Kiwango cha talaka na wanandoa kuachana kimeongeza mno nchini Saudi Arabia katika miaka ya hivi karibuni na kutishia mustakabali wa familia nyingi katika nchi hiyo inayoongozwa kwa mfumo wa kifalme wa kifamilia.
Takwimu zinaonyesha kuwa, matukio saba ya talaka na kuachana wanandoa hushuhudiwa kila baada ya saa moja nchini Saudi Arabia.
Aidha kwa mujibu wa mtandao wa Habari wa Kiarabu wa 21 ni kuwa, utafiti mpya uliofanywa unaonyesha kuuwa, kiwango cha talaka kimeongezeka mno katika jamii ya Saudi Arabia ambapo kwa wastani talaka 168 hutokea kwa siku nchini humo.
Gazeti la al-Yaum la Saudia limefichua kwamba, takwimu za idara ya takwimu ya nchi hiyo zinaonesha kuwa, kiwango cha talaka kimeongezeka mara sita katika kipindi cha miaka kumi ya hivi karibuni.
Kadhalika takwimu hizo zinaonesha kuwa, ndoa tatu kati ya kila ndoa kumi hazidumu na badala yake huishia katika talaka ikiwa na maana kwamba, theluthi moja ya ndoa zote nchini Saudia huishia kwenye talaka la kuachana kila mwaka.
Inaelezwa kuwa, mafaili ya talaka katika mwaka 2020 yalipindukia 57,000 huku baadhi ya kesi za talaka zikiwa hazisajiliwi.
Viongozi wa Saudia wametangaza kuwa, wana mpango wa kuunda kamati maalumu ambayo itachunguza na kutoa ripoti kuhusiana na sababu hasa ya kuongezeka pakubwa kiasi hiki suala la wanandoa kuachana.
Taathira mbaya ya mitandao ya kijamii inatajwa kuwa moja ya sababu za kuongezeka talaka katika jamii ya Saudi Arabia kutokana na baadhi ya wanandoa kujishughulisha na mitandao hiyo ya kijamii na kuacha majukuumu yao au kuiga mitindo ya maisha wa watu mashuhuri.
Wajuzi wa mambo wanasema kuwa, kuvurugika uchumi na ugumu wa maisha nchini Saudia ni sababu nyingine inayochangia kuongezeka idadi na kiwango cha talaka nchini Saudia.