Balozi wa Imarati amerejea hapa Tehran baada ya kupita miaka saba ambapo katika mazungumzo yake na Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiiislamu ya Iran amesisitizia suala la kukuzwa na kuimarishwa uhusiano baina ya pande mbili.
Akizungumza siku ya Jumanne na Hussein Amir-Abdollahian, Saif Mohammed Al Zaabi, balozi wa Imarati nchini Iran ameonyesha kuridhishwa kwake na kurejea tena hapa Tehran na kubainisha kwamba, uwezo mkubwa wa kiuchumi na kibiashara baina ya nchi mbili ni sababu muhimu ya kuinua kiwango cha ushirikiano baina ya pande mbili ambapo amebainisha pia mitazamo ya viongozi wa ngazi za juu wa Imarati kuhusianan na suala la ujirani mwema. Aidha ametaka kuwa amilifu kamati za pande mbili na kuweko ubadilishanaji jumbe za pande mbili.
Imarati ni moja ya mataifa jirani na Iran, ingawa uhusiano wa nchi hiyo na Iran umekuwa ukizingatia madai yasiyo na msingi kabisa ya ardhi sambamba na matukio mengine ya nje.
Imarati imekuwa ikidai umiliki wa visiwa vitatu vya Bumussa, Tomb Kubwa na Ndogo ambavyo kwa mujibu wa nyaraka za kihistoria za kuaminika visiwa hivyo ni sehemu ya ardhi ya Iran.
Jambo muhimu zaidi katika uhusiano wa Iran na Imarati ni vigezo vya nje. Imarati licha ya kuwa inadai kujitawala na kuwa na maendeleo, lakini daima imekuwa ikifuata kibubusa siasa za Saudi Arabia katika eneo la Asia Magharibi ambapo hali hii hususan katika miaka ya hivi karibuni imedhihiri na kuonekana bayana zaidi. Vita dhidi ya Yemen na kukata uhusiano na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Qatar ni mifano miwili ya wazi ya Abu Dhabi kufuata siasa za Riyadh katika eneo.
Mwaka 2016 Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) ukiwa na lengo la kuiunga mkono Saudia na kadhalika kuishinikiza Jamhuri ya Kiislamu ya Iran uliamua kukata uhusiano wake na Tehran, na fauka ya hayo ukaamua kuwa pamoja na Marekani katika sera zake dhidi ya Tehran.
Imarati ilichukua mkondo wa siasa hizo dhidi ya Iran katika hali ambayo, kwa upande mmoja Tehran daima imekkuwa ikisisitiza siasa za ujirani mwema na ni mara chache sana kumeibuka mzozo baina ya pande mbili katika hali ya kuchukua maamuzi kwa kujitegemea. Aidha katika upande wa pili kulikuwa na uhusiano imara mno wa kibiashara baina ya Tehran na Abu Dhabi.
Kuna nukta kadhaa muhimu kuhusiana na kurejea tena balozi wa Imarati hapa Tehran baada ya kupita miaka saba.
Nukta ya kwanza ni kuwa, hadi sasa siasa za Imarati zingali zinafuata utendaji wa Saudia, kwani katika kipindi cha miaka miwili iliyopita kiwango cha mvutano katika uhusiano wa Tehran na Riyadh kimepungua na pande mbili zimechukua hatua za kuhuisha uhusiano wao. Ni kutokana na sababu hiyo, ndio maana Imarati nayo imechukua hatua ya kuhuisha uhusiano wake na Iran.
Nukta ya pili ni kwamba, aina hii ya muelekeo wa Imarati katika sera zake za kigeni inaonyesha kuwa, licha ya kuwa nchi hiyo kwa upande wa kiuchumi inapiga hatua na imo katika nchi zenye ustawi kimaendeleo katika eneo, lakini bado haina uwezo wa kusimama yenye na kujitegemea katika maamuzi na kudhihiri yenyewe kama nchi yenye taathira katika eneo.
Nukta ya tatu ni kuwa, kustawisha uhusiano na Iran ni jambo linalodhamini maslahi ya Imarati. Uhusiano wa Qatar na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na himaya na uungaji mkono wa Tehran kwa Doha katika miaka ya mizozo ndani ya mataifa ya Kiarabu umethibitisha kwamba, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran daima imekuwa ikiamiliana na majirani zake kwa msingi wa kuheshimiana pande mbili na kuna wakati ikilazimu basi hujitiokeza na kutetea usalama wao.
Nukta ya nne ni kuwa, kinyume na utendaji wa Imarati, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ikiwa nchi yenye nguvu na muhimu katika eneo hususan mkabala na mataifa jirani, siku zote imeonyesha hamu na shauku ya kustawisha uhusiano, na hili ndilo jambo lililosisitizwa na Hussein Amir-Abdollahian, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika mazungumzo yake na Saif Mohammed Al Zaabi, balozi wa Imarati hapa Iran. Abdollahiana amesisitiza katika mazungumzo hayo kwamba: Sisi tukizingatia sera za mhimilii wa ujirani, tumekuwa na hamu na shauku ya kupanua ushirikiano na majirani zetu wote ukiwemo Umoja wa Falme za Kiarabu.