Kundi la ‘Arin al Usud laapa kuendelea na muqawama dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel

Kundi la mapambano ya Kiislamu la ‘Arin al Usud (Pango la Simba) linaloendesha mapambano yake katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan huko Palestina limesisitiza kuwa, watu wanaodhani kuwa muqawama umeshindwa, wanajidanganya.

Kundi la muqawama wa Kiislamu la ‘Arin al Usud lilitangaza uwepo wake mwezi Aprili mwaka huu na kuyataka makundi mengine ya Palestina yaliunge mkono.

Shirika la habari la al Maaluma limetangaza kuwa, jana Jumamosi, kundi la ‘Arin al Usud lilitoa taarifa na kusema kuwa, wanamapambano wa kweli wa kambi ya muqawama ni aina tatu. Aina ya kwanza ni wale waliouawa shahidi. Aina ya pili ni wale waliojeruhiwa na kusabilia miili yao katika njia ya muqawama na kundi la tatu ni wapiganaji wa Mwenyezi Mungu ambao wanasubiri kuingia vitani na Wazayuni wakati wote.

Kundi hilo la muqawama wa Kiislamu limesema, hata kama atabakia askari mmoja tu kati yetu ijulikane wazi kwamba askari huyo atapambana hadi tone la mwisho la damu yake kwa ajili ya kuilinda kambi ya muqawama.

Kundi la muqawama la ‘Arin al Usud limehoji kwa kusema: “Ni kwa msingi gani inawezekana kuishi kwa amani na watu ambao wanahalalisha kumwagwa damu zetu? Muqawama utaendelea hadi zitakapokombolewa kikamilifu ardhi zote za Palestina.”

Ni vyema kukumbusha hapa kuwa, vyombo vya habari za Kizayuni vimezinukuu duru za kuaminika za Kizayuni zikisema kuwa, taasisi za usalama za Israel zinaishi kwa wasiwasi mkubwa hivi sasa zikihofia kuzidi kupata nguvu kundi la muqawama la ‘Arin al Usud na kubadilika eneo la Nablus kuwa Jenin nyingine.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *