Kuwait: Tutaendelea kuisusia Israeli na makampuni yanayoshirikiana nayo

Kuwait imetangaza kuwa itaendelea kuisusia Israel, bidhaa zake na makampuni yanayoshirikiana nayo. Hayo yametangazwa katika Mkutano wa Maafisa wa Ofisi za Kikanda za Kuisusia Israel.

Shirika la Habari la Kuwait (KUNA) lilimnukuu mwakilishi wa Kuwait katika mkutano huo, Mashari Al-Jarallah, akisema, “Bidhaa zote ambazo zinashukiwa kuwa za Israeli au za kampuni zilizopigwa marufuku, zinachukuliwa hatua na kutaifishwa kulingana na maagizo ya Mkurugenzi wa Idara Kuu wa Forodha.”

Amesema kuwa sheria za kususia bidhaa za Israel ni chombo cha kuushinikiza utawala huo wa Kizayuni, akisisitiza umuhimu wa nchi nyingine za Kiarabu kuendelea kutekeleza maamuzi na mapendekezo yaliyotolewa na mkutano huo.

Kuwait ni miongoni mwa nchi chache za Kiarabu ambazo zimekuwa mstari wa mbele katika kuwatetea Wapalestina na mapambano yao ya uhuru dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel.

Mapema mwaka huu Spika wa Bunge la Kuwait alikosoa sera za undukumakuwili za Jamii ya Kimataifa kuhusu utawala haramu wa Israel na kutaka ujumbe wa utawala huo utimuliwe katika kikao cha Umoja wa Kimataifa wa Mabunge.

Vilevile Kinyume na baadhi ya watawala wa nchi za Kiarabu wanaokimbilia kufanya mapatano na utawala ghasibu wa Israel, Kuwait inafuata sera ya kupinga uamuzi wa kuanzisha uhusiano wa kawaida na Israel.

Tarehe 7 Aprili wizara ya habari ya Kuwait ilizuia rasmi kuonyeshwa nchini humo filamu ya Kifo Kwenye Nile (Death on the Nile) kwa sababu nyota mwanamke wa filamu hiyo ni askari wa zamani wa jeshi la utawala haramu wa Israel.

Halikadhalika, mwezi machi mwaka huu, wasomi wa vyuo vikuu vya Kuwait walitangaza kususia kongamano lililokuwa limeandaliwa na Chuo Kikuu cha Bahrain baada ya kubainika kuwa ujumbe kutoka utawala haramu Israel umealikwa kushiriki kongamano hilo.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *