Kutimuliwa balozi wa Ufaransa Burkina Faso; pigo jengine kwa Paris

Msemaji wa serikali ya Burkina Faso Jean-Emmanuel Ouedraogo ametangaza kuwa balozi wa Ufaransa Luc Hallade ametakiwa aondoke nchini humo kufuatia kushadidi mgogoro kati ya nchi hizo mbili.

Ufaransa na Burkina Faso zimekuwa zikizozana tangu yalipotokea mapinduzi ya kijeshi nchini Burkina Faso Septemba 30 mwaka uliopita yaliyoongozwa na Ibrahim Traoré, kapteni wa jeshi mwenye umri wa miaka 34 na kupelekea kuondolewa madarakani Luteni Kanali Paul-Henri Sandaugo Damiba. Hayo yalikuwa mapinduzi ya pili ya kijeshi nchini Burkina Faso katika mwaka 2022, ambapo wafanyamapinduzi walichukua hatua ya kusimamisha katiba na kufunga mipaka ya nchi.

Maafisa wa Burkina Faso wanaituhumu Paris kuwa inaingilia masuala ya ndani ya nchi hiyo ikiwa ni pamoja na kumpatia hifadhi Damiba. Jean-Baptiste Cabret, msemaji wa jeshi la Burkina Faso, anasema kuhusiana na suala hilo: “Damiba amejaribu kurudi nyuma hadi kwenye kambi ya kijeshi ya Ufaransa ya Kamboinsin ili kujiandaa kwa ajili ya kuanzisha shambulio na kuchochea mgawanyiko kati ya vikosi vyetu vya ulinzi na vya usalama”.

Damiba alikuwa ameahidi kurejesha demokrasia na amani nchini Burkina Faso. Lakini kiuhalisia, hakuweza kuchukua hatua madhubuti katika kukabiliana na makundi ya kigaidi yaliyoko nchini humo, na kuifanya Burkina Faso igeuzwe kuwa uwanja wa harakati za makundi ya kigaidi ya Al-Qaeda na DAESH(ISIS), na harakati za makundi hayo kuenea na kuongezeka mpaka katika nchi jirani.

Hali hiyo inashuhudiwa, ilhali kwa muda wa miaka kadhaa sasa, Ufaransa imekuwepo barani Afrika kwa kisingizio cha kusaidia kupambana na ugaidi, huku ikiwa inaingilia kwa dhahiri na kwa kificho masuala ya kisiasa na kiuchumi ya nchi za bara hilo. Uingiliaji huo wa Ufaransa umekuwa sababu ya kuongezeka lawama na ukosoaji dhidi ya nchi hiyo hususan katika miaka ya hivi karibuni, baada ya Paris kushindwa kutekeleza ahadi na majukumu yake katika mapambano dhidi ya makundi ya wanamgambo na ya kigaidi. Kwa mujibu wa ripoti, tangu mwaka 2015, Burkina Faso imekuwa ikilengwa mara kwa mara na mashambulizi mbalimbali ya kigaidi, yaliyosababisha mamia ya watu kuuawa, huku wengine zaidi ya milioni moja na nusu wakilazimika kuwa wakimbizi ndani na nje ya nchi.

Katika miongo ya karibuni, Ufaransa imekuwa ikijiingiza kila mara na kupiga kambi katika nchi mbalimbali za Kiafrika kwa visingizio tofauti. Kwa hakika, bara la Afrika limekuwa na umuhimu maalumu kwa Ufaransa katika nyanja mbalimbali za kiuchumi na kijeshi. Kwa mfano, katika upande wa kiuchumi, hadi kabla ya mwaka 2020, makampuni ya Ufaransa yalikuwa yamehodhi takribani uzalishaji wote wa rasilimali za madini katika makoloni yake ya zamani kama vile Niger na Mali. Katika sekta ya kijeshi pia, vikosi vya Ufaransa vimekuwa vikitumwa kila mara na kusambazwa katika nchi tofauti za Afrika. Ufaransa ina hata vituo vya kijeshi katika nchi kama Mali, Niger, Ivory Coast, na Chad kwa kisingizio cha kusaidia kurejesha amani na utulivu na kupambana na ugaidi.

Ukweli ni kwamba, katika miongo ya karibuni, Ufaransa imeendelea kuwepo katika nchi za Kiafrika, lakini kwa sura ya ukoloni mamboleo; ukoloni ambao haulengi kuitawala nchi moja kwa moja, lakini unajikita katika uga wa kiuchumi kupitia utoaji misaada ya kifedha, mikopo ya muda mrefu na utekelezaji miradi ya kiuchumi na kibiashara. Kwa upande wa kisiasa pia, hatua ilizochukua Ufaransa zimezingatia kukidhi manufaa na maslahi yake tu kwa kutumia satua na ushawishi wake katika muundo wa madaraka wa nchi zilizokuwa makoloni yake.

Hata hivyo sera hii ya Ufaransa imekabiliwa na mkwamo kutokana na mwamko mkubwa yaliyopata mataifa ya Afrika katika miaka ya karibuni. Mataifa ya eneo hilo, hivi sasa hayakubali tena ushawishi na uingiliaji wa Ufaransa, kiasi kwamba hivi karibuni, Mali, ambayo inajulikana kama mmoja wa washirika muhimu zaidi wa Ufaransa barani Afrika, ilivunja uhusiano wake wa kisiasa na nchi hiyo kulalamikia utendaji wa Paris, ikamuondoa pia balozi wa Ufaransa na kuvitimua vikosi vya jeshi la nchi hiyo.
Katika muktadha huu, Kanali Maiga, Waziri Mkuu wa muda wa Mali, anasema: Viongozi wa Ufaransa wamezikana thamani za maadili ya kimataifa na kujigeuza serikali ya kijeshi inayotumikia tafakuri ya giza. Wanajikita katika nchi tofauti za Kiafrika kwa kutumia sera za ukoloni mamboleo, za udunishaji na uwekaji vikwazo.
Sasa hivi Burkina Faso imechukua hatua ya kumfukuza balozi wa Ufaransa nchini humo, tukio ambalo linaonyesha jinsi ushawishi wa Ufaransa katika kitovu cha bara la Afrika unavyoendelea kupungua
Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *