Kuvunja rekodi ya kunyonga Saudi Arabia katika uongozi wa Bin Salman

Mtandao wa Mirat al-Jazeera umetangaza kuwa, utawala wa Saudi Arabia umetoa hukumu ya mwisho ya wafungwa watano kwa sababu za kiitikadi.

Chombo hicho cha habari kimenukuu duru moja na kutangaza kuwa, utawala wa Riyadh umetoa hukumu ya kunyongwa Muhammad Ali al-Shiqaq, Mansur Samir al-Haik, Marzouk Muhammad Dhaif Aal Fadhl na Raad Muhammad Dhaif Aal Fadhl. Kutolewa hukumu dhidi ya wafungwa hao kunaifanya idadi ya watu wanaokabiliwa na hatari ya kunyongwa na utawala wa Sudia Arabia kufikia 63. Majuma machache yaliyopita pia, shirika moja la haki za binadamu lilitangaza habari ya kutolewa hukumu ya kunyongwa wanaharakati wengine sita katika nchi hiyo ambao ni Muhammad Al-Tahnoun, Mustafa Abu Shahin, Abdullah Ghazvi, Zuhair Al-Samkhan, Mohammed Al-Musabah na Radhi Al-Shayib. Hii ni katika hali ambayo, kabla ya hapo pia Kamati ya Kutetea Haki za Binadamu ya Bara Arabu ilitoa ripoti inayoeleza juu ya kutolewa hukumu ya kifo dhidi ya watoto ambao hawajafikisha umri wa kisheria.

Takwimu hizi zinaakisi ukweli mchungu hasa kwa kutilia maanani kwamba, hukumu za kunyongwa wanaharakati nchini Saudi Arabia zinatolewa katika anga ya kimya cha jamii ya kimataifa huku suala la kunyonga vijana wadogo likiwa limegeuka na kuwa jambo la kawaida na la kila siku.

Katika kipindi cha miaka kumi iliyopita, Saudia imevunja rekodi ya kunyonga watu. Hii ni katika hali ambayo, kuanzia mwaka 2013 hadi Oktoba mwaka huu jumla ya watu 1100 wamenyongwa nchini Saudia huku zaidi ya matukio 990 ya unyogaji huo yakifanyika katika kipindi cha utawala wa Mfalme Salman bin Abdul-Aziz kuanzia mwanzoni mwa mwaka 2015.

Ripoti za wataalamu wa mambo zinaonyesha kuwa, kabla ya mrithi wa kiti cha ufalme wa nchi hiyo Muhammad bin Salman kushika hatamu za uongozi Saudia ilikuwa nchi ya ukandamizaji; lakini baada ya mwanamfalme huo kuchukua usukani wa uongozi mwenendo wa ukandamizaji umeshadidi katika nchi hiyo kwa kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa. Hali hii imekuwa mbaya zaidi kiasi kwamba, kila anayeukosoa utawala huo au kutetea haki zake hutiwa mbaroni na kuandamwa na mateso makali sambamba na kushikiliwa mahabusu kwa muda mrefu.

Katika kipindi cha miaka miwili iliyopita Saudia imeshadidisha mno ukandamizaji dhidi ya wanaharakati wa nchi hiyo katika anga ya kimya cha jamii ya kimataifa. Hali hii imeifanya nchi hiyo inayotawaliwa kwa mfumo wa kifalme kugeuka na kuwa moja ya wakiukaji wakubwa zaidi wa haki za binadamu duniani.

Licha ya kuwa katika tawala za hapo kabla kulikuweko na ukandamizaji nchini Saudia lakini katika zama za utawala wa Muhammad bin Salman, mrithi wa kiti cha ufalme wa nchi hiyo hali hiyo imekithiri mno kiasi kwamba, kila anayepinga sera na siasa zake hukandamizwa na kuteswa vibaya.

Takwimu kuhusiana na idadi hasa ya wafungwa wa uhuru wa kujieleza wanaoshikiliwa katika magereza ya utawala wa Aal Saud zinatofautiana ingawa takwimu za karibuni zinaonyesha kuwa, kuna wafungwa wa kisiasa 2,613 kutoka katika matabaka na makundi yote ambao wanashikiliwa katika magereza mbalimbali ya utawala wa Aal Saud.

Wanaharakati wa Saudia wanaamini kwamba, takwimu hizi zinahusiana na watu ambao walitiwa mbaroni kuanzia Septemba 2017. Hii ni kutokana na kuwa, idadi ya watu waliotiwa mbaroni iliongezeka baada ya Muhammad bin Salman kuingia madarakani Juni 2017. Magereza ya utawala wa Aal Saudia yamegeuka na kuwa makuburi ya umati tangu bin Salman aingie madarakani; kwani kila anayetiwa katika magereza hayo hukabiliwa na mateso ya kutisha na hata kuaga dunia, kama ilivyotokea kwa Fahd al-Qadhi, Sheikh Suleiman al-Dowaish, Ahmad al-Amiri, Turk al-Jassir na Ali al-Qahtani ambao waliaga dunia wakiwa gerezani kutokana na uzembe wa makusudi wa kimatibabu.

Aidha kuna dhana kwamba, idadi nyingine ya wafungwa waliopoteza maisha yao kwa mateso wakiwa gerezani lakini viongozi wa utawala wa kiimla wa Saudia wanaficha taarifa za vifo hivyo. Kile kilichotangazwa na jumuiya za kutetea haki za binadamu kuhusiana na faili la wanaoshikiliwa magerezabni nchini Saudia kinaonyesha kuwa, wafungwa hao wanaishi katika mazingira ya masaibu na hali mbaya mno.

Siasa za ukandamizaji za utawala wa Saudia zikiongozwa na unyongaji kiholela haziishi tu kwa tabaka maalumu. Licha ya kuwa huko nyuma Waislamu wa madhehebu ya Mashia ndio waliokuwa katika hatari ya siasa hizi, lakini filihali na baada ya kuingia madarakani Muhammad bin Salman inawezekana kusema kuwa, wigo wa siasa hizo za ukandamizaji umepanuka na kuwaandama hata Waislamu wa madhehebu ya Suni. Aidha wigo huo umetanuka zaidi na kufika mpaka ndani ya familia ya ukoo wa Aal Saud.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *