Abbas Ali Kadkhodaei, mkuu wa kamati maalumu ya ufuatiliaji wa kisheria na kimataifa wa mauaji na kuuawa shahidi Kamanda Haj Qassem Soleimani amesema: Mauaji ya Shahidi Soleimani na wenzake yamesajiliwa katika duru za kimataifa kama uhalifu wa kimataifa wa Marekani.
Kadkhodaei ameongeza kuwa: “Marekani ilikiuka na kukanyaga majukumu yyake yote ya kimataifa kwa mauaji ya Haj Qassim, na jinai iliyofanywa na Wamarekani ilikuwa uhalifu wa kimataifa. Wamarekani walifanya uhalifu mkubwa kwa jinai hiyo.”
Mkuu wa kamati maalumu ya ufuatiliaji wa kisheria na kimataifa wa mauaji ya Kamanda Haj Qassem Soleimani ameongeza kuwa: “Baada ya uhalifu huo, taasisi mbalimbali zikiwemo Wizara ya Mambo ya Nje na Idara ya Mahakama zilichukua hatua nzuri, na waheshimiwa majaji wanafuatilia suala hili ili liwe na matokeo mazuri katika mtazamo wa kijinai”.
Mnamo Januari 3, 2020, kwa amri ya Donald Trump, rais wa wakati huo wa Merekani, ndege zisizo na rubani za jeshi la kigaidi la Marekani, lilishambulia msafara wa Meja Jenerali Qassem Soleimani, kamanda wa zamani Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu, aliyekuwa pamoja na Abu Mahdi Al-Muhandis, Naibu Mkuu wa zamani wa Kikosi cha Kujitolea cha Wananchi wa Iraq maarufu kwa jina la al Hashdu al Shaabi, na wenzao kadhaa na kuwaua shahidi karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Baghdad.
Kisingizio kilichotumiwa na Trump kuhalalisha kitendo hiki cha kihalifu ni madai kwamba Jenerali Soleimani aliingia Iraq kwa lengo la kupanga mashambulizi dhidi ya Wamarekani na vituo vyao, na kwamba mashambulizi ya anga ya Marekani yalikuwa hatua ya kujikinga. Hii ni licha ya kwamba madai hayo yamekadhibishwa hata na maafisa wa Marekani wenyewe. Ushahidi mwingi na kauli za maafisa wakuu wa Marekani zinaonyesha kwamba Washington ilichukua uamuzi huo miezi kadhaa kabla na ilikuwa ikisubiri fursa na wakati mwafaka wa kutekeleza mpango huo wa kihalifu.
Kituo cha habari cha Marekani cha NBC kiliripoti mnamo Januari 13, 2020 kwamba Donald Trump alikuwa ametoa amri ya masharti ya kuuawa kwa Jenerali Soleimani mnamo Juni 2019, yaani miezi 7 kabla ya kutekelezwa uhalifu huo. Washauri wa kijeshi na usalama wa Trump walikuwa wakiamini kwamba, kufuatana na kuwa pamoja Jenerali Soleimani na Abu Mahdi Al-Muhandis huko Baghdad, ambao walikuwa makamanda wakuu wa Iran na Iraqi waliokuwa na nafasi muhimu katika mapambano dhidi ya kundi la kigaidi la Daesh (ISIS), ambao pia walikuwa vikwazo vikubwa vya kufikiwa kwa malengo ya Marekani eneo la Asia Magharibi, ilikuwa fursa ambayo haikupaswa kupotezwa. Kwa utaratibu huo Wamarekani walifanya jinai kubwa kwa shambulizi hilo la kigaidi.
Kuhusu kisingizio kilichotumiwa na Trump kwa ajili ya kuamuru mauaji ya Jenerali Soleimani, Kadkhodaei anasema: Wamarekani hawakuwa na sababu yoyote ya kuhalalisha jinai hiyo, na hii leo imesajiliwa katika majukwaa ya kimataifa kwamba Wamarekani walitenda uhalifu mkubwa wa kimataifa kwa kitendo hiki cha kijinai.
Suala hili pia limesadikishwa na Umoja wa Mataifa. Agnès Callamard, Ripota Maalumu wa Umoja wa Mataifa, aliandika kuhusiana na suala hili kwamba: “Kisingizio kilichotumiwa na Marekani kuhalalisha mashambulizi ya ndege zake zisizo na rubani dhidi ya Jenerali Soleimani hakikuwa na ushahidi wowote wa kuwepo tishio linaloweza kutokea haraka.”
Suala jingine ni kwamba, Marekani ilimlenga afisa mkuu wa jeshi la Iran katika hatua ambayo haijawahi kushuhudiwa na kinyume kabisa na sheria za kimataifa, bila ya kuwepo tangazo la vita kati ya nchi hizo mbili. Kuhusiana na suala hilo Kadkhodaei anasema: “Kamanda Soleimani, kama afisa mkuu wa kijeshi wa nchi yetu ambaye alikuwa mgeni wa Iraq na shakhsia wa kimataifa, alipaswa kuheshimiwa na kupewa hadhi yake; na maafisa wa serikali ya Marekani walipaswa kuheshimu hadhi na nafasi yake, kinyume chake walitenda jinai dhidi ya jenerali huyo mpendwa na wenzake.” Ukweli huo pia umesisitizwa na Ripota Maalumu wa Umoja wa Mataifa, Agnès Callamard ambaye alilaani uhalifu huo akisema umekiuka sheria za kimataifa.
Callamard ameandika kwamba: “Mauaji yaliyofanywa na Marekani dhidi ya Jenerali Soleimani katika ardhi ya Iraq yalikuwa kesi ya kwanza ya aina hiyo na yalifanyika bila ya kuwepo tangazo la vita ambapo nchi moja iliishambulia nyingine kwa kisingizio cha kujihami…”
Msimamo huo wa wazi ya Ripota Maalumu wa Umoja wa Mataifa, Agnès Callamard kuhusu jinsi mauaji ya Jenerali Soleimani na wenzake yalivyokiuka sheria za kimataifa, haubakishi shaka kwamba Marekani ni miongoni mwa wavunjaji wakuu wa sheria za kimataifa. Kwa msingi huo mashtaka ya Iran dhidi ya serikali ya Washington yanapaswa kushughulikiwa katika mahakama za kimataifa.