Ijumaa ya tarehe 21 Oktoba 2022, jeshi la Yemen lilitumia droni zake kushambulia bandari ya al Dabah huko Hadhramaut likiwa ni pigo jipya kwa wavamizi na onyo kwa madola vamizi yanayoongozwa na Saudi Arabia ambayo yanaendelea kupora utajiri wa nchi hiyo maskini zaidi ya Kiarabu.
Al Dabah ni bandari muhimu katika mkoa wa Hadhramaut wa mashariki mwa Yemen. Bandari hiyo inadhibitiwa na madola vamizi yanayoongozwa na Saudia na inatumiwa kupora utajiri wa nchi hiyo ya Waislamu.
Ijumaa usiku, Msemaji wa Jeshi la Yemen, Brigedia Jenerali Yahya Saree, alisema kuwa majeshi ya nchi hiyo yamefanya shambulio hilo kama onyo dogo tu ili kuwaambia wavamizi hao kuwa hawawezi kuruhusu utajiri wa Yemen uendelee kuporwa huku wananchi wenyewe wakiteseka tena kwa maafa yaliyosababishwa na madola hayo hayo vamizi.
Hatua ya jeshi la Yemen ya kushambulia bandari ya al Dabah ili kuzuia wizi wa mafuta ya nchi hiyo, ina umuhimu mkubwa katika pande kadhaa. Kwanza hii ni hatua ya kwanza ya jeshi la Yemen tangu baada ya kufeli usimamishaji vita. Tarehe pili mwezi huu wa Oktoba, usitishaji mapigano ulimaliza muda wake wa miezi sita na haukuongezewa muda. Serikai ya Saudia muda wote ilikuwa inapuuza vipengee vya makubaliano hayo na hilo linahesabiwa kuwa ndiyo sababu kuu ya kutoongezewa muda mapatano hayo. Wayemen walikuwa wanaonya mara kwa mara kwamba Wasaudia wanakanyaga makubaliano ya kusimamisha vita na kwamba matokeo ya jambo hilo ni mabaya. Hivyo shabulizi dhidi ya bandari ya al Dabah inayodhibitiwa na wavamizi wa Yemen, ni sehemu ya matokea mabaya ya kudharau Wasaudia makubaliano ya kusimamisha mapigano na kutoongezewa muda mapatano hayo.
Zaidi ya hayo ni kwamba, hatua hiyo ya jeshi la Yemen imechukuliwa ili kulinda utajiri na kuzuia kuporwa rasilimali za nchi hiyo. Meli moja kubwa liliingia kwenye bandari ya al Dabah kwa ajili ya kubeba mapipa milioni mbili ya wizi ya mafuta ya Yemen. Lakini ghafla moja jeshi la Yemen liliishambulia bandari hiyo na kulilazimisha meli hilo kukimbia.
Brigedia Jenerali Yahya Saree amesema kuhusu shambulizi hilo kwamba, meli hilo halikuheshimu amri ya kutopelekwa nje ya Yemen mafuta ya nchi hiyo bila ya utaratibu maalumu. Shambulio hilo ni onyo kwa yeyote anayekusudia kuuza kimagendo mafuta ya Yemen.
Nchi za Saudi Arabia na Muungano wa Falme za Kiarabu (Imarati) zinaendelea kupora utajiri wa nishati wa Yemen. Imarati ndiyo iliyojikita zaidi kwenye wizi huo kiasi kwamba hata imeuingiza utawala wa Kizayuni wa Israel kwenye uporaji wa maliasili za Yemen. Mkoa wa Hadhramaut ndio unaozalisha kwa wingi mafuta nchini Yemen. Mara kwa mara mamluki wa Saudia, Imarati na Marekani wamekuwa wakitwangana na kuuana kwenye mkoa huo kwa ajili ya kudibiti maenneo mengi zaidi yenye utajiri wa nishati. Hivi karibuni Wizara ya Mafuta ya Serikali ya Wokovu wa Kitaifa ya Yemen ilisema kuwa, muungano vamizi unaoongozwa na Saudi Arabia umeshaiba utajiri mwingi wa Yemen wenye thamani ya takriban dola bilioni 10. Hivyo shambulio la Wayemen kwenye bandari ya al Dabah inayodhibitiwa na madola vamizi, ni sawa na kutangaza kuwa, Wayemen kamwe hawezi kuendelea kuvumilia uporaji wa utajiri wao.
Nukta ya mwisho hapa ni kwamba, hatua ya Wayemen ya kushambulia bandari ya al Dabah ya mkoa wa Hadhramauti imeonesha kuwa, kama Wasaudia wametumia miezi 6 ya usimamishaji vita kujipanga upya kwa ajili ya vita vingine, hilo haliwazuii Wayemen kuingia tena vitani kuilinda nchi yao na utajiri wake. Hivyo shambulia hilo ni onyo la Wayemen kwa Riyadh na Abu Dhabi kuwa, majibu ya jeshi la nchi hiyo yatakuwa makali kwa wavamizi wa Yemen iwapo watachukua hatua yoyote ya kipuuzi. Vile vile shambulio kwenye bandari ya al Dabah limetoa onyo kwa mashirika ya Imarati, Saudia, Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel kuwa maeneo ya kusini na mashariki mwa Yemen si uwanja wa matembezi.
Brigedia Jenerali Yahya Saree amesema kwa kusisitiza kwamba, kwa mara nyingine tunatoa onyo kwa mashirika yote kuwa, yasipuuze misimamo ya San’a na yaache mara moja uporaji wa aina yoyote ile wa utajiri wa Yemen.