Kukaribia kumalizika muhula wa serikali ya muda ya Taliban nchini Afghanistan

Msemaji wa serikali ya muda ya Taliban nchini Afghanistan amesema kipindi cha uongozi wa serikali hiyo kitamalizika baada ya muda si mrefu ujao.

Zabihullah Mujahid amevieleza vyombo vya habari katika mji mkuu wa nchi hiyo Kabul kwamba: juhudi mbalimbali zinaendelea kufanywa kwa ajili ya kupatikana mazingira mapya Afghanistan na serikali ya muda kuhitimisha shughuli zake. Mujahid hata hivyo, hakutoa maelezo zaidi kuhusu kumalizika muda huo wa serikali hiyo ya muda ya Taliban.

Kabla ya hapo, Zabihullah Mujahid aliwahi kueleza kwamba, kuundwa serikali rasmi na ya kawaida kunahitaji muda; na kwamba uundaji wake utacheleweshwa hadi utakapopatikana uthabiti zaidi, kuundwa katiba na kuundwa mabaraza ya miji.

Msemaji huyo wa serikali ya muda ya kundi la Taliban alifafanua pia kwamba, uundaji wa serikali rasmi unahitaji muda, Katiba haijatungwa, mabaraza ya miji hayajaundwa na Waafghani wanaoishi nje ya nchi nao pia hawajarudi nchini; na hiyo ndiyo mihimili ya mfumo mpya wa Afghanistan.

Kauli ya msemaji wa serikali ya muda ya Taliban kuhusu kukaribia kumalizika muhula wa kuhudumu serikali hiyo ya muda ya Afghanistan na kuingia kwenye awamu mpya ya utawala, inaonekana kama suala lenye utata mwingi kwa fikra za waliowengi na makundi ya kisiasa ya nchi hiyo; kwa sababu hadi sasa bado haijafahamika wazi ni vipi utakuwa muundo na aina ya utawala ujao unaokusudiwa kuundwa na Taliban nchini Afghanstan baada ya kukamilika shughuli za serikali ya muda.

Bila shaka mtazamo uliopo hivi sasa ndani ya Afghanistan kwenyewe na katika jamii ya kimataifa kuhusu kufikia tamati shughuli za serikali ya muda ya Taliban na kuhusu kipindi cha baada yake ni tofauti kabisa na mtazamo lilionao kundi hilo.

Kwa mtazamo wa jamii ya kimataifa, baada ya kumalizika muhula wa serikali ya muda ya Taliban, inapasa wananchi na makundi ya kisiasa ya Afghanistan waandae kwa pamoja mazingira ya uundaji serikali pana na shirikishi itakayojumuisha jamii zote na mirengo yenye mitazamo tofauti ya kisiasa nchini humo; na serikali mpya itakayoundwa iwe mwakilishi kwa maana halisi, wa wananchi wote wa Afghanistan.

Mbali na hayo, na katika kiwango cha juu zaidi, matarajio yaliyopo ndani na nje ya Afghanistan ni kwamba, licha ya mtazamo ilionao Taliban wa kuwa na sauti ya juu katika mustakabali wa kisiasa wa nchi hiyo, lakini kundi hilo liwe tayari kulinda na kudumisha mfumo wa uchaguzi na msingi wa Jamhuri pamoja na kuheshimu nafasi kuu ya wananchi katika utawala.

Lakini kinyume na mtazamo huo, inavyoonekana kwa uchache ni kuwa, kutokana na yaliyoshuhudiwa katika kipindi cha zaidi ya mwaka mmoja wa kutawala tena Taliban nchini Afghanistan, kundi hilo halionyeshi kuwa linaridhia kutekelezwa katiba ya sasa, ambayo inasisitiza na kutilia mkazo kuwepo mfumo wa uchaguzi na Jamhuri sambamba na kuunda serikali kwa kutegemea kura za wananchi.

Na ndio maana hivi karibuni serikali ya muda ya Taliban ilitangaza kuwa hatua zinachukuliwa za kuunda katiba mpya ya Afghanistan, ambayo itachukua nafasi ya katiba iliyopo.

Kwa kuzingatia kauli na misimamo iliyotangazwa na viongozi mbalimbali wa Taliban, inavyoonekana, mfumo uliokusudiwa kuwepo kwa ajili ya mustakabali wa kisiasa wa Afghanistan ni wa Utawala wa Kiislamu, ambao hauendani na masuala ya msingi ya katiba ya sasa kama uchaguzi, Jamhuri na kuwa na sauti kura za wananchi, kwa sababu katika uongozi wa juu kabisa wa mfumo huo kutakuwa na mtu aitwaye “Amir” atakayekuwa mtawala wa Afghanistan; na watu wengine wote watapaswa wamtii yeye.

Katika hali na mazingira hayo ndipo linapoibuka suali la msingi ndani na nje ya Afghanistan la kwamba, baada ya kumalizika kipindi cha serikali ya muda, kundi la Taliban litaielekeza Afghanistan upande gani? Yataandaliwa kweli mazingira ya kuyashirikisha makabila na jamii zote katika uundaji wa serikali pana na jumuishi, au Afghanistan itaelekezwa upande wa kushupalia zaidi kile kinachoitwa Imarati ya Kiislamu yenye taratibu zingine mpya tu za utekelezaji?

Majibu ya masuali haya yanahitaji kuupa fursa muda, kwa sababu hatua itakazochukua Taliban katika kuratibu aina ya utawala ujao na katiba mpya ya Afghanistan, zitakuwa na nafasi kubwa na muhimu kwa jamii ya kimataifa kuamua ni kwa kiwango izidi kukaza kulegeza kamba katika kuamiliana na kundi hilo.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *