Gazeti la Times la Uingereza limeripoti kuwa, utumwa mamboleo ungalipo nchini Saudi Arabia licha ya maonyo ya asasi na jumuiya za kimataifa.
Katika ripoti yake inayozungumzia uwepo wa utumwa mamboleo, kazi za kulazimishwa na ubakaji nchini Saudi Arabia, gazeti la Times limeandika kuwa, baadhi ya wafanyabiashara haramu ya binadamu nchini Saudi Arabia wanawaadhibu wafanyakazi wao kwa kuwapiga na kuwatesa.
Ripoti ya gazeti la Times inasema, takribani wanaume na wanawake milioni nne wanaofanya kazi za nyumbani, kilimo au udereva nchini Saudi Arabia wamewekewa vikwazo vya aina mbalimbali, na waajiri wao wamewapokonya pasi zao za kusafiria.
Ripoti hiyo inasema: Nchini Saudi Arabia, wafanyakazi wa kigeni kwa namna fulani wako chini ya usimamizi na udhibiti wa waajiri wao, kwa kadiri kwamba raia wa Saudia ni sawa na wamiliki wa mfanyakazi huyo na ndio wanaoamua aina ya mkataba na masharti ya visa yake.
Wafanyakazi hao wameingia nchini Saudi Arabia wakitokea mashariki mwa Asia, Pakistan na katika mataifa ya Kiafrika. Mtazamo ambao Saudi Arabia inao kwa wafanyakazi wa kigeni ni wa kudhalilisha na kudunisha. Licha ya kuwa mwaka 1967 utumwa ulipigwa marufuku rasmi nchini Saudia, lakini akthari ya wafanyakazi wa kigeni katika nchi hiyo filihali wanaishi maisha ambayo yanashabihiana kabisa na watumwa. Ripoti mbalimbali zinaonyesha kuwa, wafanyakazi wa kigeni katika nchi hiyo wanataabika kwa matatizo mengi kama kufanyishwa na kutumikwa kazi kupita kiasi, kuchoka, kuteswa na hata kunyimwa maji na chakula.
Mbali na mateso hayo, wafanyakazi wa kike wanakabiliwa na vitendo vya kubakwa. Fauka ya hayo, mkabala na kazi kubwa wanazofanya, wafanyakazi wa kigeni wanalipwa ujira na mshahara mdogo mno ikilinganishwa na wenzao wa Saudia. Waajiri wanawalipa wafanyakazi hao dola 6 tu mkabala wa kufanya kazi kwa takriban saa 24 kwa siku.
Wakati huo huo, biashara ya kuuza na kununua wafanyakazi nchini Saudi Arabia imepamba moto kiasi kwamba, kumebuniwa aplikesheni maalumu ya biashara hiyo. Gazeti la Times limeandika, aplikesheni ya al-Haraj ambayo inahesabiwa kuwa soko kubwa zaidi za kuuza bidhaa kwa njia ya mawasiliano ya internet nchini Saudi Arabia, kila siku imekuwa ikishuhudia makumi ya matangazo ya raia wa nchi hiyo ya kuuza na kukodi wahudumu wa kazi za nyumbani, ambayo yanajumuisha kuuza au kukodisha mahadimu wa kazi za ndani, wauguzi, madereva watunza bustani na kadhalika.
Biashara ya kuuza na kununua wafanyakazi wa kigeni imekolea mno nchini Saudia kiasi kwamba, kuna soko la magendo nchini humo. Baadhi ya raia wa Saudia wametangaza kuwa, wamekuwa wakilazimika kuwauza wafanyakazi wao kwa bei ya kutupa kutokana na kuwa, hawana utendaji wenye ufanisi na watoto au hawana uwezo wa kuzungumza lugha ya Kiarabu au Kiingereza na hivyo inawawia vigumu kuwasiliana na watoto.
Hali mbaya wanayokabiliwa nayo wafanyakazi wa kigeni nchini Saudi Arabia imekabiliwa na ukosoaji mkubwa wa asasi za kimataifa. Hivi karibuni Shirika la Msamaha Duniani la Amnesty International sanjari na kuulaani utawala wa Saudia kutokana na kukiuka wazi haki za binadamu, lilionyesha wasiwasi mkubwa lilionao kuhusiana na hali ya wahajiri nchini humo. Sehemu moja ya ripoti hiyo ilieleza: Wahajiri nchini Saudia wanafungwa kiholela, kesi zao zinaendeshwa kidhulma na wamekuwa wakiteswa na kufanyiwa vitendo visivyo vya kibinadamu.
Asasi hiyo inaituhumu Saudia kwamba, ikitegemea utajiri wa mafuta imekuwa ikizuia kufanyika uchunguzi kuhusiana na hali ya haki za binadamu katika nchi hiyo. Kimsingi tunaweza kusema kuwa, vyanzo vya utajiri wa kiuchumi vya Wasaudia ndio sababu ya kutokea utumwa mamboleo katika nchi hiyo inayoandamwa kwa kukiuka haki za binadamu.