Wizara ya Mateka na Wafungwa wa Kipalestina Walioachiliwa Huru kutoka gerezani imetangaza kuwa, hivi sasa kuna watoto 170 wa Kipalestina katika magereza ya Israel huku watano kati yao wakishikiliwa pasi na kuelezwa tuhuma na makosa yao.
Takwimu mbalimbali zinaonesha kuwa, katika hali ya wastani watoto na mabarobaro zaidi ya 1000 wa Kipalestina hutiwa mbaroni kila mwaka kwa visingizio mbalimbali na kisha kufanyiwa mateso ya kiroho na kimwili wakiwa gerezani.
Licha ya kuwa kutiwa mbaroni, kushikiliwa na kuteswa watoto na mabarombaro wa Kipalestina katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu ambazo zimepachikwa jina bandia la Israel ni kinyume kabisa na misingi na kanuni za kimataifa na kwa kuzingatia kwamba, siyo wanajeshi, hivyo kuwatesa na kuwadhalilisha ni mfano wa wazi wa jinai za kivita, lakini mahakama za Israel zinahalalisha kuwatia mbaroni na kuwahukumu vifungo watoto wadogo wa Kipalestina.
Kwa msingi huo, moja ya sababu kuu za kuendelea kutiwa mbaroni na kushikiliwa magereza watoto na vijana mabarobaro wa Kipalestina licha ya hatua hizo kukinzana na sheria na kanuni zote za kimataifa ni kuwa, utawala haramu wa Israel kutokana na kujiona bora na kuwa na mitazamo ya kibaguzi hauoni kama ulazimika kutekeleza sheria hizi. Kutokana na satwa na kupenya umafia wa Kizayuni katika asasi za kimataifa na vilevile himaya na uungaji mkono wa madola ya Magharibi kinara wao ikiwa Marekani, hakuna wakati ambao utawala huo ghasibu umeandamwa kwa mashinikizo makubwa ya kimataifa na ya kuutia kiwewe ili ubadilishe mwenendo wake.
Kamakatakamata yenye wigo mpana na mtawalia dhidi ya watoto na vijana wadogo wa Kipalestina ina sababu tofauti:
Sababu ya kwanza ni kuwa, utawala haramu wa Israel unawatazama watoto wa leo wa Kipalestina kwa jicho la wanamapambano wa kesho na kwa uoni wake ni kuwa, kuwatia mbaroni na kuwatia jela ni sawa na kuziba ufa kabla ya kujenga ukuta. Hata hivyo Israel imeghafilika kwamba, hatua hizo zina matokeo hasi pia, kwani irada na azma ya watoto na mabarobaro wa Kipalestina inazidi kuimarika siku baada ya siku katika kupambana na Wazayuni maghasibu. Ukweli wa mambo ni kuwa, kuundwa makundi mapya ya muqawama katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan ni matokeo ya wazi kabisa ya tathmini hii.
Sababu ya pili ni kuwa, siasa za utawala vamizi wa Israel katika miaka yote hii na katika miongo iliyopita katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Ukanda wa Gaza zimeyabadilisha maeneo hayo ni kuwa magereza makubwa.
Licha ya kuwa, baada ya miaka mingi utawala dhalimu wa Israel ulilazimika kurejea nyuma na kukimbia kutoka katika Ukanda wa Gaza kama ulivyoondoka kwa madhila huko kusini mwa Lebanon kutokana na kuimarika muqawama na mapambano ya wananchi, lakini umeliwekea mzingiro eneo hili lenye wakazi zaidi ya milioni mbili na hivyo kuwaadhibu kwa umati wakazi wake ambao wanakosa huduma muhimu na za awali kabisa kama maji, chakula na dawa.
Katika eneo la Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan kumejengwa zaidi ya vitongoji haramu 200 na kuwekwa humo zaidi ya walowezi laki tano wa Kizayuni sambamba na kujengwa ukuta wa kibaguzi katika ukingo huo wa magharibi na hivyo kulitenga eneo hilo na kimsingi wakazi wa maeneo yote mawili wamo katika gereza kubwa.
Katika mazingira kama haya, Wapalestina wanaoishi katika maeneo hayo ili waondokane na magereza haya makubwa na kuwa huru, hawana njia nyingine isipokuwa kudumisha muqawama na mapambano yao dhidi ya Wazayuni maghasibu. Na ndio maana hata kutiwa mbaroni na kuingizwa katika magereza ya Israel hakuwashughulishi kwani wanaamini kuwa, hata hivi sasa maisha yao hayana tofauti na ya gerezani.
Ni kwa muktadha huo ndio maana kuwatia mbaroni na kuwafunga jela Wapalestina iwe ni watu wazima au watoto wadogo hakubadilishi kitu katika maisha yao kama ambavyo hakutii doa na dosari yoyote katika azma na irada yao ya mapambano dhidi ya Israel. Hata hivyo haipaswi kusahau kwamba, hatua hizi za kinyama za Israel zinazidi kulifanya faili la Tel Aviv la jinai za kivita liwe zito siku baada ya siku.
Hii ni kutokana na kuwa, kwa mujibu wa kanuni na sheria za kimataifa ukiwemo mkataba wa Geneva, kufanya mabadiliko katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na kuwaudhi, kuwatesa na kuwasumbua wakazi wake kunahesabiwa kuwa ni jinai za kivita ambazo zinapaswa kufuatiliwa kisheria. Hata hivyo kutokana na nguvu na satwa za mamafia wa Kizayuni katika asasi za kimataifa sambamba na hatua ya madola ya Magharibi yakiongowa na Marekani ya kuuunga mkono utawala huo bandia sanjari na kuupendelea, kumelifanya suala la kufuatiliwa kisheria Israel hadi sasa lisifuatiwe na kutekelezwa kikamilifu na kwa mujibu wa sheria.