Kuzingirwa Nablus, ishara ya utawala wa Kizayuni kushindwa kuzima mapambano ya Palestina

Katika kuendeleza harakati zao za chuki dhidi ya Wapalestina, askari wa utawala haramu wa Israel wamekuwa wakiuzingira kwa muda sasa mji wa Nablus, kaskazini mwa Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na kusababisha usumbufu mkubwa kwa wakazi wa mji huo.

Siku 17 zimepita tangu kuzingirwa mji huo na askari wa utawala unaokaliwa kwa mabavu mji mtakatifu wa Quds (Jerusalem). Utawala wa Kizayuni umeuweka mji wa Nablus chini ya mzingiro mkali kwa kisingizio cha kupanua operesheni zake dhidi ya wanamapambano wa Kiapalestina katika eneo hilo na  hasa uwepo wa wanachama wa kundi la mapambano la Arin al-Usud au ‘Pango la Simba’ katika mji huo. Jumanne asubuhi, vikosi maalumu vya utawala wa Kizayuni viliushambulia mji wa Nablus na kuua Wapalestina wasiopungua watano, wawili kati yao wakiwa ni makamanda wa Arin al-Usud. Kwa hivyo, sababu kuu ya kuzingirwa Nablus ni kukabiliana na uwepo wa shughuli za kundi la Arin al-Usud katika mji huo.

Kuanzishwa kundi hilo jipya katika mji wa Nablus katika kipindi cha miezi miwili iliyopita kumeufanya utawala wa Kizayuni uingiwe na hofu kubwa kuhusu kuimarika mapambano ya Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na kutobanwa mapambano hayo katika Ukanda wa Gaza pekee. Kuanzishwa kundi hilo kunaonyesha wazi kuwa mapambano ya Wapalestina yamevuka mipaka ya Ukanda wa Gaza na kuenea katika maeneo mengine ya Palestina yanayokaliwa kwa mabavu na utawala ghasibu wa Israel. Arin al-Usud ni kundi la mapambano la vijana wa Kipalestina ambalo liliundwa karibuni mjini Nablus na viunga vyake kwa ajili ya kukabiliana na jinai za askari na walowezi wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina, na linawalenga hasa askari na walowezi wa Kizayuni.

Elon Ben David, ripota wa gazeti la lugha ya Kiebrania la Ma’ariv anasema kuhusiana na suala hilo kuwa, kundi la Arin al-Usud huko Nablus si tu kwamba limeweza kufanya mashambulizi na operesheni kali dhidi ya Waisraeli, bali linawahamasisha Wapalestina wengine huko katika Ukingo wa Magharibi na hata Quds Tukufu kufanya operesheni dhidi ya Wazayuni. Anasema kundi hilo limekuwa kundi muhimu la mapambano ndani ya muda mfupi, kiasi kwamba operesheni zake zimekuwa athirifu zaidi kuliko makundi mengine mashuhuri ya mapambano, na hivyo kuwa tishio kubwa kwa uwepo wa utawala wa Israel.

Utawala wa Kizayuni ambao umekuwa ukitekeleza mzingiro wa pande zote dhidi ya Ukanda wa Gaza tangu 2006, sasa umeiweka Nablus katika mzingiro wa kukabiliana na Arin al-Usud. Kwa kuizingira Nablus, jeshi la Israel limewawekea mashinikizo makali wakazi wa mji huo ili kuwatisha wasijiunge wala kuyaunga mkono makundi ya mapambano. Utawala huo unashinikiza na kuwakandamiza Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan huku jamii ya kimataifa ikiwa imenyamaza kimya na Ulaya kushughulishwa na maandamano ya raia wanaopigania haki zao. Kama tunavyoshuhudia kuwa chini ya kimya hicho kinachoandamana na uungaji mkono wa nchi za Magharibi, Ukanda wa Gaza umekuwa chini ya mzingiro mkali wa utawala wa kigaidi wa Israel kwa muda wa miaka 16 na hivyo kuufanya ukanda huo kuwa jela kubwa zaidi ya wazi duniani.

Kuzingirwa Nablus kabla ya jambo lolote lile kunaonyesha wazi kushindwa utawala ghasibu wa Israel katika kukabiliana na wimbi jipya la mapambano ya Wapalestina. Akigusia wimbi hilo jipya la mapambano katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, Ziad an-Nakhaleh, Katibu Mkuu wa Harakati ya Jihad Islami ya Palestina anasema kuwa mzingiro wa Nablus unaonyesha kushindwa Israel kukabiliana na wimbi hilo.

Nukta nyingine ni kwamba; jamii ya kimataifa imenyamaza kimya kuhusiana na mzingiro wa Nablus, huku jinai inayotekelezwa na utawala wa Kizayuni katika eneo hilo ukiwa ni mfano wa wazi wa kutekelezwa adhabu ya pamoja dhidi ya wakazi wa mji huo wasio na hatia yoyote. Hazem Qassim, Msemaji wa Harakati ya Hamas amesisitiza kuwa, kuendelea mzingiro huo kuna maana ya kutekelezwa adhabu ya pamoja dhidi ya wakaazi wa Nablus na kuitaja kuwa ni ishara ya kushindwa mbinu za usalama za utawala huo katika kukabiliana na Intifadha ya Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi.

 

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *