Kundi la kigaidi lenye uhusiano na mtandao wa Al Qaeda, limekiri kuhusika na shambulio lililofanyika mwishoni mwa wiki lililopita ambalo limeua watu zaidi ya 200 katikati mwa Burkina Faso.
Shambulio hilo lilitekelezwa Jumamosi iliyopita kwenye mkoa wa Barsalogho, umbali wa kilometa 40 kaskazini mwa mji wa kimkakati wa Kaya, ambao wachambuzi wanasema ni ngome ya mwisho ya wanajeshi wanaolinda mji mkuu, Ouagadougou.
Wapiganaji waliokuwa na silaha, waliwashambulia raia waliokuwa wakishirikiana na wanajeshi wa serikali kuchimba mashimo yaliyokuwa yatumike kama kinga kwa wanausalama.
Zaidi ya watu 200 wameuawa na wengine 140 wamejeruhiwa katika shambulizi hilo la kigaidi. Baadhi ya duru zinasema, wanajeshi kadhaa wa Burkina Faso hawajulikani walipo na inadhaniwa kuwa huenda wamechukuliwa mateka na kundi hilo la kigaidi.
Burkina Faso imesitisha ushirikiano wake na nchi za Magharibi ikiwemo Ufaransa katika mapambano dhidi ya makundi ya kigaidi, baada ya nchi hizo kushindwa kuzuia mashambulizi ya kigaidi yanayolenga raia na maafisa usalama katika nchi hiyo na eneo la Sahel barani Afrika kwa ujumla.