Nchi za Magharibi, kinyume na nara na kaulimbiu zao za kizandiki za kutetea utu na ahadi zao za kusimamia kidemokrasia, zimeshakiuka mara nyingi misingi hiyo; na sio tu haziwezi kuwavumilia wapinzani na wakosoaji wao, bali hutumia pia njia mbalimbali kuzima sauti zao au hata kuwamaliza moja kwa moja.
Kuhusiana na suala hilo, Rais Volodymyr Zelenskyy wa Ukraine, ametangaza kuwa ameamua kuwanyima haki za kiraia na kuwavua uraia wa nchi hiyo wanasiasa wanaoipinga serikali yake.
Zelenskyy amelibainisha hilo akisema: “kwa mujibu wa vipengee vilivyoainishwa na Shirika la Usalama la Ukraine na Shirika la Uhamiaji la Serikali ya Ukraine na kulingana na Katiba ya nchi yetu, nimeamua kubatilisha uraia wa watu wanne”.
Kabla ya hapo, Rais wa Ukraine alishasaini amri ya kuwapokonya uraia makasisi 13 wa Kanisa Othodoksi la Ukraine. Aliagiza pia afuatiliwe kisiasa mkuu wa baraza la kisiasa la chama cha upinzani kwa ajili ya maisha (OPZZH), ambacho kwa sasa kimepigwa marufuku nchini humo.
Serikali ya Ukraine, na hasa tokea ulipopamba moto mgogoro kati yake na Russia, imekuwa ikiwashinikiza na kuwanyanyasa vikali wapinzani wa vita na wa sera dhidi ya Russia, na licha ya kauli mbiu zote za nchi za Magharibi kuhusu kuheshimiwa na kuzingatiwa uhuru wa kisiasa na kijamii, imekuwa ikiwaandama wapinzani na hata kuwapokonya uraia.
Ripoti zilizotolewa zinaonyesha kuwa, hata katika vita vya Ukraine pia, makumi ya mateka wa vita wa Russia wameteswa na kunyanyaswa na vikosi vya jeshi la Ukraine. Hata hivyo vitendo hivyo sio tu havijachukuliwa na nchi za Magharibi kuwa ni uhalifu wa kivita na kulaaniwa, lakini nchi hizo zimeipatia fursa zaidi serikali ya Kyiv ya kuendeleza vitendo hivyo kwa kuiongezea misaada zaidi ya fedha na silaha.
Viongozi wa Ukraine hawajawahurumia pia hata askari wa nchi hiyo kwa kuwakamata na kuwaadhibu wale wanaokataa kwenda vitani.
Matilda Bogner, mkuu wa taasisi ya Umoja wa Mataifa ya uangalizi wa haki za binadamu nchini Ukraine, amesema kuhusiana na suala hilo: “kuna ripoti za kuaminika zinazoonyesha kuwa wanajeshi wa Ukraine wamewanyonga watu ambao hawakushiriki katika vita vya nchi hiyo, bila kufuata utaratibu wa kuwafungulia kesi. Aidha zimepokelewa taarifa kadhaa kuhusu mateso na unyanyasaji waliofanyiwa mateka wa vita na vikosi vya jeshi la Ukraine”.
Nchi za Magharibi zinaitetea Kyiv licha ya hatua zote hizo za serikali ya Zelenskyy za kukiuka na kutoheshimu kauli mbiu za haki za binadamu, na huku Ukraine ikiwa inavuma pia kwa ufisadi wa fedha na utakatishaji pesa. Ukweli ni kuwa, nchi za Magharibi zinaimwagia misaada ya fedha na silaha Ukraine, huku zikilifumbia macho suala la ufisadi uliorasimishwa nchini humo. Kiasi kwamba kitambo nyuma Victoria Spartz, mbunge wa chama cha Republican katika Baraza la Wawakilishi la Marekani, ambaye alizaliwa Ukraine na hapo kabla alikuwa muungaji mkono mkubwa wa sera ya kupeleka huko misaada ya silaha na fedha, sio tu amemkosoa rais wa nchi hiyo na wafuasi wake mafisadi na wabadhirifu, lakini pia ametaka kusitishwa misaada hiyo na kufuatiliwa kadhia hiyo ya ufisadi kwa uzito mkubwa.
Ripoti zilizotolewa zinaonyesha kuwa tokea mwaka 2012 hadi 2021 Ukraine imetajwa mara kadhaa katika orodha za kimataifa kuwa moja ya nchi fisadi zaidi barani Ulaya. Mnamo mwaka 2016, Mahakama ya Ukaguzi wa Hesabu ya Umoja wa Ulaya iliitangaza Ukraine kuwa nchi fisadi zaidi barani Ulaya. Na hii ni katika hali ambayo, moja ya kauli mbiu alizotumia rais wa sasa Volodymyr Zelenskyy wakati wa kampeni za uchaguzi ilikuwa ni kupambana na rushwa iliyokithiri, lakini kwa miezi kadhaa sasa, nchi za Magharibi zimekuwa zikiimiminia misaada ya fedha nchi hiyo, huku zikilipuuza suala hilo. Ukweli ni kuwa, kwa muda wa miezi kadhaa, suala la mageuzi ya muundo wa serikali na kupambana na rushwa nchini Ukraine limepuuzwa na kuwekwa pembeni kutokana na kuathiriwa na zogo la vita, mapigano na propaganda. Hivi sasa, viongozi wa Ukraine wameamua bila hofu yoyote kulipuuza pia suala la uhuru wa mtu binafsi na haki za binadamu kwa kuwapokonya uraia wapinzani, huku nchi za Ulaya nazo zikifadhilisha kunyamaza kimya na kuendelea kuipatia nchi hiyo msaada kwa ajili ya kudhamini maslahi yao.