Bunge la Seneti la Marekani limefanya kikao kuchunguza ongezeko la uhalifu wa chuki katika nchi hiyo.
Wakati huo huo, hotuba za chuki zilizotolewa na maseneta wa Marekani katika kikao hicho dhidi ya mwanaharakati mashuhuri wa haki za Waislamu, imekabiliwa na ukosoaji mwingi. Hii ina maana kwamba, chuki nchini Marekani imeongezeka na kushadidi zaidi dhidi ya Waislamu kuliko jamii wafuasi wa dini nyingine katika nchi hiyo. Kwa kadiri kwamba, Baraza la Uhusiano wa Marekani na Uislamu (CAIR), likiwa ndilo shirika kubwa zaidi la kutetea uhuru wa kiraia wa Waislamu nchini Marekani, hivi karibuni lilichapisha ripoti kuhusu ongezeko la malalamiko yanayohusiana na ubaguzi na chuki dhidi ya Waislamu kote Marekani na kutangaza kwamba, suala hili limefikia kiwango cha juu zaidi mwaka jana 2023 katika miaka 30 iliyopita.
Ripoti zilizochapishwa zinaonyesha kuwa, ukatili na chuki dhidi ya Waislamu nchini Merekani vimeongezeka kwa 57% tangu kipindi cha urais wa Donald Trump mnamo 2016. Ripoti hiyo imeonyesha kuwa, karibu asilimia 20 ya watu wa jamii ya Marekani wanatumia lugha ya matusi dhidi ya Waislamu, ambayo kwa namna fulani inatambuliwa kuwa ni chuki dhidi ya Uislamu (Islamophobia).
Ripoti ya Baraza la Mahusiano ya Kiislamu ya Marekani (CAIR) inasema kuwa, miongoni mwa sababu za ongezeko kubwa la chuki dhidi ya Waislamu nchini Marekani ni taathira za vita vya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya taifa la Palestina. Baraza hilo limedokeza kwamba, katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita ya mwaka huu wa 2024, limepokea idadi kubwa ya malalamiko ya hujuma dhidi ya Uislamu, yaani kesi 3578, na kwamba kesi nyingi zilihusiana na ubaguzi katika sekta ya ajira na elimu dhidi ya Waislamu. Waajiri, vyuo vikuu na shule za Marekani zinafanya ubaguzi mkubwa dhidi Waislamu, na kuwakandamiza zaidi watu wanaopinga mauaji ya kimbari ya Israel huko Gaza na kutaka haki za Wapalestina zizingatiwe.
Baada ya kuongezeka jinai za Wazayuni huko Gaza kulikochochea uungaji mkono wa wananchi kwa Wapalestina huko Marekani, shule mbalimbali zilizuia kuhudhuria darasani kwa wanafunzi wenye mafungamano au wanaoitetea Palestina, na pia baadhi ya waajiri wamezuia kuajiriwa watu wanaoiunga mkono na kuitetea Palestina.
Takwimu za makundi ya kutetea haki za binadamu nchini Marekani pia zinaonyesha kuwa, ubaguzi na mashambulizi dhidi ya Waislamu na Wapalestina nchini humo yalifikia kiwango kisicho na kifani mwaka 2023. Ripoti zinaeleza kuwa 2023 ulishuhudia kuzuka upya kwa chuki dhidi ya Waislamu baada ya kushuka katika mwaka wa kabla yake. Katika miezi tisa ya kwanza ya 2023, matukio kama hayo yalikuwa wastani wa kesi 500 kwa mwezi, na zilifikia kesi 1200 kwa mwezi katika robo ya mwisho ya mwaka.
Kesi hizi za ukati na ubaguzi zinatokea katika nchi inayodai kuwa kinara wa kutetea haki za binadamu na kujipa hadhi ya kuwa mwalimu na mhadhiri wa haki za binadamu kwa nchi nyingine duniani!