Katika kipindi cha chini ya wiki mbili tokea lianze kazi baraza la mawaziri la serikali mpya ya utawala wa Kizayuni wa Israel inayoongozwa na Benjamin Netanyahu, ukosoaji dhidi ya baraza hilo umeshadidi kwa kiasi kikubwa na hata baadhi wameonya kuhusu uwezekano wa kuzuka vita vya wenyewe kwa wenyewe katika utawala huo.
Benjamin Netanyahu amerejea madarakani baada ya muda wa mwaka mmoja na nusu tu na tayari ameshaunda baraza jipya la mawaziri la utawala huo haramu. Pamoja na hayo, kuna uwezekano wa baraza hilo jipya la mawaziri kusambaratika baada ya muda usio mrefu. Wakosoaji wa baraza hilo wamelenga zaidi matamshi na sera zisizo na busara na za misimao mikali ya kufurutu ada za waziri wa usalama wa utawala huo.
Katika kipindi cha chini ya wiki mbili, Itamar Ben-Gvir amechukua maamuzi ambayo yamepelekea kujitokeza upinzani wa ndani na wa kimataifa dhidi ya baraza la mawaziri la Netanyahu.
Jumanne iliyopita, Ben-Gvir aliuhujumu Msikiti wa Al Aqsa katika mji wa Quds (Jerusalem) ambapo alivunjia heshima eneo hilo tukufu la Waislamu. Kitendo hicho kiliibua malalamiko makubwa kieneo na kimataifa na hata Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limelazimika kuitisha kikao cha dharura kuhusu uchaguzo huo. Baraza hilo limeitaka serikali ya Netanyahu kujizuia na vitendo vya kichochezi dhidi ya Wapalestina.
Ben-Gvir katika muendelezo wa maamuzi yake dhidi ya Wapalestina ametangaza kuwa vizingiti vikali zaidi vitawekwa dhidi ya mateka wa Kipalestina wanaoshikiliwa katika magereza ya Israel.
Mbali na Ben-Gvir, pia kuna Yariv Levin waziri wa sheria wa utawala wa Kizayuni wa Israel naye Jumatano iliyopita aliibua utata kwa kutangaza mabadiliko makubwa katika mfumo wa mahakama katika utawala huo. Kwa mujibu wa mabadiliko hayo, baraza la mawaziri la utawala wa Kizayuni litaweza kuchagua majaji. Uamuzi huo nao pia umekosolewa vikali sana.
Wakosoaji wa baraza la mawaziri la sasa la Israel wanaamini kuwa, maamuzi yenye utata yaliyochukuliwa na mawaziri hao wawili yaliidhinishwa na Netanyahu mwenyewe.
Yair Lapid, waziri mkuu wa zamani amemshambulia vikali Netanyahu kutokana na maamuzi hayo ya waziri wa sheria. Benny Gantz waziri wa zamani wa vita katika utawala wa Kizayuni wa Israel pia amekosoa vikali baraza la mawaziri la Netanyahu na kuongeza kuwa sera za baraza lake la mawaziri zitahatarisha mustakabali wa utawala huo. Aidha amemtuhumu Netanyahu kuwa anaanzisha vita vya ndani.
Baadhi ya wakosoaji wanasisitiza kuhusu nukta hii kwamba, hatua zenye utata za mawaziri wenye kufurutu ada wa Netanyahu zinaonyesha utambulisho halisi wa baraza hilo ambalo lina mawaziri dhaifu mno na wenye utata ambao hawastahiki kuwa madarakani.
Ehud Barak, waziri mkuu wa zamani wa utawala wa Kizayuni amesema hivi kuhusu baraza la mawaziri la Netanyahu. “Ni baraza la mawaziri la watu wenye kula rushwa ambapo pia ni dhaifu, wanyonyaji na wenye misimamo ya ubaguzi wa rangi. Waziri kama Ben-Gvir anataka kupata mlungula kutoka kwa Netanyahu.”
Kwa kuzingatia kushadidi ukosoaji dhidi ya Netanyahu, vyombo vya habari vya utawala wa Kizayuni vimeonya kuwa wenye misimamo mikali katika baraza la mawaziri la Israel watapalekea kuongezeka malalamiko na makabiliano baina ya raia na vikosi vya usalama. Netanyahu kwa upande wake amedai kuwa wapinzani wake wanahatarisha ‘demokrasia na uhuru’ katika utawala huo bandia. Inaelekea kuwa, matamshi hayo ya Netanyahu yanatokana na hofu yake kuhusu kusambaratika mapema baraza lake la mawaziri kwani hilo likijiri litakuwa ni pigo kubwa zaidi kwake kisiasa.