Wakati hali ya mchafukoge wa kisiasa kusini mwa Yemen ikiwa imefikia kiwango cha juu huku serikali tegemezi na kibaraka iliyoko huko ikiwa haina mamlaka yoyote ya uendeshaji wa mambo yake, katika njama iliyoratibiwa na Muungano wa Falme za Kiarabu Imarati, utawala haramu wa Kizayuni wa Israel umeshamirisha kuwepo kwake kijeshi katika eneo hilo la kusini mwa Yemen.
Kuwepo Wazayuni kusini mwa Yemen kulianza Septemba 2020 baada ya kufikiwa mapatano ya kuanzishwa uhusiano wa kawaida kati ya utawala haramu wa Israel na Imarati; na kadiri muda ulivyopita, ndivyo ulivyoshamiri na kupata nguvu zaidi. Kwanza kabisa Muungano wa Falme za Kiarabu (UAE) kwa kushirikiana na utawala wa Kizayuni zilifungua uwanja wa ndege katika kisiwa kidogo cha Abdul-Kuri kilichopo kwenye majimui ya visiwa vya Soqotra kusini mwa Yemen. Kufunguliwa kiwanja hicho hakukutilia maanani kupata ridhaa hata ya serikali ya Yemen iliyojiuzulu; na kimsingi ni kwamba kulifanyika bila ya kuishirikisha serikali hiyo. Kilichoendelea baada ya hapo ni utawala wa Kizayuni kupeleka idadi kadhaa ya wanajeshi na maafisa wake wa intelijensia kusini mwa Yemen na kufungua huko vituo kadhaa vya kijeshi.
Katika hatua nyingine mpya, duru za habari zimeripoti kuwa, Mahmoud Fat-h Alil-Khaajah, mmoja wa wahusika wakuu waliofanikisha mapatano kati ya Imarati na Israel, amenunua maeneo mengi ya ardhi katika sehemu ya milimani ya Hajar. Kwa mujibu wa duru hizo, lengo la Al-Khaajah ni kuanzisha kituo kingine kipya cha kijeshi kwa ajili ya utawala wa Kizayuni katika visiwa vya Soqotra. Eneo la Hajar linaelekeana na pwani ya Hudaybu.
Inasemekana kuwa, lengo hasa linalofuatiliwa na Wazayuni na Waimarati kusini mwa Yemen ni kuanzisha kituo kikuu cha kikanda cha ulinzi wa anga. Kuhusiana na suala hilo, mnamo mwezi Juni mwaka huu waziri wa vita wa utawala haramu wa Kizayuni wa Israel Benny Gantz alidai kuwa, wamo mbioni kuanzisha kituo kikuu cha kikanda cha ulinzi wa anga kitakachoitwa “muungano wa ulinzi wa anga wa Mashariki ya Kati”.
Hatua hiyo ya pamoja ya Imarati na utawala wa Kizayuni, mbali na kuwa ni mwendelezo wa ushirikiano wa pande mbili katika uga wa kijeshi na kiintelijensia, inachukuliwa pia kwa lengo la kuendeleza uporaji wa maliasili za Yemen. Maliasili za nishati za Yemen ziko kwenye maeneo ya kusini; na vilevile bandari za kistratejia ziko pia kusini mwa nchi hiyo.
Si hayo tu, lakini ushirikiano wa Imarati na utawala wa Kizayuni kusini mwa Yemen, ambao unafanyikka huku Saudi Arabia ikiwa na taarifa nao na inavyoonekana una baraka kamili za utawala wa Riyadh, unalenga pia kuigawanya Yemen vipande vipande. Siku zote utawala haramu wa Israel umekuwa ukikutazama kugawanyika kwa nchi za Kiislamu na kugeuzwa vijinchi vidogovidogo kuwa ni jambo linaloendana na maslahi yake, kwa sababu baadhi ya nchi ndogo za Kiarabu kama Imarati na Bahrain ndizo zilizokuwa mstari wa mbele kufikia mapatano na kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala huo haramu.
Nukta nyingine ni kwamba, kuwepo kijeshi utawala ghasibu wa Kizayuni wa Israel kusini mwa Yemen na kushamiri ushirikiano baina yake na Muungano wa Falme za Kiarabu Imarati kunalenga kukabiliana na kupanuka wigo wa mamlaka ya Serikali ya Uokovu wa Kitaifa ya Yemen katika maeneo ya kusini mwa nchi hiyo na kuzuia kuundwa serikali madhubuti na yenye nguvu nchini Yemen. Imarati imekusudia kuushirikisha utawala wa Kizayuni katika kufikia malengo yake, sambamba na kuvutia uungaji mkono wa nchi za Magharibi hususan Marekani katika suala hilo.
Kuhusiana na nukta hiyo, Waziri wa Ulinzi wa Serikali ya Uokovu wa Kitaifa ya Yemen Muhammad Nasir al-Atefi amedokeza kuwa, kuna njama na makubaliano rasmi ambayo yamepangwa kufikiwa baina ya nchi wavamizi, dhamira kuu ikiwa ni kuikabidhi Yemen kwa utawala haramu wa Kizayuni wa Israel na nchi zinazouunga mkono utawala huo dhalimu, mkabala wa nchi hizo vamizi kutimiziwa baadhi ya matakwa yao.