Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limepasisha azimio la haki ya taifa la Palestina ya kujiamulia hatima yake. Tangu mwaka 1948, Palestina imeshuhudia hali iliyopelekea kunyakuliwa eneo lake la kijiografia kwa kadiri kwamba hivi sasa asilimia 85 ya jiografia ya Palestina inakaliwa kwa mabavu na utawala wa Kizayuni wa Israel.
Sababu kuu ya hali hii ni tabia na mienendo ya kupenda kujitanua zaidi ya Wazayuni maghasibu, himaya na misaada ya madola ya kibeberu kwa Wazayuni hao na kutowajibika kwa Umoja wa Mataifa. Kupasishwa azimio linalotambua haki ya watu wa Palestina kujiamua hatima yao katika Umoja wa Mataifa ni hatua inayothibitisha tena haki yao katika eneo la kijiofrafia la Palestina. Azimio hili linasisitiza haki ya wananchi wa Palestina, popote pale walipo, ya kujiamulia hatima yao wenyewe na kupata uhuru, na inalitambua kuwa ndio sharti kuu la kupatikana suluhisho la kiadilifu na kamili kwa kadhia ya Palestina. Nchi 168 zimepiga kura kuunga mkono azimio hilo, nchi sita zimelipinga, na nane hazikushiriki katika upigaji kura. Uungaji mkono wa nchi 168 kwa azimio hilo ni kielelezo cha himaya na ungaji mkono wa walimwengu kwa taifa la Palestina kwa ajili ya kuunda nchi yake katika eneo maalumu la kijiografia.
Hisham Qasim, mjumbe wa harakati ya Hamas amesema kuwa: “Uungaji mkono wa kiwango cha juu wa jamii ya kimataifa kwa azimio hili unaonyesha imani inayoongezeka ya duru za jumuiya ya kimataifa kuhusu ulazima wa kutimizwa haki ya kuainisha hatima ya taifa la Palestina, kukomeshwa uvamizi na kukaliwa kwa mabavu ardhi ya taifa hilo na kuhukumiwa viongozi wa Tel Aviv kwa uchokozi na jinai zao za umwagaji damu dhidi ya taifa hilo.”
Azimio hilo lina jumbe mbili muhimu. Wa kwanza ni kwamba Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ni taasisi inayotawaliwa na madola makubwa ambayo bayawezi kutekeleza majukumu yao bila ya kuingiza mielekeo na matashi ya kisiasa na hayatilii maanani mfumo wa uadilifu. Hii ni licha ya kwamba, nchi nyingi duniani zinaunga mkono haki za taifa la Palestina na kulaani uvamizi wa utawala wa Kizayuni. Hata hivyo Baraza la Usalama halitaki kusikia sauti ya walimwengu waliowengi.
Kwa uungaji mkono wa wanachama watatu wa kudumu wa Baraza la Usalama yaani Marekani, Uingereza na Ufaransa, baraza hili halipitishi azimio lolote la kuiunga mkono Palestina dhidi ya utawala wa Kizayuni, na wala wanachama hao watatu wa Kimagharibi hawaruhusu kijadiliwa jinai zinazofanywa na Israel dhidi ya Wapalestina.
Ujumbe mwingine ni kwamba, japokuwa kupitishwa kwa azimio la kuwaunga mkono Wapalestina katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ni hatua mwafaka, lakini inatupasa kusema kuwa maazimio ya aina hii hayana athari katika suala la Palestina na jinai zinazofanywa na Tel Aviv, kwa sababu maazimio ya Baraza Kuu hayana dhamana ya utekelezaji. Mwanzoni mwa mwezi huu pia Baraza Kuu la UN lilipasisha maazimio matano kwa maslahi ya Palestina.
Ukweli ni kwamba, Umoja wa Mataifa unaweza kujiondoa katika hali yake ya kutokuwa athirifu kuhusu kadhia ya Palestina na kuwa na nafasi muhimu zaidi pale madola makubwa ya yanayodhibiti jumuiya hiyo ya kimataifa yakapositisha uungaji mkono na hiyama yao kwa utawala katili wa Israel.
Kuhusiana na suala hilo Riyad al-Maliki, Waziri wa Mambo ya Nje wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina amezitaka nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kutekeleza wajibu wao katika kuliunga mkono taifa la Palestina na haki zake na kuchukua hatua za kivitendo kukabiliana na wavamizi wa ardhi ya Palestina.