Kununuliwa ardhi kwa ajili ya Wazayuni; juhudi za kuyahudishwa Manama

Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya al-Wifah nchini Bahrain amesema kuna mpango wa siri unaotekelezwa kwa lengo la kuanzisha mtaa wa Mayahudi katika sehemu kongwe ya Manama, mji mkuu wa Bahrain.

Tangu mwaka 2020, Bahrain imeanzisha uhusiano wa wazi wa kidiplomasia na utawala haramu wa Israel unaokalia kwa mabavu Quds Tukufu, na uhusiano huo umekuwa ukiimarika katika miaka miwili iliyopita ambapo ubalozi wa utawala huo umefunguliwa mjini Manama nao ubalozi wa Bahrain kufunguliwa mjini Tel Aviv. Bila shaka, kabla ya hapo kulikuwepo na mahusiano kati ya utawala wa al-Khalifa nchini Bahrain na utawala wa Kizayuni lakini mahusiano hayo yalikuwa yakifanyika kwa siri. Kwa mujibu wa ripoti nyingi za kuaminika, tangu kuanza mapinduzi ya wananchi huko Bahrain, utawala wa al-Khalifa umekuwa ukipewa habari za siri na kiusalama na utawala wa Kizayuni kwa lengo la kukandamiza upinzani, uungaji mkono ambao ungali unaendelea hadi leo.

Mpango wa kujenga kitongoji cha Mayahudi huko Manama unaenda sambamba na mchakato wa nchi za Kiarabu kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel. Kwa mujibu wa ripoti za kuaminika, mpango wa kuyahudishwa Manama unalenga kubadilisha takriban asilimia 40 ya mitaa kongwe ya mji huo kuwa njia, majengo na nembo za Kiyahudi, ambapo majengo ya zamani katika mji huo yananunuliwa kwa gharama kubwa ili kufikia lengo hilo.

Mpango huo utakuwa na taathira kadhaa za kiusalama kwa Bahrain.

Jambo la kwanza ni kwamba, mpango kama huo uliwahi kutekelezwa huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu na Wazayuni mwanzoni mwa karne iliyopita, ambapo Wazayuni walinunua sehemu ya ardhi za Wapalestina, na hatimaye kupora ardhi na nyumba zao na kuzigeuza kuwa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni.

Kwa kutilia maanani tabia ya utawala wa Kizayuni ya kupora na kughusubu ardhi na pia udhaifu wa utawala wa al-Khalifa, kuna uwezekano mkubwa kwamba hali ya kusikitisha iliyotokea huko Palestina miaka iliyopita itakaririwa tena huko Bahrain katika siku zijazo. Kuhusiana na suala hilo, Seyyed Morteza Sandi, mmoja wa viongozi wa harakati ya Kiislamu ya al-Wafah nchini Bahrain, ameukosoa vikali utawala wa al-Khalifa kuhusiana na suala hilo na kueleza kuwa dalili zote zinaonyesha kuwa mpango huo ulio dhidi ya maslahi ya Bahrain umepangwa kwa ushirikiano wa karibu na utawala wa al-Khalifa kwa lengo la kuigeuza nchi hiyo katika siku zijazo kuwa Palestina ya pili.

Hali ya pili ni kwamba, kuanzishwa vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi huko Manama kunaweza kuleta mabadiliko ya kiutamaduni na kijamii nchini Bahrain kwa sababu Wazayuni wana rasilimali za kifedha na uungaji mkono mkubwa wa kigeni, na wakati huo huo utamaduni wao wa kijamii na kidini unatofautiana sana na utamaduni wa Kiislamu unaotawala katika nchi hiyo ya Kiarabu. Kwa msingi huo, muundo wa kijamii na kiutamaduni wa Bahrain utapitia mabadiliko makubwa. Bila shaka, kwa kuzingatia kwamba utawala wa al-Khalifa tayari uko mbioni kubadilisha muundo wa kijamii wa watu wa Bahrain kwa kuwapa uraia raia wa kigeni, huenda usiwe na wasiwasi mkubwa kuhusu taathira za Mayahudi nchini humo.

Kuhusiana na suala hilo, Sheikh Isa Qassim, kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Bahrain amesisitiza katika taarifa kwamba, ujenzi wa makazi ya walowezi wa Kiyahudi huko Manama una maana ya kubadilishwa utambulisho wa kitaifa, Kiislamu na Kiarabu na wakati huo huo kupotosha historia ya nchi hiyo na kufuta nyaraka na ushahidi wa uasilia wa raia wake na kuwafungulia milango wavamizi wa Kizayuni, kwa ushirikiano wa utawala wa al-Khalifa.

Jambo la mwisho ni kwamba; lengo kuu la utawala wa al Khalifa la kujenga vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi huko Manama ni kupata uungaji mkono zaidi kutoka kwa utawala wa Kizayuni na Marekani ndani ya Bahrain katika juhudi zake za kukabiliana na watu wa nchi hiyo.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *