Kuongezeka idadi ya Wazayuni waliokimbia kutoka ardhi za Wapalestina mwaka 2022

Vyombo vya habari vya Kiibrania vimetangaza karibuni kwamba idadi ya Wazayuni waliokimbia kutoka ardhi za Wapalestina zinazokaliwa kwa mabavu mwaka uliopita wa 2022 kutokana na mapambano makali ya Waplestina dhidi ya askari vamizi wa utawala wa Israel iliongezeka sana.

Katika miaka iliyopita Wazayuni wamekuwa wakihamia katika ardhi za Wapalestina zinazokaliwa kwa mabavu na utawala ghasibu wa Israel kama njia bora zaidi ya kuzidisha idadi yao kwenye ardhi hizo. Mayahudi kutoka pembe zote za dunia wamekuwa wakihamia katika ardhi hizo zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni baada ya kuhadaika na ahadi mbalimbali zinazotolewa na watawala wa Kizayuni zikiwemo za kupata maisha bora na rahisi, lakini katika miaka ya hivi karibuni mwenendo huo wa uhajiri wa Wazayuni kuelekea ardhi za Wapalestina umebadilika na kuwa kinyume na ilivyotarajiwa na watawala hao.

Ingawa katika mwaka 2022 ikilinganishwa na 2021, uhamiaji kwenda maeneo yanayokaliwa kwa mabavu ulikuwa karibu mara mbili na nusu na kufikia takriban watu elfu 29 hadi elfu 70, lakini ni wazi kuwa ongezeko hilo lilitokana na vita vya Ukraine. Kulingana na takwimu rasmi zilizotangazwa mnamo 2022, wahamiaji 37,364 kutoka Russia na wahamiaji 14,680 kutoka Ukraine walihamia katika maeneo ya Wapalestina yanayokaliwa kwa mabavu, jambo linaloonyesha kuwa ni watu 18,000 pekee kutoka nchi zingine ndio walifika katika maeneo hayo yanayokaliwa kwa mabavu na Wazayuni.

Hakuna takwimu kamili zilizochapishwa kuhusu idadi ya watu waliohama kutoka ardhi hizo zinazokaliwa kwa mabavu, lakini vyombo vya habari vya Kizayuni vimetangaza kwamba uhamiaji wa kinyumenyume wa Wazayuni kutoka ardhi hizo uliongezeka sana mwaka 2022. Kituo cha Sera ya Uhamiaji cha utawala ghasibu wa Israeli kilichambua data ya Ofisi Kuu ya Takwimu ya Israeli ya 2022 na kutangaza kuwa katika mwaka huo idadi ya Mayadudi wanaoishi katika ardhi za Wapalestina zilizoghusubiwa na Israel ilipungua kwa aisilimia 0.3.

Kwa mujibu wa takwimu hizo, idadi kubwa ya Mayahudi katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu ilipungua kutoka asilimia 73.9 mwishoni mwa 2021 hadi asilimia 73.6 mwishoni mwa mwaka 2022, hivi kwamba uwiano wa Mayahudi wengi katika Palestina inayokaliwa kwa mabavu ilipungua kwa asilimia 10 katika miongo 3 iliyopita, idadi ambayo yenyewe inaashiria kuondoka kwa idadi kubwa ya Wazayuni kutoka ardhi za Wapalestina zinazokaliwa kwa mabavu na kurejea katika nchi walizotoka au kuhamia katika nchi nyingine za dunia.

Siku chache zilizopita, gazeti la Kizayuni la Jerusalem Post liliandika kwamba, idadi ya Waarabu katika Palestina inayokaliwa kwa mabavu imeongezeka kwa takriban watu laki nne katika kipindi cha miaka kumi iliyopita; ambapo kati ya mwaka 2008 na 2018, idadi ya Waarabu katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu iliongezeka kwa asilimia 21, wakati idadi ya Mayahudi iliongezeka kwa asilimia 17.5.

Kuna sababu nyingi zinazosababisha uhamiaji wa kinyumenyume wa Wazayuni kutoka ardhi zinazokaliwa kwa mabavu, baadhi ya sababu muhimu zaidi zikiwa ni pamoja na:

Kuongezeka kwa hisia ya kutokuwa na usalama, ambayo imekuwa ikiongezeka tangu 2000, na katika miaka ya karibuni, hisia hiyo imekuwa ikionekana wazi kati ya Mayahudi wanaoishi kwa mabavu katika ardhi za Wapalestina. Ni mwaka 2021 tu, ambapo baada ya vita vya Seif al-Quds, Mayahudi wapatao 16,000 walihama kutoka ardhi zinazokaliwa kwa mabavu kwa hofu ya kupoteza maisha na mali zao. Kwa kuongezeka mapambano ya silaha katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, inatarajiwa kwamba idadi ya uhamiaji wa kinyumenyume itaongezeka tena.

Sababu nyingine ni kuongezeka kwa hali ya kutokuwa na imani na uwezo wa jeshi la Kizayuni katika kuudhaminia utawala wa Kizayuni usalama wake katika vita vyovyote vinavyoweza kutokea, hasa kutokana na kwamba maadui wa Israel wameongeza nguvu zao za kijeshi.

Sababu nyingine ni kuongezeka mirengo yenye misimamo mikali katika mfumo wa utawala wa Kizayuni. Kufuatia uchaguzi wa hivi karibuni wa bunge la Wazayuni, Netanyahu aliunda baraza la mawaziri wenye mielekeo na itikadi kali za ubaguzi wa Kiyahudi, suala ambalo limeogeza malalamiko katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu.

Jambo la mwisho ni kwamba hapo awali, kukimbia na kutoka Mayahudi huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu kulionekana tu miongoni mwa watu wa kawaida, lakini leo hii tatizo hilo linaonekana wazi katika tabaka la wasomi na Wazayuni wenye shahada za juu za vyuo vikuu, wataalamu na matabaka mengine muhimu ya Wazayuni wanaoishi katika ardhi hizo.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *