamuzi yaliyochukuliwa na serikali ya Benjamin Netanyahu ya kubana mfumo wa mahakama wa utawala huo na badala yake kuliongezea mamlaka Bunge na serikali.
Moja ya sifa kuu za maandamano hayo ni kwamba, yana kiongozi na yamekuwa yakiongozwa na kuungwa mkono na mirengo ya upinzani. Maandamano ya usiku wa kuamkia jana yalihudhuriwa pia na Yair Lapid kiongozi wa upinzani na Benny Gantz waziri wa zamani wa ulinzi wa Israel. Kuhudhuria wanasiasa hao wawili katika maandamano hayo ya wananchi dhidi ya serikali ya Netanyahu kuna maana kuwa, mzozo wa kisiasa huko Israel bado haujafikia tamati na kama ilivyokuwa katika mwaka mmoja uliopita ambapo Netanyahu alifanya juhudi kubwa kusambaratisha serikali ya muungano ya Yair Lapid na Benny Gantz, filihali pia wapinzani wake nao wanafanya juhudi kama hizo hizo.
Hii ni katika hali ambayo, sokomoko la kisiasa la takribani miaka minne ya hivi karibuni huko Israel linahesabiwa kuwa moja ya sababu za kukosekana uthabiti wa kisiasa sambamba na kulegalega serikali zilizoingia madarakani huko Israel katika kipindi hiki.
Hivi sasa anga inayotawala huko Israel ina ishara zote za kutokea yale yaliyotokea huko nyuma ambapo sasa baraza la mawaziri la Netanyahu lililoundwa hivi karibuni ambapo halijatatimiza hata mwezi mmoja, linakabiliwa na hatari ya kusambaratika.
Tatizo jingine linaloikabili serikali ya Benjamin Netanyahu na kuwa tishio la kuisambaratisha ni kuchaguliwa baadhi ya wanasiasa kushika nyadhifa za wizara ambao kimsingi hawana ustahiki na sifa za lazima za kushikilia vyeo hivyo. Kwa mujibu wa Mahakama Kuu ya Israel shakhsia hao hawana sifa za kutosha za kushika nyadhifa hizo.
Jumatato iliyopita majaji 9 kati ya kumi wa Mahakama Kuu ya Israel walipiga kura ya kumkataa Aryeh Deri, kiongozi wa chama chenye misimamo mikali cha Shas wakisema hastahiki kuhudumu kama waziri kutokana na kuwa amewahi kuhukumiwa na mahakama.
Baada ya vuta nivutu, jana Jumapili Benjamin Netanyahu alimfuta kazi Aryeh Deri kutoka katika wadhifa wake wa Waziri wa Afya na Masuala ya Ndani. Chama cha Shas cha Deri kilikuwa kimetishia hapo kabla kwamba, kama Netanyahu atasalimu amri mbele ya mahakama na kumuondoa kiongozi wao katika wadhifa wa uwaziri basi chama chao kitajiondoa katika serikali. Chama hicho kina Wabunge 11 na kama kitatekeleza kivitendo tishio lake na kujiondoa katika serikali ya muungano inayoongozwa na Netanyahu ina maana kuwa, Waziri Mkuu huyo atapoteza wingi wa viti Bungeni ambapo kwa sasa ana vitu 64 kati ya 120 vya Bunge la Israel. Hii ina maana kuwa, serikali yake itasambaratika na itakuwa lazima kufanyike uchaguzi mwingine wa Bunge.
Ni kwa kuzingatia hali hii na anga ya kisiasa inayotawala huko Israel ndio maana wachambuzi wa mambo wanatabiri kusambaratika haraka serikali ya Benjamin Netanyahu. Baadhi ya weledi wa mambo wanatahadharisha juu ya uwezekano wa kutokea vita vya ndani.
Yossi Melman, mchambuzi mtajika wa masuala ya kijeshi na kiusalama wa utawala haramu wa Israel sanjari na kuashiria maandamano ya usiku wa kuamkia jana ameandika: ” Leo usiku watu 125,000 wamejitokeza barabarani kuandamana dhidi ya Netanyahu. Mgogoro wa Israel yumkini ukaitumbukiza Israel katika vita vya ndani.”
Hata Isaac Herzog, Rais wa utawala ghasibu wa Israel amesema katika matamshi ambayo hayajawahi kushuhudiwa kutoka kwake kwamba: Israel inaelekea upande wa kugawanyika na kupasuka vipande vipande na hivyo kuna haja ya vyama vya siasa kuzipatia ufumbuzi hitilafu zao.