Kumalizika ziara ya Zelenskyy nchini Marekani na uwezekano wa kuendelea vita huko Ukraine

Rais Volodymyr Zelenskyy wa Ukraine amekamilisha ziara yake ya kwanza huko Marekani baada ya kuanza vita huko Ukraine. Hii ni safari ya kwanza nje ya nchi kufanywa na Zelenskyy baada ya kuanza vita huko Ukraine

Akiwa ziarani nchini Marekani, Jumatano usiku Zelenskyy alikutana na kufanya mazungumzo na Rais Joe Biden wa nchi hiyo. Pande mbili zilitoa taarifa baada ya mazungumzo yao na kusisitiza kuendeleza misaada ya kifedha na kijeshi ya Marekani kwa Ukraine na kuzidishwa vikwazo dhidi ya Russia. Kuhusiana na suala hilo, Biden ameidhinisha kutumwa Ukraine mifumo ya ulinzi wa makombora ya Patriot katika kalibu ya misaada mipya ya kijeshi ya Marekani kwa Kiev yenye thamani ya dola bilioni 1.85 na akasema anasubiri kupasishwa kifurushi kingine cha ziada cha misaada cha thamani ya dola bilioni 45 kwa ajili ya Ukraine. Zelenskyy pia ameitaja ziara yake hiyo huko Marekani kuwa ni marhala mpya katika uhusiano kati ya Ukraine na Marekani na kusisitiza juu ya msimamo wake wa huko nyuma mkabala wa kufanya mazungumzo na Russia ili kuhitimisha vita huko Ukraine.

Akihutubia Kongresi ya Marekani, Rais Volodymyr Zelenskyy wa Ukraine amekariri matamshi dhidi ya Russia na Iran na kusema hivi na hapa ninamnukuu: “misaada yenu ya mabilioni ya dola kwa Ukraine iliyopasishwa kwa ajili ya mapambano yetu dhidi ya Russia si msaada wa khiari bali ni kuwekeza katika uga wa usalama wa kimataifa na katika demokrasia. Mapambano ya wanajeshi wa Ukraine dhidi ya Russia yanashabihiana na mapambano ya vikosi vya Marekani dhidi ya Hitler mwaka 1944 na Ukraine kamwe haitasalimu amri mbele ya Russia.” mwisho wa kunukuu.”

Msimamo huo unaonyesha kuwa licha ya kuwepo baadhi ya matakwa kwa lengo la kuhitimisha vita huko Ukraine na kuanza mazungumzo ya amani kati ya Moscow na Kiev, lakini Rais wa Ukraine anadhani kwamba, anaendeleza vita vya kiaidiolojia dhidi ya Russia  ambavyo ni mfano wa mapambano ya Kiliberali ya Marekani dhidi ya Manazi wa Ujerumani. Kwa utaratibu huo, Marekani imeongezeka misaada yake kupitia kifurushi kipya kwa Kiev yenye thamani ya zaidi ya dola bilioni 1.85; na kiujumla misaada hiyo itakuwa ya dola bilioni 45 ambayo itaisaidia serikali ya Ukraine kupanua wigo wa vita vinavyoendelea dhidi ya Russia.

Suala muhimu katika misaada hii tajwa ya Washington kwa Kiev ni mfumo wa ulinzi wa anga na makombora ya Patriot iliyopatiwa Ukraine; hatua iliyosababisha radiamali kali kutoka kwa Russia. Rais Vladimir Putin wa Russia Alhamisi iliyopita alisema kuwa, kutumwa mifumo hiyo ya ulinzi wa anga huko Ukraine kutarefusha vita hivyo. “Kama Marekani itatuma mfumo  wake wa Patriot  huko Ukraine tutauangamiza,” amesema Rais wa Russia.

Nukta muhimu ambayo inatiliwa mkazo na Russia ni lengo la mwisho la Marekani la kutuma misaada yake mikubwa ya kijeshi na zana za kivita huko Ukraine. Kwa mtazamo wa Moscow ni kuwa, Marekani inaendeleza vita hivyo ili kuidhoofisha Russia kadiri inavyowezekana na mwishowe kuigawa nchi hiyo. Jambo hili ndilo ambalo Wamarekani wamekuwa wakilifuatilia tangu zama za Umoja wa Kisovieti.

Kwa mukhtadha huo Putin anasema: Marekani kwa muda mrefu sasa imekuwa ikitekeleza oparasheni katika eneo; na imekuwa ikijihusisha na mzozo dhidi ya Russia kwa muda mrefu, na sio kwamba imeanza operesheni hizo leo tu ​​na baada ya ziara ya Zelensky huko Washington.

Kwa hiyo, inatarajiwa kuwa vita vya Ukraine ambavyo sasa vinakamilimisha mwezi wake wa kumi huku vikiwa vimesababisha vifo vingi vya watu na maafa ya kijeshi na wakati huo huo vikiharibu na kubomoa miundo msingi ya nchi hiyo; si tu kuwa havijamalizika, bali vitaongezeka pakubwa katika miezi ijayo pia kwa kuzingatia msimamo wa Zelenskyy na kupatiwa misaada mikubwa ya kijeshi na Marekani. Bila shaka mara hii kuna uwezekano vita hivyo vikaenea zaidi hadi ndani ya ardhi ya Russia kuliko ilivyokuwa huko nyuma.

Bila shaka, kuendelea kwa vita hivyo kutazidisha uwezekano wa kuenea kwake katika nchi jirani na Ukraine, na hasa Poland au katika Jamhuri tatu za Baltic; hatua ambayo ni sawa na kukabiliana kijeshi moja kwa moja Russia na Muungano wa Kijeshi wa Magharibi (Nato).

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *