Bunge la Kuwait kwa mara nyingine limechukua hatua inayoashiria msimamo usiotetereka wa nchi hiyo kuhusiana na Palestina, na sasa linaandaa mpango wa kisheria wa kufanya kuwa jinai mpango wowote wa kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel.
Abdullah Al-Mousawi, mtafiti wa masuala ya Palestina amenukuliwa na shirika la habari la Iran Press akisema kuwa, “Kundi la Wabunge wa Kuwait limeandaa muswada wa sheria itakayojinaisha uhusiano na utawala wa Israel.”
Ameongeza kuwa, “Baada ya kupasishwa na kuwa sheria, juhudi yoyote ya kuanzisha uhusiano na utawala huo katika uga wowote ule itatazamwa kama jinai, na kitendo kama hicho kitachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.”
Haya yanajiri siku chache baada ya Wabunge hao sambamba na kutangaza upinzani wao kwa hatua yoyote ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel, walisisitiza himaya na uungaji mkono wao kwa taifa la Palestina
Taarifa ya Wabunge hao ilitolewa kwa mnasaba wa Siku ya Kimataifa ya Kuonesha Mshikamano na Wapalestina iliyoadhimishwa Novemba 29 na kusisitiza juu ya udharura wa kuongezwa himaya na uungaji mkono kwa muqawama na mapambano ya Palestina.
Wabunge wa Kuwait wamesisitiza katika taarifa yao pia kwamba, kuna haja kwa viongozi wa utawala ghasibu wa Israel kupandishwa kizimbani katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) kutokana na kutenda jinai za kivita huko Palestina.
Sehemu nyingine ya taarifa ya Wabunge wa Kuwait ilisisitiza kwamba, Wapalestina wana haki ya kuendesha mapambano dhidi ya maghasibu wa Wazayuni mpaka haki zao zilizoghusubiwa zitakaporejeshwa na kwamba, hilo ni katika matakwa ya kimsingi ya serikali na wananchi wa Kuwait.