Kutimia miaka 35 ya kuasisiwa HAMAS; mapambano na muqawama sambamba na siasa

Miaka 35 imepita tangu ilipoasisiwa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS. Harakati hiyo ya mapambano iliundwa katika Ukanda wa Gaza tarehe 14 Desemba 1987 na Sheikh Ahmad Yasin na viongozi kadhaa wa Ikhwanul-Muslimin.

Hamas ni moja ya makundi ya Palestina, ambayo baada ya kuasisiwa kwake, limetoa mchango mkubwa katika matukio ya nchi hiyo na katika eneo la Asia Magharibi pia. Harakati ya Hamas inaamini katika muqawama na mapambano na vilevile kushiriki katika masuala ya kisiasa. Harakati hiyo ni moja ya mavuguvugu yaliyoko mstari wa mbele katika kupambana na utawala dhalimu wa Kizayuni wa Israel na daima imekuwa ikiandamwa na visasi, hujuma na jinai za utawala huo haramu pamoja na washirika wake wa Magharibi na wa mrengo wa Waarabu wasaliti wafanya mapatano.

Mchango mkubwa na athirifu wa Hamas kwa muqawama na mapambano ya Palestina na katika eneo hili la Asia Magharibi umekuwa sababu ya kambi ya Magharibi na baadhi ya waitifaki wao kuiweka harakati hiyo ya muqawama kwenye orodha ya makundi ya kigaidi; ilhali Hamas ni mmoja wa wahanga wa ugaidi wa kiserikali unaofanywa na utawala bandia wa Israel, kwani viongozi na wanachama wake wengi wamekufa shahidi kwa kuuliwa kigaidi na utawala huo dhalimu. Sababu ya Hamas kuitwa kundi la kigaidi ni kuweza kutumia kisingizio hicho kuidhoofisha harakati hiyo na kuhalalisha sambamba na kuunga mkono jinai inazofanyiwa na utawala haramu wa Israel.

Lakini mbali na hayo, ndani ya nchi za Kiarabu pia hakuna mwafaka na msimamo mmoja kuhusiana na Hamas. Wakati baadhi ya nchi kama Saudi Arabia na Muungano wa Falme za Kiarabu, Imarati hazina uhusiano nayo wowote na zinafuata muelekeo wa kukabiliana nayo, nchi kama Qatar ina uhusiano mzuri na Hamas na inaiunga mkono harakati hiyo ya muqawama. Sababu ya Qatar kuiunga mkono Hamas ni mielekeo na ukuruba wa harakati hiyo na Ikhwanul-Muslimin. Lakini sababu kuu ya Saudia, Imarati na baadhi ya nchi zingine za Kiarabu kuwa na mtazamo hasi wa kukabiliana na Hamas ni nafasi ya harakati hiyo katika mhimili wa muqawama unaoongozwa na Iran, upinzani wake kwa msimamo wa kufanya mapatano na utawala wa Kizayuni na vilevile kukataa kufuata sera za kikanda za utawala wa Riyadh. Na ndio maana katika miaka ya karibuni wanachama wengi wa Hamas wamekamatwa na kufungwa jela nchini Saudi Arabia.

Suala jengine ni kwamba, mbali na Hamas kujishughulisha na harakati za kijeshi na kuchukua hatua za kuimarisha muqawama na mapambano ya silaha, inaamini pia katika mchakato wa uchaguzi na kushiriki katika mwenendo wa kisiasa huko Palestina. Ni katika muelekeo huo, ndio maana harakati hiyo ilishiriki uchaguzi wa mwaka 2005 wa  bunge la Palestina na kufanikiwa kunyakua viti vingi na hata kuunda serikali; hata hivyo baada ya kupita muda mfupi, Mamlaka ya Ndani ya Palestina ilikataa kulitambua Baraza la Mawaziri lililoundwa na Hamas na baada ya miezi 15, yaani mnamo mwezi Juni 2007, serikali ya Waziri Mkuu Ismail Haniya ikasambaratika.

Ushindi iliopata katika uchaguzi wa bunge wa mwaka 2005 ulithibitisha kuwa harakati ya Hamas ina uungaji mkono mkubwa wa wananchi ndani ya Palestina, na ndio maana tangu mwaka 2005 hadi sasa hakuna uchaguzi mwingine wowote uliofanyika huko Palestina. Sababu ni kuwa Mamlaka ya Ndani ya Palestina inahofu kuwa endapo itaitisha uchaguzi, itaiandalia mazingira Hamas ya kushinda tena na kuunda serikali mpya.

Ismail Haniya, Mkuu wa ofisi ya kisiasa ya Hamas, amenena yafuatayo katika hotuba aliyotoa kwa mnasaba wa kuadhimisha mwaka wa 35 wa kusisiwa harakati hiyo ya muqawama wa Kiislamu ya Palestina: “Hamas iliunganisha mapambano na siasa; na siasa haijawahi katu kuwa dhidi ya mkakati wa mapambano, kwa sababu hata wakati tuliposhinda uchaguzi na tukaunda serikali, tuliendeleza muqawama; na chini ya serikali ya Hamas, muqawama na mapambano yaliendelea kuwa imara zaidi siku baada ya siku, mpaka tukafika hatua ya kuunda jeshi la Qassam lililoongozwa na Muhammad Dhaif”.

Nukta nyingine muhimu kuhusu Hamas ni kwamba mikakati na stratejia zinazotumiwa na harakati hiyo katika kuihami Palestina na malengo yake matukufu ni muqawama na mapambano dhidi ya utawala wa Kizayuni, kutetea dhati na utambulisho wa Kipalestina wa Baitul Muqaddas na Msikiti wa Al Aqsa na kuwakomboa Wapalestina wanaoshikiliwa kwenye magereza ya Israel. Ni kwa sababu hiyo, Ismail Haniya amesisitiza kwamba, tangu kuasisiwa kwake, Hamas imekuwa thabiti katika misimamo yake ya kisiasa na mkakati wake uko wazi na wadhiha; na kwamba katu hayatafanyika mabadiliko yoyote katika misingi na misimamo yake na mbinu za mapambano ya kukabiliana na adui Mzayuni.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *