Suala la kudhaminiwa mahitaji ya gesi kwa nchi za Ulaya sasa limekuwa tatizo sugu kwa nchi hizo. Nchi za Ulaya, ambazo ziliamua kuiwekea Russia vikwazo vya kila aina ili kuishinikiza katika vita vya Ukraine, sasa zinaituhumu Moscow kwamba inaitumia gesi kama silaha ya vita.
Kabla ya kuanza vita vya Russia na Ukraine, Moscow ilikuwa moja ya wauzaji wakubwa zaidi wa gesi kwa Ulaya, kutokana na kudhamini zaidi ya 40% ya gesi inayotumiwa na nchi hizo. Lakini baada ya kuanza vita hivyo, na nchi za Ulaya kuamua kuiunga mkono Ukraine, nchi hizo zilichukua hatua ya kuiwekea vikwazo mbalimbali Russia. Kuisusia sekta ya nishati ya Russia na kupunguza ununuzi wa gesi ya nchi hiyo ni hatua zingine walizotangaza na kuanza kutekeleza viongozi wa nchi za Ulaya kwa matakwa na maelekezo ya Marekani.
Kwa hakika viongozi wa nchi za bara la Ulaya walichukua hatua ya kuiwekea Russia vikwazo vya kiuchumi ili kuiweka nchi hiyo kwenye mbinyo na mashinikizo katika vita vya Ukraine; lakini hadi sasa sera hiyo imekuwa na matokeo kinyume kwa nchi hizo. Kutokana na kuwekewa vikwazo, kupunguza nchi za Ulaya gesi inayonunua kutoka Moscow na kusita kuipatia vipuri inavyohitajia kwa ajili ya ukarabati wa mabomba ya mafuta, Russia nayo iliamua kujibu mapigo kwa kupunguza uuzaji gesi yake kwa Ulaya, kiasi kwamba hivi sasa nchi za bara hilo zina hofu kuwa, hazitaweza kujidhaminia fueli wakati wa msimu wa baridi kali. Isitoshe, kutokana na kupanda bei za bidhaa zinazotegemea nishati, uchumi wa Ulaya umeathirika sana. Biashara na shughuli nyingi ziko hatarini kufungwa kutokana na ughali wa umeme; na raia wengi wa nchi za Ulaya hawana uwezo wa kulipa bili zao za umeme na gesi. Hali hii imewatia wasiwasi viongozi wa nchi mbalimbali za Ulaya wa kuzuka maandamano na malalamiko ya kijamii.
Licha ya kujitokeza hali hiyo na kuendelezwa sera za Ulaya za uwekaji vikwazo, wakuu wa nchi za bara hilo wanajaribu kuonyesha kuwa Russia ndiyo inayopasa kubebeshwa mzigo wa lawama. Viongozi wa Ulaya wanadai, Moscow inatumia gesi kama silaha ya vita na kwamba imeanzisha vita vya gesi dhidi ya nchi hizo.
Hata hivyo Russia kwa upande wake imekuwa ikikanusha kila mara madai hayo. Dmitry Peskov, msemaji wa rais wa Russia amesema, “Moscow haina nia ya kukata moja kwa moja usambazaji gesi kwa nchi za Ulaya. Russia ina jukumu la kudhamini gesi; -na bila kujali kile kinachosemwa katika Tume ya Ulaya, katika miji mikuu ya Ulaya na Marekani-, Russia ilikuwa, iko hivyo sasa, na itaendelea kwa kiwango kikubwa kuwa mdhamini wa usalama wa nishati kwa Ulaya”. Lakini wakati huo huo Peskov ameonya kwamba, ikiwa Ulaya itaendelea kufuata njia iliyochagua ya kuweka vizuizi na vikwazo, hali ya mambo itabadilika kikamilifu.
“Kevin Book, Mkurugenzi Mkuu wa shirika la utafiti la Clearview Energy Partners anasema: Hali ya sasa ya gesi asilia ni kama ilivyokuwa ya mafuta katika muongo wa 1970. Dunia hivi sasa inafikiria kuhusu gesi, sawa na ilivyokuwa wakati fulani ikifikiria kuhusu mafuta; na mchango mkuu ambao gesi inatoa katika chumi za kisasa na kuhitajika kwake katika kudhamini na kuwezesha kuwepo anuai za vyanzo vya nishati kumeshabainika kwa uwazi zaidi.”
Viongozi wa Ulaya ambao wameshapoteza matumaini ya kupata vyanzo mbadala vya gesi ya Russia huku wakiwa wamefeli pia katika mipango yao ya kujiwekea akiba ya gesi, wameamua kuanzisha juhudi nyingine mpya. Kwa mfano, Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa ametaka kiitishwe kikao cha Baraza la Ulinzi wa Nchi baada ya usafirishaji gesi ya Russia kwenda Ufaransa kusimamishwa. Kwa kuchukua maamuzi hayo, serikali ya Ufaransa inatarajia kwamba itaweza kulifungamanisha suala la kupanda kwa bili za umeme na gesi nchini humo na masuala ya usalama na ulinzi wa taifa ili kupata fursa ya kuweza kukabiliana na maandamano ya malalamiko ya kijamii, ambayo yanatabiriwa kutokea wakati wa msimu wa baridi kali.