Kuondolewa vikwazo Iran; siri ya mafanikio ya mazungumzo ya Vienna

Mazungumzo ya nyuklia ya Iran na kundi la 4+1 linaloundwa na mataifa ya Russia, China, Uingereza, Ufaransa pamoja Ujerumani yaliendelea tena leo huko Vienna Austria maudhui kuu ikiwa ni suala la kuondolewa vikwazo na kutilia mkazo mapendekezo ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusu masuala mawili muhimu, yaani uhakika kwamba vikwazo vimeondolewa na dhamana yake.

Awamu ya nane ya mazungumzo ya Vienna yanayoangazia suala la kuondolewa vikwazo vya kidhalimu na haramu dhidi ya Iran ilianza jana Jumatatu kwa kikao cha Kamisheni ya Pamoja iliyoongozwa na Ali Bagheri Kani, Mkuu Timu ya Mazungumzo ya Nyuklia ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Enrique Mora, Naibu Katibu Mkuu wa Huduma ya Kigeni ya Umoja wa Ulaya.

Katika kikao cha Kamisheni ya pamoja ya JCPOA pande zote akiwemo Mratibu wa Kamisheni ya Pamoja ya JCPOA alisisitiza kuhusiana na kuwa na mafanikio duru ya mazungumzo ya hapo kabla na kukiri kwamba, kumepigwa hatua nzuri katika duru iliyopita ya mazungumzo hayo na kimsingi kumeandaliwa fremu inayofaa kwa ajili ya kusukuma mbele gurudumu la mazungumzo hayo.

Mikhail Ulyanov, mwakilishi wa Russia katika mazungumzo ya Vienna alisema mwishoni mwa kikao cha Kamisheni ya Pamoja ya JCPOA kwamba, duru mpya ya mazungumzo ina muelekeo wa kiutendaji na kujikita katika natija na kubainisha kwamba, washiriki wa mazungumzo hayo wameafiki kuanza kwa umakini mchakato wa uandishi wa rasimu ili makubaliano yafikiwe haraka iwezekanavyo.

Enrique Mora, Naibu Katibu Mkuu wa Huduma ya Kigeni ya Umoja wa Ulaya na mratibu wa kikao cha kamisheni ya pamoja ya makubaliano ya nyuklia ya JCPOA naye ametangaza kuwa, kuna ishara chanya za mafanikio katika duru ya nane ya mazunguzmo. Pande zote husika zimeonyesha utayarifu wa kupatiwa ufumbuzi hitilafu kama ambavyo wote wameahidi kuhakikisha kunafikiwa natija inayofaa.

Duru ya saba ya mazungumzo ya Vienna katika serikali mpya ya Iran ilianza Novemba 29 katika mji mkuu wa Austria; na hatimaye Iran tarehe Mosi mwezi huu wa Disemba iliwasilisha rasimu mbili kuhusu kuondolewa vikwazo vya upande mmoja vya Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kuhusu miradi ya nyuklia ya nchi hiyo. Mazungumzo hayo yalianza baada ya kusimama kwa miezi mitatu katika anga ya propanda ya Marekani na madola matatu ya Ulaya ya Uingereza, Ufaransa na Ujerumani kwa madai kwamba, ujumbe wa Iran umekwenda Vienna bila ya mpango maalumu na lengo ni kupoteza muda.
Jamhuri ya Kiisalamu ya Iran ikiwa nchi yenye kukubali na kutekeleza majukumu ilitangaza kwamba, kwa kuzingatia kuwa, Marekani ndiyo upande uliokiuka makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na madola matatu ya Ulaya ambayo ni wanachama wa makubaliano hayo hayakuchukua hatua yoyote athirifu kwa ajili ya kutekeleza ahadi zao, hivyo basi kwanza vikwazo vyote dhidi ya Tehran vinapaswa kuondolewa na kisha na taifa hili lijiridhishe na kupata dhamana ya utekelezwaji wa ahadi za Washington.

Ali Bagheri Kani, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alisema baada ya kikao cha jana usiku cha Kamisheni ya Pamoja huko Vienna kwamba, msingi wa mafanikio ya mazungumzo hayo ni kufikia makubaliano ya kuondolewa kikamilifu vikwazo dhidi ya Iran. Bagheri Kani amesisitiza kuwa, wawakilishi wa nchi mbalimbali katika kikao cha Vienna wamesisitiza umuhimu na kutoa kipaumbele kwa suala la kuondolewa vikwazo na jinsi ya kuthibitisha kwamba suala hilo limetekelezwa na dhamana yake imepatikana katika awamu ya nane ya mazungumzo ya Vienna.
Hapana shaka kuwa, filihali pande zinazoshiriki katika mazungumzo ya nyuklia ya Vienna zimekubali kuendelezwa mazungumzo kuhusiana na suala la kuondolewa vikwazo na kutilia mkazo mapendekezo ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusu masuala mawili muhimu, yaani uhakika kwamba vikwazo vimeondolewa na kupatikana dhamana yake.

Kwa mtazamo wa Iran ni kuwa, natija ya mazungumzo hayo inategemea nia ya dhati na kukubali majukumu ya pande nyingine katika mazungumzo hayo hususan madola ya Magharibi ambapo kwa kuchukua hatua athirifu ya kuondolewa vikwazio na kutekeleza ahadi zao, yatakuwa yameandaa uwanja wa kufikiwa makubaliano ambayo yatadhamini maslahi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *